Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga uzio katika Kituo cha Afya cha Uru Kusini - Moshi Vijijini?

Supplementary Question 1

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nitakuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza. Lakini kabla ya hapo, naomba kutoa pole kwa Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Jimbo la Moshi Vijijini, Kata ya Mbokomu ambao wamepata maafa ya mvua na nyumba zaidi ya 100 haziwezi kukalika tena na vifo vya watu watatu na majeruhi wako katika Hospitali ya KCMC. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; ameongelea Kituo cha Uru Kusini, lakini adha hii ipo katika Kituo cha Uru Kaskazini, Uru Mashariki na Okaoni. Ni lini Serikali itakwenda kujenga uzio katika vituo hivi ili kunusuru majengo yasiharibiwe na mvua hizi zinazonyesha?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika Kituo hicho hicho cha Uru Kusini kuna shida ya watumishi: watumishi waliopo leo ni 16, lakini wanaohitajika ni watumishi 50, kwa hiyo, kuna shida sana ya watumishi. Ni lini Serikali itaongeza watumishi katika kituo hiki ili kupata ufanisi? Ahsante. (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na uzio katika vituo vya afya ili kuboresha usalama wa wagonjwa na watumishi, lakini pia mali za Serikali katika vituo hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa utoaji huduma kwa wananchi, Serikali iliweka kipaumbele katika kukamilisha miundombinu ya vituo ili viweze kuanza kutoa huduma, kabla ya kuendelea na hatua ya ujenzi wa uzio. Kwa hiyo, ninafahamu kwamba tunahitaji uzio katika Kituo cha Afya cha Uru Mashariki, Kaskazini na hicho kingine ambacho amekitaja. Ninapenda kumhakikishia kwamba, Serikali itaendelea kupanga bajeti kwa awamu kwa ajili ya kujenga uzio katika vituo hivyo na tutahakikisha tunakamilisha pia ujenzi wa miundombinu mingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu watumishi, Serikali hii ya Awamu ya Sita kwa miaka hii minne imeajiri watumishi wa sekta ya afya 34,720. Haijawahi kutokea katika historia ya nchi hii katika miaka minne kuajiri watumishi wengi kiasi hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, watumishi hawa wanaendelea kuongezeka sambamba na upanuzi wa miundombinu ya sekta ya afya, ikijumuisha ujenzi wa vituo vya afya, zahanati, na hospitali za halmashauri. Ninapenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kutenga bajeti na kutoa vibali vya ajira na kutoa kipaumbele kwenye Kituo cha Afya cha Uru Kusini. Ahsante.

Name

Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga uzio katika Kituo cha Afya cha Uru Kusini - Moshi Vijijini?

Supplementary Question 2

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa kuwa, Zahanati ya Rononi kule Uru Kaskazini ina hali mbaya sana na miundombinu aliyosema kwamba Serikali inakamilisha haijawahi kukamilisha kwani haina vyoo kabisa, wala samani za ndani, hakuna mabenchi ya wagonjwa kusubiri. Ni lini sasa Serikali itatoa kipaumbele kwa Zahanati hiyo ya Rononi? (Makofi)

Name

Dr. Festo John Dugange

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, Serikali ilifanya mpango mkakati wa ukarabati na upanuzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali za halmashauri kongwe. Tayari tumeanza na hospitali za halmashauri, tutakwenda vituo vya afya kongwe na baadaye tutakwenda zahanati chakavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kumkumbusha Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kwamba ni wajibu wake suala kama la mabenchi na viti vya ndani ya zahanati viko ndani ya uwezo wa mkurugenzi wa halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninatoa maelekezo haya kwa Mkurugenzi, kwa haraka iwezekanavyo waende kwanza wakafanye tathmini ya uhitaji wa ukarabati wa zahanati hiyo na watenge fedha kupitia mapato ya ndani kwa sababu ipo ndani ya uwezo wao. Wanunue viti na mabenchi kwa ajili ya huduma za wagonjwa ili huduma katika zahanati hiyo ziweze kuboreshwa zaidi. Ahsante sana. (Makofi)