Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mtwara Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema nami kuweza kusimama mbele ya Bunge tukufu ili niweze kuchangia hoja mbili ambazo zimewasilishwa katika Bunge letu Tukufu. Pia napenda niwapongeze Wenyeviti wote wa Kamati kwa taarifa nzuri sana ambazo wameziwasilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia maeneo machache sana, kwanza nikianza na taarifa ya mwaka ya Kamati ya Uwekezaji Mitaji ya Umma (PIC). Niwapongeze wote waliochangia nami niungane nao katika kuiomba Serikali kuziongezea mitaji taasisi zetu ambazo ziko chini ya Msajili wa Hazina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndio maduka yetu, hivi ndio viwanda vyetu ambavyo Serikali inaweza ikatuongezea pato letu la Taifa na katika biashara yoyote ni lazima uwekeze ndipo uweze kuvuna. Kwa hiyo, kwanza nashauri Sheria ya Msajili wa Hazina ipitiwe upya ili kuweza kumwezesha Msajili wa Hazina kufanya kazi zake kwa ufanisi. Pia napendekeza ikama katika Ofisi ya Msajili wa Hazina iongezwe na pia katika kuipitia sheria napendekeza ikiwezekana tuanzishe Mfuko wa uwekezaji ambao wenyewe ndio utakuwa unatoa mitaji kupeleka katika mashirika yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo mashirika ambayo tumeingia ubia, PUMA tuna ubia lakini tunayo mashirika mengi kama TPDC imeingia ubia na mashirika mengi kama MMP na pia tumeingia ubia sigara, tumeingia ubia ALAF, lakini katika ubia ule uwekezaji wetu kidogo ni mdogo sana ukilinganisha na wabia wenzetu. Sasa kwa kuwekeza kidogo inapelekea mapato yetu au gawio letu kwa kweli kuwa kidogo kwa sababu tunawekeza kidogo. Kwa hiyo napendekeza tuwe na mfuko wa uwekezaji ambao utamwezesha Msajili wa Hazina kuweza kutoa mitaji katika yale mashirika ambayo anayasimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ambalo nataka nichangie ni kuhusu suala la ATCL. Niungane na wenzangu kuipongeza Serikali yetu kwa kuwa na Shirika letu la Ndege. Napenda niwaambie kwamba Shirika la Ndege tusiangalie balance sheet ya shirika kwamba, faida tumetumia kiasi gani tunapata kiasi gani, tuangalie faida katika uchumi mpana, idadi ya watalii walioletwa, uwekezaji utakaokuja. Katika kuthibitisha hilo nendeni mkaangalie Shirika la Emirate ambalo sasa hivi kila mtu analipigia mfano, wakati linaanza lengo lake kubwa halikuwa kuweka faida. Lengo lilikuwa ni kuifanya Dubai iwe kituo cha uwekezaji, iwe kituo cha utalii. Sasa hivi Dubai asilimia 20 ya mapato yake...
T A A R I F A
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unitunzie muda wangu, taarifa naipokea, na ndio maana nilikuwa nasema naungana na Serikali kwa kununua ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu leo labda China hata Tanzania hawaijui, lakini siku ndege yetu ikitua Guangzhou, watu wataanza kujiuliza, Tanzania iko wapi, kuna nini, kuna vitu gani vinapatikana huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dubai kuanzia Disemba mpaka inafika Machi hoteli zote zimejaa, mji umejaa na pato la Taifa la Dubai kwa mwaka 2018 asilimia 20 lilichangiwa na utalii na utalii huo ulibebwa au watalii hao walibebwa na Shirika la Emirate na walichangia katika uchumi mpana kwa watalii kwenda pale. Kwa hiyo, niwaombe ile habari ya kusema sijui tumenunua hivi, tumepata vile, hiyo ni biashara ya machungwa, lakini unavyoangalia biashara kama ndege unaangalia katika uchumi mpana, idadi ya watalii shirika litatangaza nchi yetu na italeta multiplier effect kubwa sana kuliko ambavyo watu wanafikiria, lakini pia nina imani kabisa shirika letu litakuja kufanya faida na kupunguza gharama za usafirishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Mtwara ambako Bombadier zimekatiza kwa sababu ya Ruvuma, nauli ya ndege kwa kutumia Precision ni kubwa kuliko eneo lingine lolote ndani ya Tanzania hii. Kwa hiyo, kwa kuwa na Shirika letu pia tunasaidia kupunguza gharama za usafiri wa anga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)