Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Primary Question

MHE. DESDERIUS J. MIPATA aliuliza:- Vijiji vya Sintali, Nkana, Nkomachindo na Katani viko kwenye mpango wa kupata umeme wa REA Awamu ya III lakini mpaka sasa hakuna kazi zinazoendelea:- Je, ni lini kazi hiyo itaanza?

Supplementary Question 1

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza vijiji nilivyovitaja vya Katani, Sintali, Nkana na Nkomachindo niseme na Malongwe pamoja na Wapembe nimeuliza kwenye swali la msingi ni lini hasa vitapata umeme? Hapa amesema viatapata kwenye mzunguko wa pili ambao utaisha mwaka 2021 na utaanza mwezi Julai mwaka huu. Sasa ni lini hasa nataka kujua kwa sababu wananchi wa maeneo haya wamezungukwa na maeneo ya umeme?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili vijiji vya Kipande, Kundi kuna sekondari zetu lakini sekondari zote hazijaunganishwa na umeme, pia Kijiji cha Ntemba ambako kuna umeme unapelekwa safari hii hatua chache kama kilometa nne kuna Chuo cha Ufundi cha Mvima na kuna pia Kituo cha Afya cha Mvima. Mheshimiwa Naibu Waziri alipokuja walitoa ombi la kuunganishiwa umeme na hadharani tulikubali kwamba tutawaunganishia umeme. Ni lini katika maeneo haya huduma za jamii yatapata umeme?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nilifanya naye ziara katika Jimbo la Nkasi Kusini na maeneo aliyoyataja hayo tulitembea kwa pamoja. Lakini nataka niseme kwamba katika swali lake la msingi kwa vijiji alivyovitaja ikiwemo cha Wampembe anaulizia ni lini hasa umeme utawaka. Kama ambavyo tumejieleza katika jibu la msingi kwamba mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili unatarajiwa kuanza tarehe 01 Julai, 2019 na kwa kuwa leo ni bajeti yetu nimwombe Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako tukufu liridhie bajeti hii ili tuanze kutekeleza mradi huu na kwa kuwa hatua za awali zimeshafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anaulizia umeme ambao unapelekwa katika Kijiji cha Ntemba ambako mita chache kuna Kituo cha Ufundi na Kituo cha Afya, ni kweli nilivyofanya ziara katika eneo lake jambo hili lilijitokeza na kwa kuwa ni sera ya Serikali ya Awamu ya Tano kwamba maeneo yote ya huduma za jamii ikiwemo vyuo, shule za sekondari na vituo vya afya vipatiwe umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kusisitiza ahadi hii ipo na kwamba eneo hili litapatiwa umeme na kama alivyosema Mheshimiwa Waziri katika majibu ya nyongeza kwamba tumeelekeza TANESCO kufikisha umeme katika taasisi mbalimbali na kazi hiyo inaendelea. Ahsante.