Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Kiteto Zawadi Koshuma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kutoa mchango wangu katika Wizara ya Katiba na Sheria.
Pili, naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia fursa hii ili niweze pia kuendelea kuchangia katika Hotuba hii ya Wizara ya Katiba na Sheria. Ninawashukuru pia wanawake wa Mkoa wa Mwanza ambao waliniamini na kunipa kura nyingi na kuweza kuwawakilisha katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninaomba kuchangia kwa upande wa Sheria ya Ndoa. Katika Sheria ya Ndoa nimeangalia na kuona kwamba kuna upungufu ambao unafanya sheria hii kukandamiza haki za wanawake katika Sheria ya Ndoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kuna contradictions ambazo zinatokea katika Sheria ya Ndoa. Mtoto wa kike katika sheria hii anaweza akaolewa akiwa na umri wa miaka 16 lakini ukija katika Sheria ya Watoto (Children Act Law) mtoto anajulikana ni mtoto mwenye umri wa kuanzia sifuri hadi miaka 18, lakini kuna sheria ya Sexual Offensive Act, sheria hii pia na yenyewe inakuambia kwamba mtu ambaye anafanya mapenzi na mtoto mwenye umri chini ya miaka 18 amefanya kosa la jinai. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapata wakati mgumu sana kwamba hizi sheria tatu ambazo nimeziangalia zinaleta contradictions na zinamgusa mtoto wa kike, kwa sababu mimi ni mwakilishi wa wanawake siyo tu wa Mkoa wa Mwanza bali ni mwakilishi wa wanawake Tanzania nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, inaniuma sana kuona kwamba mtoto mdogo, tayari umemuita ni mtoto katika Children Act Law, mtoto ni wa umri chini ya miaka 18 lakini kwenye Sheria ya Ndoa unampa mwanaume mamlaka ya kumchukua huyu mtoto asiyekuwa na hatia, ambaye psychologically akili yake bado haijaweza kufikiria lolote kuhusiana na suala zima la ndoa. Lakini umempa mamlaka mwanaume aweze kumchukua mtoto huyu na kumweka unyumba kitu ambacho naona ni unyanyasaji kwa mtoto wa kike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, ninaitaka Serikali itakapokuja kujibu hoja za hotuba yake basi ije na kauli moja, kwamba inasema nini kuhusiana na hizi contradictions ambazo zinatokea katika hizo sheria tatu ambazo nimeziainisha hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusiana na kesi kurundikana katika mahakama zetu. Kesi zimekuwa ni nyingi sana zinarudikana kwenye mahakama na kufanya mahabusu kuwa wengi kwenye mahakama zetu. Lakini ukiangalia katika kesi hizo siyo wote wanaoenda kushtakiwa mahakamani wana makosa, wengi wao wamekuwa wakibambikwa kesi. Mfano mtu kaiba kuku lakini kwa sababu kuna fisadi mmoja ambaye amejificha somewhere anataka kumtumia huyu mtu ambaye ameiba kuku tu basi ahukumiwe kwa kesi ya kuiba kuku, lakini mtu huyu anapewa kesi ya mauaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inasikitisha sana unajiuliza Taifa letu la Tanzania tunaelekea wapi. Kwa uchungu mkubwa sana ninaiomba Serikali ianze kuangalia kesi hizi, japokuwa kwa juhudi za Mheshimiwa Rais wetu Mheshimiwa John Pombe Magufuli amelikemea sana suala hili la kesi kurundikana mahakamani hadi akaweza kuwaongezea Majaji fedha kwa ajili ya kuweza kuendesha kesi, lakini bado kesi zinaendelea kurundikana mahakamani na kesi nyingi kwa kweli ni zile za kusakiziwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naiomba Serikali itoe tamko kwa vyombo hivi vya kisheria ambavyo vinasimamia reinforcement ya sheria kwamba ni nini kinatakiwa kifanyike kwenye kesi ambazo ziko mahakamani ili kuweza kupunguza watuhumiwa hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ni kuhusiana na utoaji wa haki na utawala wa sheria. Kwa masikitiko makubwa sana na hata kama ni kulia ningeweza kulia mbele ya Bunge lako Tukufu, wanawake wamekuwa wakinyanyasika sana, mwanamke utakuta amepigwa na mume wake, anakwenda kushtaki polisi mwanaume anapelekwa mahakamani, lakini bado mwanamke huyu anaoneka kwamba ilikuwa ni halali kwa mwanaume kumpiga huyu mwanamke kana kwamba ni ngoma yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali ijaribu kuangalia suala zima la wanawake kunyanyasika katika utoaji wa haki zao. Unakuta kwa mfano, hapa sijui ni sheria gani inahusika lakini unakuta mwanamke ameolewa na mume wake kwa ridhaa yake na wanaishi vizuri, baada ya muda mfupi mwanamke huyu na mwanaume wanaamua kutengana kwa sababu labda wametofautiana baadhi ya vitu. Katika utofauti huo basi unakuta mwanaume anapofika Mahakamani kwa ajili ya kutoa talaka, mwanamke huyo anapopewa talaka anaambiwa nenda halafu mali zote anaachiwa mwanaume.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inasikitisha sana kwa sababu ni wanawake wengi sana afadhali hata wale ambao wamejaliwa basi hata kusoma wamepata elimu wanajua ni jinsi gani wataweza kujikwamua kuondokana na unyanyasaji huu ambao tunaupata kutoka kwa wanaume. Lakini vipi wale kundi kubwa la wanawake ambao hawajakwenda shule? Hawajui ni nini wafanye?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali kwa kushirikiana na Wizara husika waweze kuangalia dawati la kijinsia ambalo lipo lakini kiuhalisia halina kazi linayofanya. Ninaitaka Serikali sasa ianze kuangalia masuala ya kusaidia utoaji wa haki kwa wanawake na kuhakikisha kwamba wanawake wote wanapatiwa haki zao. Kwa sababu wanawake wengi wamekuwa wakinyimwa haki zao hata pale wanapofiwa na waume zao. Wajane wameteseka, wamenyang‘anywa mali na kuondoka bila chochote, wanabaki wanahagaika mtaani wakati ndugu wamebeba mali zote wameondoka wanajisifia mtaani kwamba wanazo mali halafu mwanamke huyu anaanza kukanda maandazi, anauza karanga, anafunga ufuta ili mradi maisha yake yaweze kusogea. Inasikitisha sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuongelea kuhusiana na kesi za Serikali. Inasikitisha kwamba Serikali inakuwa na kesi nyingi sana, inashitaki watu kwa kufanya makosa, lakini kesi zote almost 99 percent ya kesi za Serikali inapoteza ama Serikali inashindwa. Ninaitaka Wizara ije iseme, itoe tamko lake kwamba kwa nini Serikali inapoteza kesi nyingi? Ni kwa sababu gani kesi ziwe nyingi Serikali inashindwa? Kesi 1000 Serikali inashinda kesi mbili tu, inasikitisha sana! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumalizia kwa kuongelea kuhusiana na suala zima la majengo ya mahakama ambayo yamechakaa sana. Naomba Serikali katika bajeti yake iangalie ni namna gani itaweza kusaidia kufanya renovation ya majengo ya mahakama Tanzania nzima kwa sababu ya kuweza kuwasaidia wananchi kupata haki zao lakini pia kuongeza watumishi katika Mahakama zetu. Kwa sababu upungufu wa watumishi ume-deprive haki za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nimalizie kwa kukushukuru sana na kumshukuru Mungu kwa sababu ya kutoa speech hii ahsante sana. Naunga hoja mkono ahsante.