Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Segerea
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mawazo yangu katika Mpango wa Bajeti wa 2019/2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nishukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa miradi mikubwa ambayo inaendelea nchi nzima lakini specifically katika Mkoa wangu wa Dar es Salaam. Kuna mambo mengi ambayo yamefanyika katika Mkoa wa Dar es Salaam, tuna barabara za juu lakini pia hata hii treni ambayo inajengwa sasa hivi ya kisasa imepita kwenye Mkoa wetu wa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuishukuru Wizara ya Afya kwa kuleta pesa katika Jimbo langu la Segerea kwa ajili ya vituo vya afya. Vilevile nimshukuru Waziri wa Miundombinu kuhakikisha kwamba Jimbo la Segerea linakuwa na miundombinu mingi, japokuwa tuna changamoto chache lakini naamini kabisa mtazimaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, sasa naomba nitoe mchango wangu katika mpango wa 2019/ 2020 . Nashauri mpango utakaokuja 2019/2020 kuwepo na mpango wa kibajeti wa kuhakikisha kwamba tunamaliza mafuriko katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya na Morogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Dar es Salaam japokuwa sasa hivi siyo mji mkuu wa Serikali lakini bado ni mji maarufu na mji ambao unaiongezea kipato kikubwa Tanzania. Mafuriko yanapotokea kwanza yanaathiri uchumi, uchumi wa mtu mmoja mmoja lakini pia hata uchumi wa Serikali. Kama juzi hapa kulikuwa na mafuriko tuliona hata mabasi yetu mengi yalishindwa kutembea lakini pia wafanyabiashara walifunga maduka yao lakini siyo tu kwa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na Mikoa ya Dodoma, Morogoro pamoja naMbeya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri katika mpango unaokuja basi aweze kuweka mpango wa kibajeti wa kuweza kumaliza kabisa mafuriko haya ili wananchi waweze kukaa au wafanyabiashara waweze kufanya biashara zao vizuri na Taifa liweze kupata kipato. Kwa sababu tunapokuwa tunayashughulikia haya mambo wakati yanapotokea tunashindwa kuyamaliza. Kwa hiyo, nashauri sana kuwepo na mpango kwa ajili ya kumaliza mafuriko katika mikoa ambayo nimeitaja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine nashauri kuwepo na mpango wa kurasimisha makazi holela ambayo yapo kwenye mikoa tofauti tofauti kama Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine. Kwa hiyo, Mheshimiwa Dkt. Mpango aje na mpango wa kuweza kushirikisha wadau na sekta binafsi ambao wanaweza wakaongea na hawa watu ambao wako kwenye makazi holela waweze kushirikianao nao, aidha, kuwajengea nyumba kwa kuingia nao ubia labda anaweza kupewa apartment moja halafu nyingine wakachukua hao watu wanaojenga kwa ajili ya kusaidia kuondoa hayo makazi holela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakapoweza kuingia ubia na hawa wananchi ambao wanakaa kwenye makazi holela basi hata uchumi unaweza kukua kwa sababu kwanza tunawaongezea thamani ya maeneo yao lakini pia lile eneo ambalo tunaliita makazi holela linakuwa limetoka. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Dkt. Mpango aweze kuja na mpango ambao utaweza kuwasaidia wananchi ambao wanakaa kwenye makazi holela washirikiane nao kwa ajili ya kuwajengea nyumba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine nilichokuwa nataka kuongelea ni kwa ajili ya kutengeneza miundombinu.
Mheshimiwa Waziri aje na miundombinu rafiki kwa wajasiliamali wetu ambao wako Dar es Salaam kama mama ntilie, bodaboda, waweze kuwatengenezea miundombinu rafiki. Hawa watu hii ndiyo ajira yao, mfano bodaboda wapo Tanzania nzima na ajira nyingi ya vijana sasa hivi imekuwa ni bodaboda. Sasa hivi kinachoendelea ni kwamba wanapata ajali nyingi lakini pia wamekuwa na matatizo ya hapa na pale mara wanakamatwa na mambo kama hayo. Kama Mheshimiwa Waziri akija na mpango wa kuwatengenezea miundombinu mizuri ambapo wenyewe watakuwa wanapita lakini pia kuwatambua kwamba Dar es Salaam nina bodaboda kadhaa, hiyo pia itaisaidia Serikali kuweza kupata kipato wanapolipa kodi kujulikana kwamba hawa bodaboda wapo wapi sambamba na mama ntilie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine nataka niongelee kuhusiana na suala vijana wetu wanaomaliza vyuo. Vijana wetu ambao wanaomaliza vyuo wamejengwa katika mazingira kwamba unapomaliza chuo moja kwa moja unaenda kuajiriwa. Tofauti na watu ambao wamesoma ualimu, udaktari na vitu ambavyo unaweza ukaenda ukaajiriwa, mfano, kama mtu amesoma udaktari, anaweza akaajiriwa kwenye hospitali binafsi, mtu ambaye amesomea ualimu anaweza akaajiriwa shule binafsi lakini wale waliosoma sayansi, Serikali ije na mpango wa kuwajenga ili wakimaliza chuo wajue kwamba wanakuja kujiajiri na siyo kwamba wanakuja kuajiriwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inasema sasa hivi tunajiandaa kwa ajili ya kwenda kwenye uchumi wa kati, vijana wetu wengi hawawezi kushindana na vijana ambao wanatoka East Africa kwenye kufanya kazi. Mfano kama sasa hivi tunasema Serikali ya Awamu ya Tano ni ya viwanda lakini hatujawaandaa wale vijana kwamba wakimaliza tu chuo waje kufanya kazi kwenye viwanda, wanaishia tu kupata kazi ambazo ni za vibarua na kazi nyingine ambazo haziwezi kuwasaidia kiuchumi ili kupata wanachokipata. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja aje na mpango wa kuangalia vijana wetu ambao wanamaliza vyuo waweze kujiajiri wenyewe na isiwe wanamaliza chuo kwa ajili ya kuajiriwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja.