Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Mbozi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nichangie ukurasa ule wa nane na wa 17 wa hotuba ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa ule wa nane hotuba ya Mhesimiwa Rais imegusa suala la walimu pamoja na malalamiko yao kwamba wana malalamiko. Ni kweli kabisa kwamba suala hili ni suala ambalo lipo. Walimu wana malalamiko kwamba hawana nyumba, lakini pia imefika mahali wana madai ya muda mrefu sana. Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali ya awamu ya tano ambayo ina slogan ya Hapa Kazi Tu; kama kweli itakwenda kujenga nyumba za walimu, italipa madeni sugu ya walimu ya muda mrefu sana, nadhani nchi hii kweli itakwenda, kwa sababu awamu zote zilizopita wote hawakuona umuhimu wa kuwalipa walimu madeni na kuwajengea nyumba bora. Kwa hiyo, nadhani Serikali hii ikifanya hivyo mambo yatakwenda vizuri kabisa. Mheshimiwa Naibu Spika, natoa mfano mdogo. Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi hivi ninavyozungumza inaonekana kwamba walimu waliosimamia mtihani wa kidato wa cha nne mwaka 2014 hawajalipwa fedha zao; na sio walimu tu lakini pia na Watumishi mbalimbali wa Halmashauri wakiwepo askari na madereva. Kwa hiyo, naomba katika haya maneno aliyoyazungumza Mheshimiwa Rais muweze pia kuliangalia hili. Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani kabisa kwamba Serikali yoyote ambayo iko makini inafika mahali deni la mwaka wa jana halijalipwa, lakini leo sina uhakika sana kama sisi Wabunge kuna Mbunge ambaye anaweza akawa anadai deni la mwaka wa jana au mwaka wa juzi. Inawezekana walimu wamesahaulika sana katika Taifa hili, ndiyo maana tunafikia hali kama hii. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba walimu wakumbukwe na deni hili lilipwe kwa kweli;
walimu wa Halmashauri ya Mbozi na walimu wengine wowote wanaoidai Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichangie ukurasa ule wa 17. Wakulima imefika mahali wana malalamiko makubwa sana. Mheshimiwa Rais alipokuwa akilihutubia Bunge, alisema atawasaidia wakulima, ataondoa ushuru wa kwenye mazao. Kwa mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi tunalima sana kahawa, wakulima wana shida kubwa sana, wanatozwa ushuru wa kahawa 5%, ambayo ni sawasawa na shilingi 175/= kwa kilo moja; lakini pia wanatozwa ushuru wa Bodi ya Kahawa; ushuru wa utafiti; wakulima wamebebeshwa mzigo mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali hii ya awamu ya tano iweze kuliangalia hili. alichokuwa anakizungumza Mheshimiwa Rais naomba akifanyie kazi kweli kweli na isiwe maneno tu. Ninaamini kabisa kwamba Mungu atambariki na atakwenda kuwasaidia wakulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, imekuwa ni mzigo, inafika mahali mkulima wa kahawa licha ya kwamba anatozwa ushuru huo ambao nimesema ni 5%, pamoja na matatizo mengine lakini mkulima huyu wa kahawa na mazao mengine ameshindwa kutafutiwa somo zuri na mwisho wa
siku inaonekana kwamba anauza kwa bei ndogo sana. Kwa mfano, msimu uliopita wakulima wa Kahawa wameuza kahawa yao kwa bei ndogo sana. Naomba Serikali iangalie suala hili maana bila kuwasaidia wakulima kwa kweli tutakuwa tunarudi nyuma, maana tunajua kabisa kwamba kilimo kinachangia zaidi ya asilimia 70 ya pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niweze kuzungumza kwa ufupi sana ukurasa wa nne wa hotuba ya Rais. Alizungumzia suala la siku ya uchaguzi kwamba ilikuwa na utulivu na amani. Naomba nizungumze tu kwamba katika hili nadhani Rais wetu atakuwa kidogo aliteleza.
Siku ya uchaguzi tarehe 25 Oktoba, 2015 ilikuwa na amani na utulivu; hayo maneno sijajua vizuri kwamba labda alikosea au aliteleza.
Ni kwamba kuna maeneo mengi sana vurugu zilifanyika, kuna watu walipigwa, watu waliwekwa ndani, watu wamebambikiziwa kesi, watu hadi leo wengine wamekimbia maeneo yao, halafu Rais anasema eti siku hiyo ilikuwa ya amani na utulivu. Mimi nadhani kuna watu
labda walimpotosha Mheshimiwa Rais kwenye hili, nami naomba tu Mheshimiwa Rais inabidi kidogo afuatilie hili vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano natoa mfano mdogo wa Jimboni kwangu Mbozi.
Jimbo la Mbozi uchaguzi siku ya Jumapili, tarehe 25 Oktoba, 2015 watu waliwekwa ndani wakiwa wanadai matokeo. Wamefunguliwa kesi hadi leo! Wengine wameshakimbia, hivi ninavyozungumza hawapo kwenye Jimbo langu. Mheshimiwa Rais anakuja anasema kwamba
Uchaguzi ulikuwa wa amani na huru.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu kwamba siku nyingine Serikali tujipange vizuri. Kunapokuwa na uchaguzi tujaribu kutumia Jeshi la Polisi vizuri na yule aliyeshinda kihalali atangazwe haraka sana. Kwa sababu mambo yote haya yanajitokeza pale mtu ameshinda wanashindwa kutangaza matokeo mapema, inafika mahali watu wanadai matokeo wanaanza kupigwa, wanapelekwa ndani, wanafunguliwa kesi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili kwa kweli linasikitisha sana na machafuko mengi tu yametokea katika sehemu mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine mdogo tu naweza nikatoa. Hata ndugu zetu kule Zanzibar hali kwa kweli haiko shwari kabisa hadi hivi ninavyozungumza. Hali haiko shwari! Hili limejitokeza! Mwenyekiti wa ZEC amekaa peke yake anatangaza kwamba tunarudia uchaguzi
wakati huo unaona kabisa kwamba hawajakubaliana na Tume.
Mheshimiwa Naibu Spika, imefika mahali na ushahidi upo, tutajaribu kuuwasilisha kama utahitajika kwa muda ambao tutapangiwa, Makamu Mwenyekiti wa ZEC alikamatwa akawekwa ndani.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Haonga naomba umalize!
MHE. PASCAL Y. HAONGA: Kwa hiyo, hali haikuwa nzuri, hapakuwa na utulivu wowote ule. Naomba tunapoelekea huko siku za usoni kweli kabisa tuishauri Serikali isimamie uchaguzi vizuri, aliyeshinda awe ameshinda na mambo yaweze kwenda vizuri kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichangie suala lingine. Kwenye kilimo kuna suala dogo nilikuwa nimelisahau, kuhusu mfumo wa vocha ambao Serikali inautumia kuweza kuwapa wakulima. Mfumo wa vocha kusema ukweli siyo mzuri kabisa. Vocha hizi zinawanufaisha wale watendaji wachache, Watendaji wa Vijiji, Watendaji wa Kata na watu wachache, mara nyingi sana wanazigawa kwa kufuata itikadi ya Vyama vya Siasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hizi vocha za pembejeo zinazotolewa kuna mtu akiwa chama fulani cha upinzani vocha hizi hazimhusu, hata kama ni mnufaika, hapewi. Vocha hizi zinawanufaisha watu wachache sana. Natoa mfano mdogo tu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, msimu wa kilimo huu uliokwisha vocha zilikuja 13,000 kwa Wilaya nzima ya Mbozi. Wilaya ina wakazi zaidi ya 500,000 vocha zimekuja 13,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani kwamba mfumo huu siyo mzuri kabisa, ni mfumo wa ubaguzi, hauwezi kuwasaidia wakulima wetu. Nasema kabisa kwamba kuna namna ambayo inatakiwa tuifanye ili kubadilisha mfumo huu wa kugawa vocha hizi za kilimo. Kama kuna
uwezekano Serikali itafute utaratibu mzuri kwamba mbolea inapoingizwa nchini, kama Serikali inaweza ikatoa ruzuku moja kwa moja kwa ile mbolea inapoingizwa nchi nzima, inapouzwa basi iwe imeshalipiwa ruzuku na kila kitu, angalau sasa ionekane ni ya ruzuku nchi nzima, hata kama ni pesa kiasi kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mfuko wa mbolea leo unauzwa shilingi 70,000/=. Labda mfuko wa mbolea Dar es Salaam hapo unauzwa shilingi 70,000/=. Kama Serikali inaweza ikaweka pesa yake ya ruzuku kidogo pale, ikalipa kwa mfano hata 40% au 50%, maana yake
shilingi 70,000/= inaweza ikashuka hadi kufikia shilingi 35,000/=hadi shilingi 40,000/=. Hiyo ni nchi nzima, maana yake watu wa Mbozi wanunue kwa bei hiyo, lakini pia watu wa Kigoma wanunue kwa bei hiyo kuliko mfumo wa sasa ambao unawanufaisha wafanyabiashara
wachache, lakini pia ni mfumo wa kibaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba suala hili tuliangalie sana kwa sababu Tanzania bila kilimo haiwezekani, ninaamini Kilimo kinachangia asilimia kubwa sana katika pato la Taifa.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Haonga, muda wako umekwisha.
MHE. PASCHAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kidogo.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Haonga muda wako umekwisha tafadhali! Mheshimiwa Haji Khatib Kai! Mheshimiwa Abdallah Mtolea.