Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Zaynab Matitu Vulu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kusimama hapa leo na namuomba Mwenyezi Mungu alijalie Bunge hili tuendelee kujadiliana kwa salama na amani katika Kamati hizi mbili ambazo zinalenga kubeba uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatoe hofu Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, inapotokea Mbunge yeyote anapochangia, anapotoka nje ya mstari msisite kusimama kwa mujibu wa kanuni na kufafanua yale ambayo yanapaswa yafafanuliwe. Maana kuna wengine hapa wanataka kutulisha matango pori na sisi hatutaki kula matango pori, tumeona bundi na bundi wameshindwa. Kwa hiyo, endeleeni kuchapa kazi na fanyeni kazi yenu kwa uadilifu kama ilivyo. Ninyi mnaisimamia Serikali na tunapaswa na wananchi wanapaswa kujua Serikali yetu inafanya nini, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia suala la uwekezaji. tunapozungumzia suala la uwekezaji Serikali inaweka mkono wake ili kuhakikisha uchumi na mapato ya nchi yetu yanaendelea. Niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuifufua ATCL, imenunua ndege sita hadi sasa na inahakikisha uchumi unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimsaidie mwanangu, mwanafunzi wangu Ester Bulaya, unapojua kuendesha gari ya Volkswagen hushindwi kuendesha V8 na unapotoka kuendesha V8 huwezi kushindwa kuja kuendesha beetle, IT au corolla kama unavyosema mwenyewe. Kwa hiyo, mwanafunzi wangu naomba hilo ulizingatie usisahau ulipotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anapozungumzia kwamba marubani wanakosea kukosea ndege, anataka kuupotosha umma. Mimi nasema Serikali imefanya jambo zuri na la uhakika kufufua uchumi wa ndege na kuendelea kujenga reli ya SGR. Ndege na reli zikiwa pamoja uchumi utaimarika.

Tunaomba tu Serikali ihakikishe na suala la bandari linawekwa katika moja ya ajenda zake ili wafanyabiashara badala ya kutumia magari kutoa hapa kupeleka maeneo mengine kwa kutumia barabara sasa wanaweza wakatumia hiyo reli na ikapokelewa bandarini na uchumi ukaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongeze kusema kwamba tunahitaji kuyasimamia na kuyaboresha mashirika yetu ya umma. Iangalie uwezekano, wa pale panapohitaji kupeleka mtaji basi ipeleke mtaji kwa wakati, wakati huo huo kuangalia rasilimali watu. Rasilimali watu katika mashirika yetu ni muhimu sana, wao ndio watasaidia kuhakikisha kazi zinakwenda vizuri na kwa weledi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la bodi za Wakurugenzi na Wenyeviti, mashirika yahakikishe kwamba bodi za Wakurugenzi na Wenyeviti wanateuliwa kwa wakati ili waweze kusimamia shirika alilopangiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Shirika la SUMA JKT, hili shirika lina vitengo vingi vya kufanyia kazi, lakini nishauri kama Kamati ilivyoshauri, wale vijana wanaokwenda JKT iwe kwa mujibu wa sheria au kujitolea kuwekwe na sera ambayo itawasaidia na kusaidia shirika na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, wanaokwenda kufanya kazi za kujitolea, wafanye mafunzo ya kijeshi ambayo ni nidhamu, lakini baada ya hapo, waende kwenye Shirika la SUMA JKT ambako kule watafundishwa kushona, kulima, kutengeneza maji kwa ajili ya biashara; na mbinu za ujenzi na ujenzi ambao hauna gharama kubwa. Nao wakitoka hapo, wanakwenda kujiajiri wenyewe ama wanaweza wakaajiriwa kwenye Taasisi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hili shirika likiwezeshwa vizuri, linaweza likasaidia, kwa mfano, tukisema shirika hili lipewe kazi ya kushona uniforms za Jeshi zote, kwa sababu tayari wana kiwanda cha nguo. Pia tunaweza tukasema washone viatu vya majeshi yote, kwa sababu tayari wana kiwanda cha kushona viatu na ngozi. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikaona ni jinsi gani tunaweza tukaisaidia SUMA JKT ikawa kiwanda cha kuzalisha bidhaa lakini vilevile ikawa kiwanda cha kuzalisha rasilimali watu, wakitoka hapo wakaenda kufanya kazi maeneo mengine ama wajiajiri wenyewe. Kwa sababu sehemu kubwa ya vijana wetu wako mitaani wamezagaa, wengine hawana utaalam lakini wana elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, elimu wanayoipata shuleni na elimu watakayokuwa wameipata vyuoni, wakienda huko wanaweza wakapata utaalam wa kuja kufanya kazi za kujipatia kipato; na vilevile kipato watakachopata kitakatwa kodi na hiyo kodi itaingia kwenye sehemu ya kipato cha Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri tukaona ni jinsi gani tunaweza kuisaidia Serikali kwa kuzalisha vijana ambao watakwenda kufanya kazi na kujiajiri, wakati huo huo SUMA JKT na yenyewe ikafanya kazi ya kuwafundisha hata maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo, SUMA JKT wamekopesha matrekta, tunaiomba Serikali isimamie upatikanaji wa fedha ambazo zinatokana na malipo ya matrekta waliokopa watu. Matrekta hayo, mengine Wabunge tumo humo tunaodaiwa. Tunaomba Bunge lisimamie kama wamo Wabunge waliokopa, basi Serikali ilete barua huku ili hela zilizokopwa zirudishwe kwa wanaohusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Mimi ni miongoni mwa Wajumbe wa Kamati ya PIC.