Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na usipate hofu. Bahati mbaya sana kila mara tunapopewa nafasi tunapojaribu kuishauri Serikali kwa sababu wametubandika jina wanaita vyama vya upinzani badala ya kuita vyama rafiki vya vyama tawala, basi kile tunachokisema mara nyingi wao wanafikiri kwamba tunakuja kupinga. Hata hivyo, kila mara tukija humu ndani tuna mawazo mazuri kabisa, tumeona hotuba yetu ya Kambi ilivyosema, bahati mbaya sana wakati wa bajeti hatukupata nafasi ya kutoa hizi hotuba lakini leo tumewaeleza hapo kuhusiana na huu mpango uliko hapo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hiki kitabu cha mpango wa mwaka mmoja ambao Mheshimiwa Dkt. Mpango ametuletea hapa, sisi kama Wabunge kazi yetu ya kwanza kabisa ni pamoja na kuishauri Serikali. Tumejaribu kushauri mara nyingi lakini Mheshimiwa Dkt. Mpango alikuwa anafikiri kama tunampinga na kubeza, kile tunachokiwaza sisi na mawazo yetu mengi yalikuwa hayachukuliwi ili kuboresha na kulifanya Taifa letu liende pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kwenye hotuba yake kama ambavyo iko mbele yetu kwenye ukurasa wa 34, maeneo mengi yanaonesha ni namna gani mipango mingi iliyokuwa imepangwa itekelezwa mwaka jana haikutekelezeka. Nitatoa tu mfano wa masuala machache. Anasema kutofikiwa kwa lengo la kodi zinazotokana na ajira (Pay As You Earn), anatoa na sababu, kulikosababishwa na kutofikiwa kwa malengo ya ajira mpya na kutoongezeka kwa mishahara. Sasa ni mara ngapi humu ndani tumesimama tunajaribu kuishauri Serikali iongeze mishahara kwa watumishi ili haya mambo yaweze kufuatiliwa pale? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa kweli kabisa kutoka moyoni na ningetamani sana kabla ya ule mdahalo ambao ulifanyika chuo kikuu usingefanyika kwanza mpaka Mheshimiwa Dkt. Mpango alete huu mpango wake na kulieleza Taifa ni nini kinatokea. Maprofesa walismama pale wakaishia tu kusifu, kutukuza na kupongeza, muda wote ndiyo kazi ambayo waliifanya lakini hawakushauri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Mheshimiwa Dkt. Mpango anakuja tena ndani ya Bunge anatueleza mwenyewe ni namna gani mambo huko nje hayaendi. Hili ni jambo la sisi wote kumpongeza badala ya kuishia tu kusifia yale mazuri au kusifia yale mengine tunayofikiri kwamba ni ya kujenga lakini kimsingi Mheshimiwa Dkt. Mpango mwenyewe anakiri kwamba mambo hayaendi, uchumi umeporomoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukieda kwenye point yake namba tatu anasema, kushuka kwa biashara za kimataifa kulikopelekea kutofikia malengo ya uingizwaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi kama ambavyo ilitarajiwa. Anaendelea kusema kwamba, kuendelea kuwepo kwa madai mbalimbali yakiwemo ya wakandarasi, watoa huduma, wazabuni na watumishi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndani kila siku tunakuja na neno uhakiki ili tuweze kuwalipa watumishi wa umma lakini bado wanakiri madai hayo yapo, wakandarasi wa ndani hawalipwi, kwa hiyo, maana yake pesa haizunguki. Hawa wakandarasi wa ndani ndiyo watu ambao wanaendesha uchumi wa nchi yetu, wao ndiyo wanaokwenda kununua kwenye maduka yetu madogomadogo na kufanya uchumi uweze kuzunguka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mimi nimwambie kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mpango, kwamba sisi Chama cha Demokrasia na Maendeleo tumekuja na Sera Mbadala na naomba nikupe hii copy kama zawadi ukaisome na jioni nitakuletea copy nyingine ikiwezekana umfikishie Mheshimiwa Rais naye asome aone mawazo yetu, alinganishe na hayo ya kwenu muweze kuboresha. Haya yote uliyoyasema hapa ndani na kuyaandika hapo mimi nataka tu nikupeleke katika baadhi ya pages kwenye sera yetu halafu wewe utakwenda kusoma zaidi uweze kudadavua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukija kwenye Sera ya CHADEMA ukurasa wa 17, hapa tumeweka wazi Mheshimiwa Dkt. Mpango na naomba ukasome vizuri tu, tunaongelea kuhusu mikakati jumuishi ya uchumi wa Taifa. Tunasema hivi, kuimarisha uchumi, kukabiliana na changamoto za ajira na bei ya bidhaa, ndiyo ambayo umeyalalamikia huku, sisi tumepata suluhisho, utakwenda kuisoma mwenyewe vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili tunasema, kuwa na mfumo wa kodi unaotabirika. Mheshimiwa Zungu hapa ametoka kuchangia sasa hivi anakueleza masuala ya kodi yasiyotabirika (unrealistic taxes). Tunakwenda kutoza watu kodi, watu wanalalamika VAT hazirudishwi, kodi ya sukari ghafi kwenye viwanda hazirudishwi. Kwa hiyo, tunaomba kuwe kuna mfumo wa kodi unaotabirika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tunasema hivi, kuhakikisha kuwa kuna uwiano kati ya mauzo ya nje na kuagiza bidhaa za chini. Hii inakwenda sambamba kabisa na unapokuja hapa, sisi tumeanza kutengeneza reli na tulimshauri wakati fulani, tunakwenda kutengeneza ReIi ya Kati (Standard Gauge), tunanunua chuma nje, wataalam nao wanatoka nje, hivi kwa nini tusifikirie kwanza tukaanza kutengeneza kiwanda mama cha chuma kule Mchuchuma pamoja na kuboresha na kutengeneza Reli ya Kusini ili kwamba chuma yetu ya Mchuchuma tuilete Bandari ya Mtwara ikifika pale Mtwara itaondoka, nyingine itakwenda kuuzwa nje, nyingine itakuja kutengeneza Reli yetu ya Kati.
Ile tutakayouza nje tutapata pesa za kigeni, badala ya kwenda kukopa kule nje tutakuja kutengeza reli yetu kwa kutumia pesa zetu sisi wenyewe. Kwa hiyo, haya ni mawazo ambayo sisi tunayo na yapo kwenye sera yetu, utakapopata nafasi Mheshimiwa Waziri nenda kaisome vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda pia ukurasa wa 19, nataka nikuongezee madini ili tuweze kuboresha, tuishauri Serikali ili nchi yetu iweze kusonga mbele kwa sababu sasa hivi imesimama. Tunakuja hapa kwenye uchumi wa viwanda vyenye tija, hiyo ndiyo sera yetu sisi inavyosema. Tunasema kwamba, kutekeleza mkakati wa mabadiliko makubwa katika sekta ya viwanda. Mheshimiwa Dkt. Mpango, nadhani unaona hali ilivyo sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara lakini tumejaribu kuomba kwa Waziri wa Viwanda watupeleke kwenye viwanda wanavyoviita vilibinafsishwa, viwanda 155 tuweze kujua viko kwenye status gani ili tuweze kuishauri vizuri Serikali na kuona namna ya kusonga mbele lakini nikueleze kabisa sijui kama Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na Naibu wake wana nia njema kabisa ya kuhakikisha wanamsaidia Rais kwenye kupata viwanda. Sisi kama CHADEMA tumekuja na suluhisho utakapopata nafasi utasoma utaona namna ya kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesema tunatamani kufungamanisha uchumi wa ndani na viwanda. Tunaimba kuhusu viwanda, viwanda vinavyofanya kazi ni viwanda vichache vya tiles, vya nondo ambavyo vyote vimekuwa concentrated huu Ukanda wa Pwani kwa maana ya maeneo ya Mkuranga na kwingine. Sasa atakayekwenda kununua nondo ni nani na anakwenda kuzitumia wapi kama mazao yake ya shambani hayapatai bei bora? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia sasa hivi hapa kuna hii sintofahamu ya masuala ya korosho lakini ni kwa sababu tu ya kutokuwa na mpango bora kwenye jambo hili. Wale wanunuzi walilazimishwa kuitikia kwamba watakwenda kununua kwa bei ya Sh.3,000. Kimsingi gharama ya kuitoa korosho sasa hivi kuifikisha India ni zaidi ya Sh.4,000 wakati kule wanauza kwa dola moja na senti tatu sawasawa na Sh.3,800 ya Kitanzaia. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali kwanza ikiwezekana warudishe ile Sheria ya export levy, iletwe hapa ndani ifutwe kabisa ili kuweza kunusuru hawa wakulima sasa hivi waweze kupata pesa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, tuwaombe sasa, kwa sababu hiyo bei iliyopangwa siyo realistic na watu wanafikiri kwamba wanaolazimisha hii bei isitokee pale ni watu wa Kangomba. Korosho bei elekezi ni Sh.1,550 ndiyo ambayo ilipangwa pale, mtu anakuja na Sh.2,700 anataka kununua tunamwambia hii bei haijakidhi. Ndiyo ni bei ya chini lakini inategemea na soko. Kitendo cha kuondoa export levy, ile pesa ambayo ilitakiwa irudi kwa wakulima zile pembejeo na vitu vingine ndiyo imeleta hii trickle action, tunaona sasa athari zake zinazopatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itapoteza mapato kutokana na mauzo ya korosho na uzalishaji umeshuka. Pia Serikali inaweza ikaleta shida zaidi kwamba hizi korosho mwaka huu zisiishe kwa sababu msimu wa maeneo mengine unaanza, korosho yetu inaweza ikabaki, iko nyingi kwenye maghala. Kwa taarifa yako tu, tunavyoongea hapa sasa hivi leo ilikuwa ufanyike mnada wa Tunduru lakini kimsingi hakuna mnunuzi hata mmoja aliyekwenda Tunduru kwenda ku-bid kwa sababu hawawezi kutimiza yale masharti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado niendelee na kitabu chetu cha sera. Ukienda pia ukurasa wa 22 katika harakati za kuendelea kumshuari Mheshimiwa Dkt. Mpango tunasema hivi, usimamizi madhubuti, endelevu wa sekta ya madini…
T A A R I F A . . .
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mnaweza mkaingia wanafunzi wawili darasani mnafanya mtihani halafu yule anayedesa akafaulu vizuri kuliko aliyeingia na desa lenyewe kule ndani. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini unaulinda muda wangu, kwa hiyo, anachokifanya Mheshimiwa Innocent sikishangai na hawa ndugu zetu wa Chama cha Mapinduzi wanachokifanya wao wanaongelea kuhusu Ilani, sisi tunaongelea kuhusu sera na sisi tuna mawazo yetu tunataka tuyalete hapo mbele ya safari ili yatumike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naomba niendelee, nimesikia alichokisema napokea taarifa yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Mheshimiwa Zitto nimeipokea na yenyewe iingie kama sehemu ya mchango wangu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niseme kwamba kuna jambo ambalo linaendelea pale, suala la usimamizi madhubuti na endelevu wa sekta ya madini.
Tunaomba kabisa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)