Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Rashid Mohamed Chuachua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Masasi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. RASHID M. CHUACHUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Na mimi nashukuru kupata fursa ya kuchangia kidogo katika maeneo ambayo nilipata nafasi ya kuyamakinikia wakati ninapitia vitabu vilivyotolewa na Serikali kwa ajili ya mjadala wetu wa leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze na kutoa pongezi kwa Serikali kwa kazi kubwa waliyofanya ya kutekeleza miradi katika kipindi ambacho wameikiainisha, lakini niseme tu wakati najaribu kumakinika zaidi kwenye taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kipindi cha mwaka 2016/2019 sikuona kazi zilizofanywa na Wizara ya Maji kwenye kitabu hiki. Kama itampendeza Waziri Mpango basi atupatie miradi hiyo tuione maana tuna wajibu wa kujua Wizara yetu ya Maji imefanya kazi kwa kiwango gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mengine nilitaka kufahamu utekelezaji wa suala la maji kwa Serikali kwa upande wa Mradi wa Maji wa Mbinji ambapo tulitengewa shilingi bilioni mbili katika kipindi kilichopita kwa hiyo, tungepeta fursa ya kuona utekelezaji huo tungeweza kujua kama fedha hizo zimetoka au zimefikia katika hatua gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapopitia mapendekezo ya mpango pamoja na utekelezaji wa miradi bado naona kuna kazi kubwa na Serikali inapaswa kuona umuhimu sasa wa kutenga fedha za kutosha kwenye miradi ambayo inatoa huduma za jamii, huo ndio mtazamo wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo miradi ya umeme, tuna miradi ya maji, lakini pia tuna suala la elimu, hayo ndio maeneo matatu nitakayoyazungumzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na umeme, suala la usambazaji wa umeme wa REA kwa kweli, haliendi sambamba na matarajio ambayo sisi kama Wabunge tunayo. Kwa hiyo, kwa mfano ukisoma kitabu cha utekelezaji ukurasa wa 55 inaonesha kwamba takribani vijiji kama 5,000 ndivyo ambavyo vimefikiwa katika mpango huo. Tukumbuke tunao mpango wa utekelezaji wa REA kwa awamu ya tatu sasa na zaidi ya vijiji 7,000 mpaka sasa bado havijafikiwa. Ukienda kwenye mapendekezo ya mpango, katika mapendekezo ya mpango ukurasa wa 30 inaonesha kwamba mwaka kwa 2019/2020 matarajio ni kufikia vijiji 557.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Mkoa wa Mtwara peke yake, Wilaya ya Nanyumbu, Wilaya ya Masasi, Wilaya ya Tandahimba, Wilaya ya Newala na Wilaya ya Mtwara DC utaona kwamba wastani wa utekelezaji wa mpango huu wa REA kwa jumla ukitafuta wastani ni kama vile ni 23.6% jumlisha na bajeti ya 2018/2019. Katika mkoa huu peke yake vijiji 497 vimeachwa mpaka sasa bado havijafikiwa, lakini 2019/2020 tuna mpango wa kufikia vijiji 557, vijiji vingine hivi tunavifikia lini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda unakwenda na hapa mimi napendekeza sasa kama tatizo linaloonekana katika utekelezaji wa miradi ya REA ni fedha, basi napendekeza Serikali ione umuhimu sasa wa kupunguza fedha katika baadhi ya miradi mikubwa ambayo tunataka kuitekeleza ili tupeleke fedha hizo kwenye miradi inayowagusa wananchi, hususan miradi ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la maji, tatizo liko palepale, fedha katika utekelezaji wa miradi. Ukisoma hotuba ya Waziri ukurasa wa 31, inaonesha kwamba tumeshawafikia Watanzania milioni 31 kuwawekea maji ya bomba. Hii ni kama 50% tu ya Watanzania wote, bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika hili na bado nashauri, ili kuweza kufikia miradi mingi kwa pamoja na kuwafikia wananchi wengi ni muhimu Serikali ikaona umuhimu wa kupeleka fedha za kutosha kwenye miradi hii na ikibidi kupunguza fedha kwenye baadhi ya miradi mikubwa, ili kufika katika miradi ambayo inawagusa wananchi moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la elimu, kila nilipokuwa nachangia mpango nimekuwa nikisema kwamba mipango inayoletwa na Serikali pamoja na mambo mazuri mengi yanayofanywa, lakini haigusi elimu nje ya mfumo rasmi na leo nitarudia kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, tangu tumeanzisha kutoa elimu bila malipo, kwa mfano katika shule ya msingi wanafunzi wengi sasahivi wanaandikishwa na wengi wanamaliza, lakini bado najiuliza wanafunzi hawa ambao kimsingi shule za msingi ni nyingi sana kuliko shule za sekondari, wanapomaliza, ni wazi kabisa watoto hawa kwanza wengi wao ni watoto wa wanyonge na hawawezi kwenda shule za sekondari za kulipia au shule za binafsi, lakini katika shule za sekondari za Serikali wanachukuliwa wachache, wengi wanabaki, wanakwenda wapi? Hili ni swali ambalo najiuliza kila siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kutoa tu mfano, ukisoma Ripoti ya UNICEF ya mwaka 2018 inaonesha kwamba walifanya utafiti kwenye watoto milioni 3.7 wakabaini kwamba katika watoto wale milioni 3.7 wenye umri wa miaka 14 mpaka miaka 17 ni watoto 59.1% ndio ambao walikuwa shuleni, takribani 40.9% hawakuwa madarasani, hawakuwa shuleni, walikuwa mitaani na wapo katika umri wa kupata elimu. Na watoto hawa walikuwa wamegawanyika katika makundi mawili tu, kulikuwa kuna watoto ambao hawakwenda kabisa shuleni na kulikuwa kuna watoto ambao wameacha shule. Hivi kweli Serikali inajua kwamba inalo jukumu la kutoa elimu hata kwa watot ambao wako nje ya mfumo wa elimu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba ni muhimu Serikali itambue kuwa pamoja na juhudi inazozifanya za kuhakikisha kwamba Watanzania waasoma bila ya kulipa, lakini hata tufanye nini hatuwezi kuwa- accommodate Watanzania wote kwenda form one kwa sababu shule hatuna za kutosha. Kwa hiyo, kwa namna yoyote lazima tuwe na alternative means ya kuhakikisha kwamba, hawa watoto wanapata elimu kwa sababu wapo wanaoacha shule kwa sababu ya mimba, utoro, migogoro ya kifamilia na wapo wanaoacha kwa sababu ya uyatima. Baada ya kuacha shule ambazo ni shule rasmi za Serikali sisi kama Wabunge tunao wajibu wa kuiambia sasa Serikali ichukue majukumu haya ya kuhakikisha kwamba, watoto hawa wanapata elimu kwa sababu, nao ni watoto ambao wanahitaji kusoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nizungumze kitu kimoja, tunayo Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ambapo inaonesha takwimu zake kutoka mwaka 2004 mpaka mwaka 2017 imepitisha takribani watoto 159 kumaliza kidato cha nne, 159,000 yaani 150,000 kumaliza kidato cha nne. Hawa watoto ni wachache, maana yake Serikali katika watoto karibu milioni ambao tunawaacha kila mwaka wasioweza kuingia shuleni au wanaoacha shule tunawaacha wakiwa mtaani. Hii ina maana kwamba kila tunavyozidi kwenda mbele ndivyo kiwango cha watu wasiojua kusoma na kuandika kinaongezeka. Ndivyo kiwango cha watu ambao hawamalizi kidato cha nne kinaongezeka, ndivyo kiwango cha watu ambao hawamalizi hata darasa la saba kinaongezeka. Jukumu letu ni nini Serikali katika jambo hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijawataja bado vijana ambao hawapo katika umri wa shle ya msingi, wapo katika umri wa shule ya sekondari, wako mtaani. Wana ari ya kutaka kusoma, hawawezi kwa sababu ya umaskini, tunafanyaje kama Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu tunayoitoa kwa wanyonge kwa walio ndani ya shule inapaswa pia, tuitoe kwa wanyonge kwa walio nje ya shule kwa kupitia mfumo wa elimu ya watu wazima pamoja na kwa kutumia nje ya mfomo rasmi. Naomba Serikali iangalie maeneo haya, lakini pamoja na mambo mengi niliyozungumza kama sehemu ya kupata marekebisho katika mpango wetu, naunga mkono hoja ya Serikali. Ahsante sana.