Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bukene
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi hii ili jioni hii name niweze kuchangia taarifa hii ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na kwa hiyo mchango wangu kwa kiasi kikubwa utajikita kwenye mapendekezo ya Kamati yangu ya LAAC kama ambavyo yalivyo kwenye kitabu cha taarifa ya Kamati tulichokiwasilisha hapa Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yangu ya LAAC imependekeza mambo kadha lakini mojawapo ambalo nitaelezea kwa kwa kifupi kwanini tumependekeza ni kwamba katika kamati ya LAAC baada ya kupitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ya Serikali tumependekeza kuhusu Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, kwamba yale malimbikizo ya nyuma ya michango ambayo halmashuri zilipaswa kuchangia kwenye Mfuko huo kabla ya sheria mpya ya kufanya jambo hili kuwa sharia, malimbikizo yale kwa hali ya halisi kwa sababu hayawezi kulipika, tumeomba Serikali ianze mchakato wa kuangalia namna ya kuyafuta yale malimbilikizo ya nyuma kabla ya Sheria ya Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu kuwa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumependekeza jambo hili baada ya kuangalia kwa kina karibu halmashauri zote zilizokuwa zikija mbele ya Kamati yetu ukiangalia malimbikizo ya fedha ambazo halmashauri hazikuweza kuchangia kwenye Mifuko hii miaka ya nyuma kabla ya mwaka jana kabla hatujaweka sharia, utakuta halmashauri zina madeni makubwa ambayo kwa hali halisi hayawezi kulipika. Kwa hiyo tukaona kwamba hata kama tukilazimisha halmashauri zilipe malimbikizo hayo ambayo hawakuchangia itakuwa ni kazi bure kwa sababu ni figure kubwa ambazo hakuna halmashauri hizi za kawaida zinazoweza kulipa, kwa sababu kutokana na analysis imeonekana kwamba halmashauri nyingi haya malimbikizo ni makubwa kulingana na mapato yao ya ndani ya mwaka .
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo unakuta halmashuri mapato ya ni bilioni moja, lakini malimbikizo ambayo hawajayapeleka kwenye Mfuko ni zaidi ya bilioni moja, kwa hiyo hakuna namna halmashauri hii inaweza kulipa. Kwa hiyo tumependekeza kwamba yale malimbikizo ya nyuma, jambo la kukusisitiza hapo ni kwamba kabla ya mwaka jana tulipoamua kwamba jambo hili liwe sharia, huko nyuma ambako halmshauri zili-relax na kutengeneza malimbikizo mengi Serikali iangalie namna ya haya malimbikizo kuyafuta, tuanze upya kwa sababu nina uhakika Halmashauri zitaweza kulipa current figure, lakini huo mzigo wa nyuma tusaidie namna ya kuondoa, kwa hiyo hilo ni pendekezo letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo tumependekeza baada ya kuangalia taarifa ya Mkaguzi ni kwamba, bado kuna tatizo kubwa la upelekaji wa fedha za maendeleo kwenye halmashauri zetu ambazo zimeidhinishwa kwenye bajeti. Taarifa ya Mkaguzi kwamba bado halmashauri zinakuwa na bajeti za maendeleo ambazo zinaidhinishwa na Bunge lakini mwaka unaisha Hazina haijapeleka fedha za maendeleo kwenye halmashauri na miradi mingi inashindwa kufanyika.
Mheshimiwa naibu Spika, jambo hili limevunja moyo hasa katika maeneo ambayo miradi kwa hatua ya kwanza ilichangiwa na nguvu za wananchi. Leo hii ukipita kwenye majimbo yetu utakuta kuna maboma ya madarasa, nyumba za Walimu, zahanati, vituo vya afya ambavyo wananchi walichangia kwa fedha zao na ilikuwa kazi ya Serikali kukamilisha na halmashauri nyingi zimekuwa zikipitisha fedha hizi kwenye bajeti ili Hazina itoe ili kwenda kumaliziai kazi hizo ambazo zilianzwa na wananchi, lakini miaka yote fedha zimekuwa haziji pamoja na kwamba zipo kwenye bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo jambo hili limekuwa likivunja morali ya wananchi kuchangia kwa sababu wamechangia sana lakini maboma yamebaki maboma tu. Kuna maboma mengine yana miaka mitano, sita, saba mpaka 10 hayajaweza kumaliziwa na Serikali. Kwa hiyo tumeiomba Serikali kwamba miradi ya maendeleo ambayo fedha zake zinapitishwa na Bunge, Hazina iweze serious kuhakikisha angalau kwa 90% fedha zinakwenda kwa sababu jambo hili limekuwa likifunja moyo wananchi ambao wanachangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo Kamati imeliona na kupendekeza ni kuhusu udhaifu katika mfumo wa udhibiti wa ndani katika halmashauri nyingi. Taarifa ya Mkaguzi imebaini kwamba kumekuwa na miamala isiyofuata taratibu mingi katika miamala inayofanywa na halmashuri na sisi Kamati tumeona hili jambo linasababishwa na ubovu wa mifumo ya udhibiti wa ndani. Katika dunia ya leo unaweza ukadhibiti kiasi kikubwa miamala ambayo inafanywa kinyume cha taratibu kwa kuwa na mifumo ya kisasa inayozuia.
Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo kama unakuta halmashauri inahamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya amana, fedha ambazo labda zilikuwa kwa ajili ya malipo ya Walimu au mitihani, halmashauri inazihamisha na kuzipeleka kununua mafuta au kufanya jambo ambalo halijakusudiwa. Jambo hili unaweza ukalizuia kama una mfumo wa kisasa wa kudhibiti kwa sababu unatakiwa mfumo ndio ukatae. Ukitaka kuhamisha fedha kutoka kwenye akaunti ya amana kwenda kwenye jambo lingine ambalo halikubaliki inatakiwa mfumo ukukatalie, yaani inatakiwa jambo hili lizuiwe na mfumo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Kamati tumebaini kwamba mifumo na accounting package ambazo zinatumika kwenye halmashauri bado kuna haja zikaboreshwa zikawa za kisasa na zikaweza kuzuia irregularity mbalimbali ambazo kwa sasa zinafanyika kwa sababu mifumo inaruhusu. Ushauri mkubwa wa Kamati hapa ni kwamba TAMISEMI ijaribu kuja na mifumo ya kisasa ya udhibiti wa ndani wa namna hesabu zinafanyika ili kuzuia irregularity na miamala ambayo inakwenda kinyume cha taratibu. Haya mambo kwa dunia ya kileo yanatakiwa kuzuiwa na mifumo. Ukiwa na mfumo wa kisasa, wenyewe ndio unakuzuia. Ni kama vile sasa hivi ukitaka ku-raise purchase order ya kununua bidhaa fulani, kama kwenye bajeti hela hiyo haipo kwenye maana yake purchase order haitoki, huwezi kui- process ikatoka. Kwa hiyo tunataka mifumo ya namna hiyo kwa dunia ya kisasa ili kuweza kuzuia mambo ambayo hayatakiwi yafanyike. Kwa hiyo kuna kila haja ya TAMISEMI kuja na accounting package ya kisasa ili kuweza kuzuia mambo mengi ambayo yanaweza yakazuilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tumegundua ukosefu wa ujuzi wa kutumia mifumo kwa watumishi wengi wa halmashauri zetu. Kumekuwa na matatizo ya miamala mingi kushindwa kufanyika, ripoti kushindwa kuchapishwa katika halmashauri zetu kwa sababu mifumo iliyopo ya TAMISEMI watu walipo kwenye halmashauri nyingi wamekuwa hawana ujuzi na utalaam mzuri wa kuitumia. Kwa hiyo mambo mengi yanashindikana na sababu unaambiwa mfumo haufanyi kazi, lakini kumbe ni utaalam. Kwa hiyo tumependekeza kwamba TAMISEMI iwe na progamu za kutoa mafunzo kwa ajili ya watumishi wa halmashauri mbalimbali ili waweze ku-master hii mifumo ya kisasa iliyopo ili shughuli nyingi za halmashauri ziweze kufanyika kwa mifumo na taratibu za kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwa jumla taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa ambapo sisi kama Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa wajibu wetu ni kuangalia maeneo sugu katika taarifa ya Serikali za Mitaa ukilinganisha na miaka ya nyuma, ukiangalia trend utaona kwamba pamoja na kwamba matatizo bado yapo, lakini kwa kiasi kikubwa kadri tunavyokwenda matatizo katika maeneo yote yanapungua; maeneo ya malipo yasiyo na nyaraka, maeneo ya ukiukwaji wa taratibu za manunuzi na maeneo mengi yenye matatizo, ukingalia trend mtiririko ni kwamba kuna improvement kubwa na kwamba matatizo hayo yanaenda yakipungua kadri siku zinavyokwenda. Kwa hiyo ni imani ya Kamati kwamba jitihada zinazofanywa na TAMISEMI zikiendelea tunakwenda mahali ambapo kutaleta picha nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono taarifa yangu ya Kamati ya LAAC kwa asilimia mia moja na naomba kuwasilisha. Ahsante. (Makofi)