Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyenijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako hili tukufu, lakini nikushukuru sana wewe kwa kunipa fursa ya kuchangia katika mapendekezo haya ya mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kusema kwamba lengo kuu la Serikali ni ustawi wa Wananchi wake. Na Wananchi ndio msingi wa mamlaka na Serikali itapata madaraka na mamlaka yote kutoka kwa Wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya mpango yana mambo saba ambayo yamezingatiwa. Jambo la kwanza lililozingatiwa wakati Mheshimiwa Dkt. Mpango anaandaa mpango wake ni Dira ya Taifa ya Maendeleo mwaka 2025, lakini pia Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2016/2017, 2020/2021, lakini pia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi 2015/2020 pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuzingatia kuyandaa haya mpango pia ni lazima uzingatie Katiba, lakini pia uzingatie sheria na maelekezo ya viongozi. Maelekezo ya viongozi ni sheria kama ambavyo leo hii tunapitia mpango na baadae mapitio yale yatakuwa ni sheria ambayo yatakwenda moja kwa moja katika kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona nianze na hili na niseme tu kwa nia njema kabisa, kumekuwepo na sintofahamu ambayo baadhi ya Wabunge wamezungumzia kutoridhishwa na baadhi ya majibu ya Waziri wetu wa Ujenzi.

Sisi ni miongoni mwa watu ambao tulimpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi akiwa Waziri wa Maji, lakini amekuwa akitoa kauli ambazo wakati fulani haziridhishi na mimi nichukue nafasi hii kumuomba sana kwamba ile kazi nzuri aliyoifanya akiwa Waziri wa Maji basi aweze kuiendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo ambapo Mheshimiwa Rais aliweka ahadi. Ahadi zile ni sheria ambazo zinahitaji kutekelezwa, lakini sasa wewe Mheshimiwa Waziri ukinijibu mimi kwamba yale uliyoachiwa na Mheshimiwa Profesa Mbarawa wewe hauhusiani nayo, ninapata taabu sana kuelewa ni namna gani sasa umeamua kuwasaidia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sote tunafahamu kwamba sheria ya uongozi inatutaka viongozi kugusa mioyo ya wananchi wetu na kutugusa sisi wenyewe, leaders touch the heart before they ask for hands. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Waziri arekebishe na arejee kwenye kasi yake nzuri aliyokuwanayo akiwa Waziri wa Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 9 ya Katiba inazungumzia namna ambavyo shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya Wananchi wetu wote, lakini Ibara ya 9(d) inasema kwamba maendeleo ya uchumi wa Taifa yanakuzwa na kupangwa kwa uangalifu na kwa pamoja. Mheshimiwa Dkt. Mpango amezungumza changamoto nyingi ambazo kimsingi ndio mijadala ya Bunge letu hili tukufu, amezungumzia ugumu wa ukusanji wa kodi, amezungumzia kushuka kwa biashara za Kimataifa, amezungumzia upungufu wa wafanyakazi (ajira), lakini pia amezungumzia kupungua kwa misaada na pia amezungumzia madai ya watumishi.

Mimi nimuombe sana Dkt. Mpango wakati sasa anakuja kujibu hapa hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge, kwanza kabisa atambue kwamba lipo andiko liliwahi kutolewa na Tony Cliff katika kitabu chake alichowahi kuandika Building the Party ambacho kimetolewa mwaka 1975, akimnukuu Lenin.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Taifa lolote ni vyema tukajiuliza tulichonacho na namna ambavyo tunataka tukitumie, mimi kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji na kwa Watanzania wote, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa nia yake thabiti katika ya kutekeleza mradi wa kuzalisha umeme yaanai Stigler’s Gorge, mradi wa kuzalisha umeme kule Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki ni kilio cha muda mrefu sana cha Watanzania, kwa kuwa historia inatuambia kwamba jambo hili lilianzia miaka ya 56.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Mwalimu Nyerere yeye akiwa ni pioneer wa jambo hili, alisisitiza sana kwa mchakato huu wa uzalishaji wa umeme ambao utakwenda kuwasasidia Watanzania wote kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nipongeze Serikali, lakini pia niwapongeze sana wananchi wangu wa Jimbo la Rufiji kwa kuwa jambo hili wao walinikabidhi mwaka 2015 na ilikuwa ni ahadi yetu sisi nyakati za kampeni, lakini pia mwaka 2016 niliingia nalo ndani ya Bunge lako hili tukufu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, lakini pia nimpongeze sana Waziri wa Nishati atambue kwamba wananchi wetu wa Jimbo la Rufiji wanamuunga mkono sana, na kwa kuwa mradi huu upo Rufiji, asikate tamaa na sisi tunasema kwamba Serikali iendelee na mchakato wote wa kuandaa miundombinu ya ujenzi wa bwawa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zipo changamoto ambazo sisi wananchi tunaziona. Leo hii tunatambua kwamba hata tukiwauliza Mawaziri wetu wanaohusika suala la wakulima na wafugaji, halijazungumzwa sana katika vitabu vyetu hivi, hata Dkt. Mpango hajalizungumzia sana ambavyo ni namna gani Serikali itakwenda kuwasaidia wafugaji katika kuandaa maeneo ambayo wataweza kufanya mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais kutekeleza ujenzi huu wa uzalishaji wa umeme katika Bwawa la Stigler’s Gorge pale Rufiji, lakini tunahofia sana wananchi wa Rufiji, kwa kuwa leo hii mifugo imeingia sana katika eneo la Bonde la Mto Rufiji na pengine tunalaumu sana Serikali wakati ule miaka ya 2005
walipoamua kuondoa mifugo katika Bonde la Ihefu na kuleta mifugo katika Bonde la Mto Rufiji wakijua kabisa kwamba dhamira ya Mwalimu Nyerere ya mwaka 1956 ilikuwa ni kulilinda Bonde la Mto Rufiji na ndio maana Mwalimu Nyerere mwaka 1978 alianzisha sheria maalum kabisa sheria ya kuanzisha RUBADA ili kuweza kulinda Bonde la Mto Rufiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Serikali na nimuombe sana Dkt. Mpango, atakapokuja kuhitimisha hapa basi aone changamoto hii kubwa ambayo Mheshimiwa Rais leo hii anakwenda kutekeleza mradi huu wa Stigler’s Gorge, mradi wa kuzalisha umeme Bonde la Mto Rufiji. Lakini leo hii tuna mifugo zaidi ya laki tano ndani ya Bonde la Mto Rufiji, tunafahamu Bonde la Ihefu lilikufa na uoto wa asili ukaharibika, mvua zilikuwa hazinyeshi na leo hii tunakwenda kuandaa Bonde la Mto Rufiji ambalo mifugo zaidi ya laki tano imeingia kwenye Bonde, hakuna jitihada zozote ambazo zimeandaliwa na Wizara yaK ilimo, Wizara ya Mifugo na Wizara ya Ardhi na Wizara nyingine namna gani wanakwenda kutatua kero kubwa ya wakulima na wafugaji, ili sasa kumsaidia Mheshimiwa Rais wakati anakwenda kutekeleza mradi huu wa kuzalisha umeme, kuwepo na maji ya kutosha kwa sababu tunatambua kwamba mradi huu utahitaji uzalishaji wa maji yaani mvua za zaidi ya miaka miwili au miaka mitatu kuweza kujaza bonde lile katika uzalishaji umeme.

Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, atakapokuja kuhitimisha aelezee mpango wa Serikali ni namna gani sasa Serikali itakwenda kutatua kero kati ya wakulima na wafugaji. Ahsante sana.