Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Omari Mohamed Kigua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nikushukuru kwa kunipa fursa jioni ya leo niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Sheria. Kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri husika wa Wizara hii kwa bajeti nzuri sana ambayo ameiwasilisha kwa siku ya leo. Bajeti hii imechukua mambo mengi sana ambayo yalikuwa ni kilio cha wananchi, nikiamini kabisa kwamba imeweza kujibu kilio cha wananchi wa maeneo mbalimbali, hususan wa Jimbo la Kilindi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakililia Mahakama ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hatua zake anazochukua za kutumbua majipu.
Vilevile nimpe moyo kwa changamoto anazozichukua kwa wale watendaji ambao kwa muda mrefu wamekuwa ni matatizo ya nchi hii, ninaamini kabisa Waheshimiwa Wabunge na hata wale wa upande mwingine wanajua Mheshimiwa Rais anachukua msimamo ulio sahihi kabisa. Mambo haya ni ya msingi tukiweza kuyazungumzia kwa mustakabali wa nchi yetu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze moja kwa moja kuchangia hususan kwenye Mahakama zetu. Tanzania hii ina Mahakama za Mikoa, Mahakama za Rufaa na Mahakama za Mwanzo, lakini ninaamini kabisa changamoto za Mahakama hasa hizi za Mwanzo na Wilaya zimekuwa ni kubwa sana, kwa maana kwamba mahakama nyingi zimekuwa chakavu na hazijafanyiwa ukarabati wa muda mrefu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna maeneo ambayo yana Wilaya lakini hayana Mahakama za Wilaya. Mfano katika Jimbo langu la Wilaya ya Kilindi ni takribani miaka 13 toka tumepata Wilaya lakini hatuna Mahakama za Wilaya. Jambo hili limekuwa ni kero kubwa sana kwa sababu wakazi wa Jimbo la Kilindi wamekuwa wakifuata huduma hii ya Mahakama kwa takribani kilometa 200 au 190 kutoka Wilaya moja hadi Wilaya nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kilindi kwa ujumla ina changamoto nyingi sana za migogoro hasa ya wakulima na wafugaji. Kwa hiyo, unakuta kwamba, jambo hili limekuwa ni kero ya muda mrefu na hata Mbunge aliyepita alikuwa akilipigia kelele suala hili, lakini ninamshukuru Mheshimiwa Waziri husika kwenye bajeti yake ameweza kuliona hili na miongoni mwa Wilaya 12 ambazo zimetengewa hela kwa ajili ya kujengewa Mahakama ya Wilaya basi na Wilaya ya Kilindi imepata fursa hiyo. Naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni suala la Mahakama hizi za Wilaya kutokuwa na Mawakili wa Serikali. Mawakili wa Serikali wamekuwa ni msaada mkubwa sana kwa wananchi ambao hawana uelewa wa elimu ya sheria. Nashauri hususan kaka yangu Waziri, Mheshimiwa Mwakyembe kwamba muda umefika sasa hivi wa kuwa na Mawakili katika kila Mahakama ya Wilaya, kwa sababu watu hawa wanawasaidia wananchi wasiokuwa na uwezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme jambo moja, Mawakili katika kitabu chako umeeleza hapa kwamba mna mpango wa kupunguza idadi ya mrundikano ya kesi, kwa maana ya kwamba zero case backload! Mheshimiwa Waziri hebu nikuulize swali moja pengine utanipa maelezo wakati unajibu hoja hizi kwamba unatarajia Mahakama ya Wilaya at least iweze kujibu kesi 250 kwa mwaka, sasa Hakimu wa Wilaya ambaye anabeba Wilaya mbili kwa maana ya Wilaya ya Kilindi na Wilaya ya Handeni anawezaje kutatua kesi hizi kwa kipindi cha mwaka mmoja? Haya ni mambo ya msingi kabisa na unaweza tu ukaenda ukauliza pale Mahakama ya Wilaya ya Handeni kwamba, Hakimu ana idadi kiasi gani ya kesi za kutoka Wilaya hizi mbili?
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba wakati tunasubiria kujenga Mahakama ya Wilaya, sisi tunayo majengo katika Jimbo la Kilindi tunaweza tukapewa Hakimu wakati tunasubiri jengo likijengwa. Mimi nadhani fursa hii ni nzuri, ili tuweze kuwapa haki wananchi wa Wilaya ya Kilindi. Ninadhani changamoto hii haipo katika Jimbo langu tu, ipo katika Wilaya mbalimbali ambazo hazina Mahakama za Wilaya, nikiamini kwamba wananchi wanayo haki ya kuwa na huduma hizi za kimsingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kuchangia siku ya leo ni suala la Serikali kupoteza kesi. Serikali inapokuwa inawashtaki watu mbalimbali mara nyingi huwa inapoteza kesi! Sasa tunatakiwa tujiulize sababu za msingi ni kwa nini Serikali inapoteza kesi? Haya ni mambo ya msingi kwa sababu wakati mwingine Serikali inashtaki mambo ambayo watu wamehujumu nchi! Tuchukulie mfano wa kesi ya samaki wale, Serikali imepoteza na inatakiwa kulipa fidia. Sasa ni nini kilichosababisha Serikali ikapoteza kesi hiyo wakati Serikali inao wataalam, inao Waendesha Mashitaka wa kutosha na wenye elimu yakutosha! Nadhani imefika muda sasa tuangalie utaratibu mzuri wa namna gani tunaweza kupata watu ambao wamebobea wanaoweza kuishauri Serikali katika mambo ya kesi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulichangia ni juu ya bajeti ya Wizara hii. Mheshimiwa Waziri husika wa bajeti hii amezungumza sana kwamba ana changamoto ya bajeti, nadhani kwa sababu Wizara hii inahusika na mambo ya sheria na mambo ya mahakama ifike wakati kwamba, Wizara hii yenyewe tuiongezee hela ili tuweze kuondokana na changamoto mbalimbali kwa ajili ya kutatua kesi za wananchi na kutoa haki kwa wananchi wa Tanzania kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ningependa kuchangia katika upande wa Mahakama za Mwanzo. Nichukulie mfano katika Jimbo langu la Kilindi, Mahakama za Mwanzo ziko chache sana! Jimbo lenye Kata 21 na vijiji visivyopungua 102, Mahakama za Wilaya nadhani ziko kama tatu kama siyo nne! Maana yake ni kwamba wananchi wanakosa haki zao za kimsingi. Kwa hiyo, imefika wakati Mheshimiwa Waziri husika ahakikishe kwamba ule mpango wa kuwa na Mahakama za Mwanzo katika kila Kata, basi mpango huo Serikali kwa dhati ya moyo wake ihakikishe kwamba mahakama hizo zinaanzishwa na zinakuwa na Mahakimu wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa kushauri ni juu ya idadi ya Mahakimu katika Mahakama zetu. Sehemu nyingi sana utakuta utakuta kwamba, hatuna Mahakimu, lakini tunacho Chuo cha Mahakama Lushoto! Kwa nini Serikali isingetia nguvu pale tukahakikisha kwamba wataalam wengi wanapatikana, Mahakimu wanapatikana, ili Mahakama zetu ziweze kuwa na Mahakimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango huu kuna uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi ambayo inatarajiwa kuanza mwaka wa fedha huu. Jambo hili nataka niipongeze sana Serikali hususan Mheshimiwa Rais kwa uamuzi wa dhati wa kuanzisha Mahakama hii. Mimi naamini kabisa kwamba muda umefika sasa hivi wa kuwa na Mahakimu wa kutosha katika kila Wilaya, kila Kata, ili wananchi wetu waweze kupata haki za msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ningependa kuchangia juu ya ukusanyaji wa maduhuli katika mahakama zetu. Nadhani utaratibu uliopo sasa hivi ni mzuri lakini inabidi uboreshwe sana. Uboreshwe kwa sababu mahakama hizi zina mahitaji mengi sana, wakitegemea OC ya Serikali maana yake uendeshaji wa mahakama hizi hautakwenda vizuri. Mimi ni imani yangu kwamba Serikali imesikia haya na imesikia michango ya Waheshimiwa Wabunge mbalimbali tukiamini kwamba muda umefika wa kuweza kutoa haki kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo machache, naomba kuunga mkono hoja ya bajeti hii. Ahsante.