Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Albert Ntabaliba Obama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buhigwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii nami nichangie kwenye taarifa hizi mbili. Kwanza nawashukuru Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati zote hizi mbili kwa ripoti nzuri ambayo wameweza kutuletea hapa mbele yetu; lakini pili niendelee kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa inayofanya kutuletea maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuanza na moja hili la Mheshimiwa Msigwa ambalo alisema, economic growth haiendani na development growth; ikiwa na maana kwamba anaongelea pato la Taifa. Kwanza tuipongeze Serikali yetu kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia 2015, 2016 na 2017 uchumi umeendelea ku-grow kwa 7% ambapo ni kitu kikubwa sana, lazima tujipongeze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mchungaji Msigwa ameendelea kuchanganya, haelewei maana ya pato la Taifa kukua. Viashiria vya uchumi kukua ni kuongezeka kwa miundombinu hii ambayo inaendelea katika nchi yetu. Kwa hiyo, unapoona miundombinu inaendelea kukua, ni moja ya kiashiria kwamba uchumi umekua na maendeleo sasa yanaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ya kupatikana umeme wa uhakika kuliko tulipotoka, vilevile ni kiashiria cha kwamba pato limeongezeka na huduma ya umeme sasa inakuwa nzuri vilevile na huduma za jamii. Hivyo, vyote ni viashiria ambavyo vinaonyesha uchumi wa nchi kukua. Kwa hiyo, haina uhusiano wa moja kwa moja na fedha zake za mfukoni kama hufanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niendelee kuipongeza Serikali kupitia TRA, wamefanya kazi nzuri chini ya Mkurugenzi, Mheshimiwa Kichele. Ukiangalia mwenendo wa makusanyo ya nchi yetu, mapato yameendelea kuwa mazuri. Naendelea kumpongeza Waziri wa Fedha na timu yake ya wataalam wamefanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, wamekuja kwenye Kamati yetu, wamejaribu kuonyesha mapato ya nusu mwaka: Je, wameweza kufanyaje katika makusanyo? Ukienda kwenye mapato yanayotokana na kodi, jumla yake wameweza ku-achieve kwa asilimia 91, lazima tuwapigie makofi kwa namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma namba mbili, kuhusu ushuru wa forodha lengo la mwaka ni shilingi bilioni 1.2, lakini wameweza kukusanya shilingi bilioni 588 ambayo ni asilimia 88.7. Ni jambo kubwa ambalo inabidi tuwapongeze. Kwa hiyo, TRA mnafanya kazi nzuri, hongereni sana na Waziri wa Fedha mnafanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye mwenendo wa misaada na mikopo nafuu hadi Desemba, ukiwapima kwa miezi sita ufanisi wao ukoje? Watu wanasema wafadhili hawatupi fedha, mikopo haiji; naomba niwaambie wameweza ku-achieve kwa lengo la nusu mwaka, wamefikia asilimia 66.4. Wapigieni makofi kwamba Serikali inafanya kazi nzuri. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuendelee kuwapigia makofi kwa sababu ukiangalia mfumuko wa bei kwa nchi za Afrika Mashariki, sisi sasa Januari tumeweza kufika 3%. Mpaka Desemba, Kenya walikuwa 5.7% ambao wako juu, sisi tuko chini, ni lazima tuwe proud na tunachokifanya. Kwa hiyo, ni jambo zuri, tuendelee kuwapongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimpima, Mheshimiwa Waziri Mpango, kaka yangu: Je, fedha anazokusanya anapeleka zinapoitajika? Kwa miezi sita mfano, kwa matumizi ya kawaida kwa lengo lake alivyojipangia kwa nusu mwaka amefikisha 62.7%. Kwa nini usimpe haki yake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia na madeni mengine; ulipaji wa madeni ya ndani na nje, malipo na riba za ndani amefikia asilimia 32. Malipo ya riba na mitaji ya nje amelipa kwa asilimia 53 ya lengo. Kwa hiyo, naweza nikasema, Wizara ya Fedha ukiipima na nchi nzima kwa ujumla tunavyotekeleza bajeti yetu, Mheshimiwa Zitto unacho hiki kitabu umesoma, tunaenda vizuri na uende kwenye media na uwaambie Watanzania tunaenda vizuri. Kwa hiyo, ukiwapima, wanaenda vizuri kwa viashiria vyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishukuru sana Serikali kwa kazi nzuri sana inayofanya chini ya uongozi wa Jemedari JPM.