Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017

Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote naomba nichukue nafasi hii, kuzipongeza sana Kamati zote mbili kwa kazi nzuri ambayo wamezifanya na kwa ripoti ambazo wamezitoa ambazo zimetoa ufafanuzi na uchambuzi wa kina wa masuala mbalimbali. Inawezekana tukajadili mambo ya msingi na inawezekana wakati mwingine tukaingia kwenye siasa katika mambo ambayo hayastahili siasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu tunachokijadili hapa ni mahesabu ya Kamati hizi mbili, mahesabu yaliyokaguliwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali; Kamati ya PAC na Kamati ya LAAC na hizi Kamati kwa kawaida ndiyo zinafanya kazi kwa niaba ya Bunge, kwa niaba ya sisi wote hapa, katika kuchambua taarifa mbalimbali zinazohusiana na masuala ya mapato na matumizi ya fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema tu kidogo kwamba tunapozungumzia suala lolote kuna vitabu vya uhasibu ambavyo ni vya msingi ambavyo ndiyo vinatupa taarifa za kuzichambua. Hivyo vitabu visipoonesha chochote, ukichangia tofauti na hicho utakuwa una jambo lako kichwani. Sasa ukisoma Kanuni za Kimataifa za Utayarishaji wa Mahesabu ya Umma, ambazo ni IPSAS, ambayo tunaizungumzia sasa hivi imekuja na utaraibu kwamba tunatumia Accrual Account System. Pengine nikilisema hili watu wanaweza wasielewi nifafanue, kuna misingi mitatu unaweza ukatumia Accrual Account System, unaweza ukatumia Cash Accounting System, unaweza ukatumia Modified Accrual Account System. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka yote ya nyuma, miaka ya nyuma tulikuwa tunatumia Cash Accounting System ambayo tulikuwa tunalinganisha fedha ulizokusanya na matumizi uliyotumia, basi umemaliza. Unaposema Accrual Accounting System maana yake, mapato unayoiripoti kwenye vitabu ni mapato ambayo unaweza ukawa umepokea cash, unaweza ukawa hujapokea cash, lakini tayari huduma imeshatolewa. Unapozungumzia matumizi, tunayoyasema yanaweza yakawa ni matumizi ambayo tumeshalipa tayari fedha na yanaweza yakawa matumizi ambayo bado hujalipa fedha, lakini tayari unadaiwa unatakiwa ulipe,

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiyajua hayo vizuri, utazichambua hizo taarifa vizuri. Taarifa ya kwanza ambayo tunaichambua ni kitabu cha mali na madeni ambacho kinaitwa Statement of Financial Position inaonesha hayo na hili ukielewe hicho uelewe mali zilizopo, uelewe madeni yaliyokuwepo tarehe ile kwa tarehe 30 Juni mwaka 2017, ndiyo maana tunaita as at 30th June.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitabu cha pili cha muhimu ni kitabu cha mapato na matumizi ambayo tunaita Statement of Financial Performance. Katika hili tunaonesha mapato yote, yale tuliyopokea na ambayo bado hatujapokea lakini tunadai, yote tunaonesha. Ndiyo maana kwenye ripoti ile ya awali mlielekezwa kwamba kuna receivables, ambazo maana yake ni mapato ambayo tumeshatoa huduma, lakini bado hatujayapokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hayo kwa mantiki hiyo hayo ukiangalia kwenye exchequer huwezi kuyaona, sitosikia, kwa sababu ni mapato bado hujapokea, ndivyo hivyo kwenye matumizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitabu cha tatu na cha msingi kinaonesha mtiririko wa fedha yaani Cash Flow Statement; sasa ukiunganisha Cash Flow Statement itakavyoonesha balance huko ilingane na kile kitabu cha mali na madeni ile cash and cash equivalent inayokuwa reported pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiendelea kuchambua kuna kitabu cha nne changes in equity; kuna kitabu cha tano kinaitwa Budgetary Performance Report. Budgetary Performance Report ndiyo inatupa taarifa ya bajeti nzima ya Serikali na matumizi yalivyofanyika katika mwaka huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unapokuja na hoja kwamba kuna trilioni 1.5 imepotea cha kwanza tunakuuliza unatumia kitabu gani ambacho taarifa hizo zipo? Ndiyo maana ukisoma kwenye vitabu vyote hivyo nilivyovisema ukiongeza Directors report, sijui Accounting Officers report, hakuna hayo. Mtu pekee ambaye angeweza kutuambia hayo kwamba kuna matatizo ni CAG. Kwenye ripoti yake alipoileta hakuonesha kama kuna tatizo, haiwezekani CAG ambaye ni Mtaalam ambaye ana wataalam waliobea akaandika eti akaficha trilioni 1.5 haiwezekani, hilo ni ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ya pili, kwenye Kamati ndiyo maana hoja hii tunayoijadili, ni hoja ambayo imetoka kwenye uchambuzi wa mitaani ambao haupo kwenye misingi ya vitabu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mtu anayeelewa ukichukua huu ukurasa wachambua hata hili ripoti ya Kamati inayoongoza na wenyewe wenzetu, ripoti hii kuanzia pale ukurasa wa 21, 22 23 mpaka 24 wameonesha maana ya reconciliation kuanzia mwanzo mpaka mwisho, mmesoma hizi mmezielewa? Inawezekana tunajadili kwa sababu hatujapata tafsiri hizi za figures. Naomba tuwe na muda wa kutosha wa kuchambua kilichoandikwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nafurahia sana ninapoona kwamba CAG hajaonesha, Kamati yenyewe ya kwao haijaonesha, ambayo ndiyo msingi wa majadiliano ya humu Bungeni. Kwa hiyo na maazimio yao waliyoyasema wameonesha waliuliza, je fedha zilipotea? Wakasema hazijapotea, sasa tunapoteza wa nini? Kwa hiyo, hilo naomba, liwe vizuri, lieleweke vizuri na tusitake kupotoshana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nataka kusema, vitabu vinafungwa tarehe 30 Juni. Baada ya vitabu kufungwa kuna miezi mitatu, miezi mitatu ile maana yake nini? Maana yake kama kuna matumizi mengine yako yuko kama kuna adjustment, mnatakiwa mzifanye, ndiyo maana mnapewa miezi mitatu. Kwa mfano, inawezekana ikawa watu walichukua imprest, imprest hatuzitambui kama matumizi mpaka pale zinapokuwa zimekuwa retired; sasa zile zote zitakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ukija mwezi wa Tisa ukifunga na ukifunga mwezi wa Tisa unapopeleka kwa CAG vile vinaitwa draft financial stastement, draft maana yake nini, maana yake unapompelekea Auditor akienda akakagua kama kuna maeneo yakurekebisha atakwambia karekebishe hiki, usiporekebisha nitakupa qualified opinion, ukirekebisha hakuna hoja; akikwambia fanya hiki, ukafanya, hoja imekwisha, ndiyo maana ya audit.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri kuna haja ya Bunge lako Tukufu kupewa muda wa kutosha na kupatiwa semina ya kutosha ya namna ya kuchambua hivi vitabu, kwa sababu tukiipata hiyo, nadhani hata matatizo ya tofauti zetu hizi yatakuwa yamekwisha. Hata hivyo, nataka kusema tunafanya kazi nzuri, lakini tunahitaji kuwa na uchambuzi wa kisayansi na wa kina ili tuchangie vizuri tuisaidie Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nawashukuru sana na nawapongeza wote. Ahsanteni sana. (Makofi/Vigelegele)