Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Primary Question

MHE. FRANCIS I. MTINGA K.n.y. MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza: - Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya mchepuko kutoka Kisaki – Unyamikumbi - Unyambwa hadi Mtipa?

Supplementary Question 1

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Manispaa ya Singida ipo katikati ya nchi na malori kutoka upande wa nchi yanapita pale; je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kuwahisha ujenzi wa bypass hii ili kuondoa msongamano unaokua kwa kasi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Wakati wenzetu wanaongelea Bypass, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama haina hata mita moja ya lami; na kwa kuwa, upembuzi yakinifu wa barabara ya Simiyu – Singida umekamilika: Serikali haioni haja katika bajeti hii kutenga walau kilometa 20 Makao Makuu ya Halmashauri ya Mkalama? Ahsante.

Name

Eng. Godfrey Msongwe Kasekenya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ileje

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Francis Mtinga, Mbunge wa Mkalama, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Singida kuna traffic kubwa. Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba tumekamilisha mwaka 2022 kufanya usanifu na tunavyoongea sasa hivi, tayari tumeshafanya tathmini ya wale watakaofidiwa kupisha barabara; na Serikali inaandaa malipo kwa ajili ya kuwafidia hawa watu watakaopisha barabara. Kwa hiyo, tunataka tumhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Singida kwamba, Serikali imedhamiria kwa dhati kujenga hiyo bypass.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tunatambua kwamba barabara aliyoitaja ni muhimu sana ambayo pia ni kutoka Singida kwenda Sibiti hadi Bariadi. Naomba pia, avute Subira, tuone kwenye bajeti hii inayokuja tumetenga nini? Ahsante.