Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mchinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia na kunijalia mimi jioni ya leo kupata fursa ya kuweza kushauri machache ambayo yanaweza, kama mtaamua kuyasikiliza na kuyafanyia kazi yanaweza kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo swali moja kwa Mheshimiwa Dkt. Mpango. Naomba tu kwanza Mheshimiwa Mpango anijibu atakapokuja kwenye kufanya majumuisho, ama atujibu Watanzania, kilio kikubwa cha Watanzania ni kwamba watu hawana fedha mifukoni, yaani mifukoni fedha hakuna, kwenye mabenki fedha hakuna, kwanza tunataka tujue fedha ziko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, kinachoshangaza zaidi, mie sio mchumi mtatusaiia nyie wachumi, kinachoshangaza zaidi kwamba fedha mfukoni hakuna, benki hakuna fedha, halafu kuna mfumuko wa bei, sasa kiuchumi hii inakuwaje? Yaani fedha, purchasing power ya watu imepungua mifukoni, lakini pia kwenye benki watu hawana pesa, halafu kunakuwa na price flactuation, hii inakuwaje kwenye uchumi? Kwa kawaida watu wanapokuwa na fedha nyingi mifukoni ndio panapotokea na hiyo boom, sasa inakuwaje kwamba watu hawana fedha, halafu kumekuwa na mfumuko wa bei?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tusaidie na watu hawana fedha kweli kweli, hawana fedha kabisa na sio watu tu hata makampuni tunashuhudia sasa TTCL juzi wametangaza kupunguza wafanyakazi 500, TBL huko ndio watu wako hoi kabisa na makampuni mengine tunajua namna hali ilivyo, sasa hilo ni swali langu la kwanza Mheshimiwa Mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili wakati nachangia ninaomba niishauri Serikali, tumeisahau sana sekta ya gesi na tumeisahau bila kujua kwa nini tunafanya hivi, wakati Serikali hii hii ndio iliyowaahidi Watanzania kwamba, itaibadili Mikoa ya Lindi na Mtwara kuwa Qatar ya Afrika, lakini pia Serikali hii hii ilituaminisha Watanzania kwamba kwa kupitia uchumi wa gesi tutakuwa na umeme wa uhakika, tutakuwa na viwanda vingi vya mbolea, tutakuwa na viwanda vya menthol, kutakuwa na viwanda vya Liquified Natural Gas pale Lindi, tutakuwa na vitu vingi, tuliahidiwa na Serikali hii hii, leo tumefikia wapi kwenye gesi? Tunaomba maelezo Mheshimiwa Mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, asubuhi nilikuwa nasoma taarifa kwenye mtandao mmoja, Hydro-carbons Technology Limited ambao ndio wanatoa sana taarifa za gesi. Russia ambao ndio leading na super power wa gesi duniani ambao wana cubic litre karibu milioni 47,000 wao ndio wanaouza umeme karibu 60% ya umeme wa Ulaya unatoka Russia na hili mnalifahamu, lakini sisi umeme wa gesi Watanzania hatuutaki tunaona sijui kwamba una gharama, tunaachana na umeme wa gesi tunaenda kwenye maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ajabu ambalo ni jambo la hatari sana, nilikuwa nafuatilia taarifa kwenye mtandao, sisi mpaka sasa ni nchi ya 22 kwa kuwa na reserve nyingi ya gesi, kwa taarifa zilizopo mpaka Januari, 2017 ni nchi ya 22 duniani. Msumbiji ni nchi ya 15 na mkumbuke gesi ya Tanzania iko kwenye eneo moja na gesi ya Msumbiji, ni pale Ruvuma Basin ambayo wenzetu tayari sasahivi wameshagundua na wanaitumia karibu milioni mbili cubic litres hizo kwenye trillion huko, hata mahesabu yake sijui, 2,100,086 sisi tuko kwenye milioni 1,068,000 wakati sisi tunagundua gesi, Msumbiji walikuwa bado hawajaanza matumizi ya gesi. Kwa hiyo, wana-extract gesi nyingi ambayo gesi ni kitu kinachohama, probably watakuwa wanaichukua gesi hata hii ambayo sisi ingekuwa tungeweza kui-extract kwenye eneo la Tanzania. Mwisho wa siku tutakuja kujikuta kwamba, gesi yote ya Ruvuma Basin imetumika Msumbiji, sisi hatuna gesi ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mpango hili liangalie sana, gesi ile pale Msimbati pale, Mnazi Bay, iko mpakani kabisa kati ya Tanzania na Msumbiji na wenzetu mpaka sasa wana plant za LNG tatu ambazo wana- export gas sasa hivi, sisi hatuna hata moja. Kulikuwa na mpango wa kujenga mitambo ya LNG pale Lindi, pale Likong’o na mpakani kabisa kwenye eneo la jimbo langu na watu mmekwenda, mmefanya tathmini kwamba mnataka kulipa fedha bilioni tano mkatuambia kwenye mpango wa mwaka juzi, wa mwaka jana kwamba mmetenga, mpaka leo hata mtu mmoja hamjamlipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuambieni mtakapokuja kujibu kwamba, mnaachana kabisa na mipango ya gesi, mnaachana kabisa na mipango ya LNG ili tuweze kujua kwa sababu kule Lindi na Mtwara tunaishi kwa matumaini tukijua LNG itakuja kumbe kitu chenyewe hakipo kabisa. Kwa hiyo, naomba hili tuliweke wazi na kila mtu alifahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2013 wakati watu wa Lindi na Mtwara walipofanya riot kuikumbusha Serikali juu ya majukumu ya wao kunufaika na gesi na mnakumbuka tarehe 16 Mei, TPDC walifanya press conference kuwajulisha umma namna gani wananchi wa Lindi na Mtwara watanufaika na ugunduzi wa gesi kule Lindi na Mtwara. Ndugu zangu, Mheshimiwa Mpango, ninachotaka nikueleze yale waliyoyasema TPDC jambo moja la uhakika ambalo sasa lipo ni moja tu kwamba umeme wa uhakika upo, lakini mengine yote mmetudanganya hayapo kabisa.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mpango hili tunapolisema naomba uli-take very serious na ninaona lazima tuseme kwamba tukiidharau gesi, si tukiidharau, gesi ni kimiminika kinachohama, Msumbiji wataitumia na mwisho wa siku sisi tutakuja kuvuna mabua kama alivyosema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wanasema sana mbishi Mheshimiwa Mpango, haambiliki, lakini ndio tunasema hivyo. Tuliongea humu kwenye korosho na wengine tulisema kabisa kwamba ikifika mwezi wa 10 majibu yatapatikana hapa na mwezi wa 10 majibu yamepatikana ni kwa sababu hii hii ya kueleza mkatudharau. Sasa ukichukua ule msemo wa Kiswahili kwamba kama husikii la muadhini hautasikia la mchoteamaji, basi sawa tutaendelea hivyo hivyo, lakini naamini madhara yake yanatugusa sisi Watanzania wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, mimi nilitaka kujua sera ya uwekezaji ya Tanzania sasa hivi wapi tumekwama? Juzi nimeona taarifa imetolewa kwamba usalama wa biashara Tanzania tumeshuka kutoka 137, aliyoisema hata mama yangu hapa Mheshimiwa Ruth Mollel, sasa hivi tuko 144. Hali ya ufanyaji wa biashara, usalama wa biashara Tanzania tuko nafasi ya 144 duniani, tunaendelea kuporomoka, tatizo ni nini? Kwamba kadri siku zinavyokwenda sisi kibiashara tunashuka, tumekwama wapi Mheshimiwa Mpango?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kengele imepigwa, jambo la mwisho Mheshimiwa Mpango ni suala la korosho. Korosho ni moja ya giant cash crop in this country na inatuingizia fedha kubwa. Mwaka jana imeingiza 1.3 trillion katika nchi hii, sio kitu kidogo cha kukidharau ni jambo kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mpango tunakata kujua, tumesikia Mheshimiwa Rais amesema kwamba zingeweza kununuliwa, hebu tupe assurance watu wa Lindi na Mtwara; na nimemsikia Waziri anasema eti minada hii ni ya awali, sijui ile sheria haijasomwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, minada ya korosho Lindi inaanza tarehe 1 Oktoba, leo tuko tarehe 7 Novemba, ukituambia ni minada ya awali unatudanganya. Miaka yote korosho tunaanza kuuza tarehe 1 Oktoba, leo hili jambo sio la kawaida, lazima tuseme ukweli ndugu zangu, tuseme kwamba, kuna tatizo lipo na tuwaambie Watanzania kuna tatizo moja, mbili, tatu na solution ni hii. Mkituambia solution kwamba, jeshi litabangua hata kwa meno it is not a solution, tunaona kama mnatutania. Mtuambie what is a way forward, solution ya korosho iko wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda kule Lindi watu wananyanyaswa, korosho zinabaguliwa, korosho ambazo mwaka jana zilikuwa zinaonekana ni super leo watu hawazitaki na zina content za kutosha kwa sababu wanajua hatuna soko la uhakika mtu anakwenda anasema content ya korosho hii ndogo. Mheshimiwa Mpango tunaomba majibu ya uhakika korosho yetu lini tutauza na soko likoje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.