Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kwa kutoa pongezi kwa Serikali ambayo kimsingi imeonyesha njia. Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake kwa hii Awamu ya Tano kwa kweli nitakuwa mchoyo sana kama sijaweza kumpongeza kwa kazi anazozifanya. Ukiangalia wako wanaombeza hasa katika suala la kununua ndege, ukiangalia sasa hivi kwa kweli mimi mwenyewe nafurahia sana kuona hali hii ambako leo Tanzania tunaweza kuona huko angani ndege zinapishana na sisi tunasafiri. Naamua kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa ajili ya hili. Wako wanaobeza juhudi hizi kuonekana kwamba kipaumbele chetu sio ndege lakini ukweli ukiona baba amenunua kitu fulani nyumbani unaamua kumpongeza kwa sababu tu kwanza fedha zinatumika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si vibaya nikampongeza pia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi anazozifanya. Kwa kweli ni namuona mara nyingi katika shughuli za Serikali hasa kwenye maeneo yetu anapofanya ziara za kuhimiza maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi hizi sasa naomba niende kutoa mchango wangu katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa 2019/2020. Kuna mambo ambayo Mheshimiwa Dkt. Mpango anapaswa aangalie kwenye mpango huu. Nimeangalia sana na kusoma kitabu hiki cha mpango ukiangalia miradi mingi kwa kweli imetekelezwa. Ukurasa wa 31 anaonyesha miradi 1,595 ya maji imekamilika, kwa hili nimpongeze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado sasa tu natakiwa kuongeza kasi zaidi kwa sababu miradi hii tunayoiita miradi ya maji, kimsingi visima vingi vimechimbwa kila mahali na maeneo mengi sana kwenye maeneo yetu miradi hii haikuisha, imeishia nusu mengine 90%, mingine 40% hasa ukiangalia miradi hii mingi imeanza miaka mingi. Kwa hiyo, tusipoweka mipango ya kuimalizia miradi hii ni wazi thamani ya shilingi inashuka na miradi hii inakuwa ghali kwa maana hiyo Serikali inapata hasara hata ukipanga bajeti ya namna gani inaweza kuwa shida kumaliza miradi hii vizuri na wananchi wakapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri ni vizuri tunapopanga mipango yetu hii na tunapopanga fedha ziende kwa wakati ili wakandarasi walipwe wanapomaliza ili iweze kuhudumia wananchi na wakati huo basi inakuwa na kiwango kile kile kilichokusudiwa kumalizia mradi. Hii itasaidia pia katika uchumi wa nchi yetu, tutakuwa hatutumii fedha nyingi ambazo hazikukadiriwa kwa sababu unapochelewa kumaliza mradi ni wazi kabisa ule mradi unapanda gharama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende sasa kwenye eneo hili la miundombinu. Kwanza kwa kweli naipongeza Serikali kwa eneo hili la miundombinu barabara nyingi zimejengwa, maeneo mengi sasa yanapitika. Kuna eneo ambalo nalipongeza, Mheshimiwa Rais amefungua Daraja la Sibiti ambalo ukiangalia kwa kanda hii ya Simiyu, Shinyanga kuja mpaka Singida na Manyara kwenda upande wa Arusha utakuwa umetengeneza njia nyingine ya kupeleka usafiri wa hakika kwa wakulima au wafanyabiashara. Kwa hiyo, nashauri fedha zitengwe ili walau lile Daraja la Sibiti linalojengwa limalizike ili barabara hiyo inayokuja Singida inayopita Manyara inayokwenda moja kwa moja mpaka Arusha ifanye kazi kwani ni njia rahisi utakuwa umeokoa kilomita 200 kuliko kupitia Singida kwenda Babati kwenda Arusha kwa njia ile. Kwa hiyo, nilitaka nimuongezee ndugu yangu ili alielewe hili, barabara ile inapopita maeneo yale itakuwa na tija kubwa sana kwa maendeleo ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizi za Serikali, naona wazi na natambua juhudi za Serikali hasa katika suala la elimu. Niipongeze pia Serikali kwa kutenga shilingi bilioni 20.9 kila mwezi kwenda kwenye elimu bure, kwa kweli kwa hili mnastahili pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa zaidi elimu ya msingi imeboreka na mambo yanaenda si vibaya na elimu ya sekondari vilevile, lakini tunapoenda kwenye vyuo na kuhitaji wataalam kwenye viwanda tunayo kasoro kidogo katika mitaala. Ni vizuri kutafuta wataalam na kubadilisha modules zetu katika ufundishaji wa vyuo vyetu hivi, Vyuo vya Maendeleo ya Jamii ambayo itasaidia kupatikana kwa wataalam watakaosaidia katika viwanda vyetu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafundi mchundo, mafundi sanifu, hatuwezi kuwapata kama module na ile mitaala iliyopo katika vile vyuo vyetu itabaki vilevile. Ukiangalia China waliweza kufanya kazi nzuri wakati wa mapinduzi yao kwenda kwenye uchumi wa kati. Ukiangalia historia yao walitumia ujanja wa kufundisha wataalam wao ili wataalam hao wakaweze ku-cover kwenye kufanya shughuli za viwandani. Ukiangalia leo hii hata sufuria tunazopikia nchini hapa zinatengenezwa Kenya na maeneo mengine lakini tukiwa na watu wetu tukawafundisha ni rahisi basi tukawa na wataalam ambao watatengeneza vyombo hivi na viwanda vyetu vitapata wataalam na hivyo, tutakuwa tumewapatia watu wetu kazi na vijana watapata ajira na pia viwanda vyetu vitainuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote katika kilimo tunahitaji kufanya jambo moja ambalo ni rahisi kulifikiri, hatuwezi kutegemea kilimo cha mvua. Nchi nyingine ukiangalia na sisi bahati nzuri tuna mvua nyingi za kutosha, tuangalie namna ya kuzuia mvua zinazonyesha kipindi cha masika ili kuwa na mabwawa mengi tukalima kilimo ambacho kinaweza kusaidia. Kilimo cha mabwawa, tutakuwa tunazalisha kila mwaka na kwa vipindi mbalimbali bila kutegemea mvua, kwa hali hii itasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa nimeona kwenye mpango huu kwa kiasi kidogo sana umezungumzia kilimo lakini kilimo kinabeba kwa kweli eneo kubwa la Mtanzania.

Watanzania wengi wanatumia kilimo zaidi ya asilimia sitini na kitu mpaka sabaini. Kwa hiyo, ukielekeza nguvu nyingi kwenye kilimo Mheshimiwa Dkt. Mpango utakuwa umesaidia Watanzania wengi ambao kimsingi tunategemea kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niipongeze pia Serikali kwa kutekeleza huu mpango wa REA Vijijini. REA tatizo lake ni moja tu, wakandarasi wanadai hawana fedha, sasa sina hakika kama Serikali haiwalipi au ni nini kilichopo. Hakuna kiwanda bila umeme, tukitaka tuweze kuzalisha vizuri ni vizuri tukapeleka umeme kwenye viwanda vyetu na hii miradi ya mkakati kwa kweli tusipoangalia itakuwa shida sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakandarasi wengi sana saa hizi wanalia habari ya kutokuwa na fedha, sasa sina hakika kwenye mpango uliopita nini kilifanyika, lakini sasa hivi tunaona kabisa yako maeneo mengi wakandarasi wanasuasua. Sasa niombe fedha tunazozipanga mara nyingi ziende moja kwa moja kwenye mpango na tunapopanga tupange nini tunafanya na kipi ni kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa hiyo, kizuri ukishaweza kuziba sehemu hii ya wakandarasi hawa hakika mambo yataenda vizuri na Tanzania ya viwanda itapatikana ikiwa Serikali itawekeza katika suala la umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo niliwahi kushauri zamani kwenye mpango uliopita suala la gesi. Nimewahi kutembelea sana na kuangalia miradi hii ya gesi, sina hakika wapi imepotelea lakini nimeiona imendikwa kidogo kwenye ukurasa huu wa 25.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tumepata matumaini sana gesi inaweza kusaidia nchi hii, hasa kutupatia fedha za kigeni au kwa matumizi ya kawaida. Tungeweza kusaidia lakini tuone nini changamoto hasa za gesi ili tupate namna ya kusogea mbele ili…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa hili, nitakuwa mchoyo sana kama sijasema suala la mifugo na wafugaji. Tuone namna ya kuisaidia mifugo na wafugaji kwani kwa kufanya hivyo mambo yataenda vizuri sana. Mifugo yenyewe, kwa mfano ng’ombe kila kitu ni thamani kuanzia ngozi, maziwa, kwato na kadhalika, tukiweza kuweka viwanda ambavyo vitachakata mazao haya ya mifugo hakika Tanzania itasonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.