Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI WA MITAJI YA UMMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi napenda sana niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango mizuri ambayo kwa kweli imetupa afya njema sisi Wanakamati wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na hoja mbalimbali, na taarifa yetu ya kamati imechangiwa na Waheshimiwa Wabunge 21. Sina haja ya kuwataja wote lakini niwashukuru wale wote ambao wamepata nafasi ya kuzungumza na hata mlitoa kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kamati hii ukiangalia msingi wake mkubwa ni kuangalia mapato ambayo hayatokani na kodi (no-ntax revenue) na ndio kigezo kikubwa sana cha uhai wa ufanisi wa Kamati hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii imejikita kuelezea ni mambo gani ya msingi ili Serikali iweze kuyazingatia. Kama itafanya vile maana yake tutapunguza ile nakisi ya bajeti kupitia mapato ambayo hayatokani na kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wachangiaji wengi wamezungumza lakini ningependa nianze na jambo moja kidogo hapa la kufanya clarification.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa ambazo Kamati inazo, Serikali ina taasisi 11 ambazo ina ubia wa kuanzia asilimia 50 na chini ya asilimia 50. Moja ya taasisi hizo zimechangia sana kupata mapato ya zaidi ya shilingi bilioni 35.9. Katika taasisi zile tatu zinazoongoza kuna Benki ya NMB iliyotoa shilingi bilioni 10 kama gawio, PUMA Energy ambayo Serikali ina asilimia 50 na ninaomba nirudie kwamba Serikali tuna ubia wa asilimia 50 kwenye Shirika la PUMA Energy. Sasa nasikitika sana kama kuna watu ndani ya Bunge au ndani ya Serikali hawa-acknowledge hiyo, huyu ni mtoto wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna asilimia 31.8 kwenye Benki ya NMB, huyu ni mtoto wetu, tuna asilimia 30 kwenye Benki ya NBC, huyu ni mtoto wetu. Tuna asilimia 25 kwenye Tanzania Planting Company Ltd., huyu ni mtoto wetu na ametoa gawio kubwa kuliko wote la shilingi bilioni 13.4. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sana na naamini kwamba kama una mtoto msaidie na kama ana mapungufu mrekebishe lakini ningeona kwamba ni fahari tuone kwamba taasisi hizi tuzibebe vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inawekeza kwenye Shirika la Ndege - ATCL na Mheshimiwa Rais alikuwa very clear na akasema kwamba Serikali imewekeza pesa nyingi, tunawakabidhi ATCL muendeshe shirika hili, mkishindwa nawanyang’anya nawapa hata Precision. Maana yake ni kwamba tunataka uwekezaji huu uwe na tija kwa Watanzania na tunadhani ni fahari kwa wewe Mtanzania kutumia mali ya kwako, brand ya kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa sana kwamba Watanzania tujawe na uzalendo; na hata wenzangu waliochangia akiwemo dada yangu Mheshimiwa Ester Bulaya, amezunguma vizuri, lakini hoja ni kwamba uwekezaji kwenye ndege huwezi ukapata faida leo au kesho. Mashirika yote ya ndege hapa duniani hayapati faida peke yake, isipokuwa yanachochea kukuza uchumi kwenye sekta zote za uchumi wa nchi hiyo. Kwa hiyo, uwekezaji huu tusiuangalie kwa kuangalia faida, tuangalie una multiply effect gani kwenye uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na haya kuna suala la kujua kwamba TRA wanakusanya kodi, Msajili wa Hazina (Treasury Registrar) yeye anakusanya mapato yasiyotokana na kodi. Mapato yapo ya aina tatu makubwa; kuna gawio, redemption of excess capital au mtaji uliozidi na kuna asilimia 15 ya mapato ghafi, haya ndiyo makusanyo yanayopitia katika Ofisi ya TR. Ninachoomba Serikali huyu mtu awezeshwe, kwa maana ya staffing, technology lakini vilevile na namna ya kupata wataalam wenye weledi kuendesha Ofisi ya Msajili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiyafanya haya na kwa bahati nzuri nimeshafanya consultation na Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mawaziri husika wameona umuhimu huu kwamba Ofisi ya TR lazima tuiwezeshe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine cha msingi katika hili ni suala la Seikali kutokulipa madeni…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwenyekiti naomba utoe hoja muda umeisha.

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI WA MITAJI YA
UMMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika kumi tayari?

MWENYEKITI: Ndiyo, naomba utoe hoja.

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI WA MITAJI YA UMMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naomba basi niwashukuru wale wote waliochangia ukiwepo wewe mwenyewe kwa kuweza kutupa fursa hii; na basi naomba nitoe hoja kwamba lipokee maoni na mapendekezo ya kamati yetu, ahsante.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.

MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.