Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru sana kwa kunipa nafasi kwa kuwa mtu wa kwanza kuchangia ili tujaribu sasa kulielekeza Taifa kwenye mambo ya msingi kabisa ambayo sisi tulitamani tuyaone yanafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kuunga mkono, Taarifa ya Kamati ambayo imejaribu kuonesha upungufu mbalimbali ulioko kwenye utekeleza wa azma ya Mheshimiwa Rais inayohusiana na masuala ya viwanda na niishauri meza yako moja kwa moja kabla sijaenda mbali kwamba kwa kweli kwenye suala la viwanda kama ambavyo taarifa yetu ya Kamati imeonesha kuna matatizo makubwa sana, hasa zaidi kwenye utekelezaji wa hili wazo la kuwa na viwanda, lakini pia ukienda kwenye suala la viwanda vilivyobinafsishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo Mheshimiwa Rais aliwaita wawekezaji kwenye sekta ya madini, lakini pia Mheshimiwa Spika naye aliunda hapa tume maalum ya kuchunguza masuala yanayohusiana na madini na makinikia na majibu yaliletwa humu ndani. Sasa nipendekeza kama inawezekana Mheshimiwa Spika naye afikirie kutengeneza tume maalum ya Kibunge ambayo itakwenda kufanya uchunguzi na kuleta majibu yanayohusiana na masuala ya viwanda zaidi ya 150 vilivyobinafsishwa kwa sababu kimsingi hakuna chochote kinachoendelea kwenye hivi viwanda, viwanda pekee vinavyofanya kazi ni viwanda kumi tu kwa hiyo tunamrudisha nyuma sana Rais kwenye wazo lake la viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ukifuatilia kabisa michango inayotolewa na Wabunge, lakini na michango mbalimbali maeneo mengi inaonesha kabisa la Rais la kutaka kuwa na viwanda kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, linakwenda kufeli. Miaka ya 1980 na huko chini kama tunavyoongea hapa tulikuwa na viwanda zaidi ya 150 vya Serikali vilifeli. Sasa sidhani kama kuna utafiti uliofanyika unaoonesha kinaga ubaga ni kwa nini viwanda hivi vilifeli ambavyo Rais anasimama navyo na tumetumia kama ndio sera ya nchi yetu kuhakikisha tunakwenda kuboresha viwanda. Vinginevyo kama hatutafanya haya, vile viwanda vinavyotajwa 3000, viwanda vinavyotajwa 4000 na vyenyewe vitakwenda kufeli kama ambavyo vimefeli hivyo viwanda vingine huko nyuma, tena vilikuwa vichache tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe kushauri kwamba tufanye mabadiliko ya makusudi kabisa ya sera ya viwanda, tufanye mabadiliko makusudi kabisa na utafiti kuona hivi viwanda tunavyovijenga masoko yake yako wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye taarifa ya Kamati ukurasa wa 16 kwenye taarifa ya Kamati hii ambayo iko hapo mbele yako, kwenye ukurasa wa 16 wanaongelea hapa habari ya import duty zaidi sana kwenye sukari ya viwanda. Hawa wenye viwanda wana lalamika kwamba Serikali imekuwa ikiwatoza wao pesa kwa ajili ya kuingiza sukari ya viwanda inayotumika kuzalisha soda na vinywaji vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa bahati mbaya sana kwa miaka mitatu sasa Serikali haijarudisha hii pesa kwao na inaonyesha wazi kabisa na labda Waziri aje kutuambia hapa baadae kwamba Serikali haina mpango wa kurudisha hizi pesa za watu wenye viwanda. Sasa badala ya kuwazungusha kila siku ni bora watuambie moja kwa moja kwamba hizo pesa hazitapatikana kwa sababu hazipo kwenye mfuko wowote na kwa ufupi Serikali haina hiyo pesa ambayo inatakiwa irudishwe kwa watu wenye viwanda kutokana na hii pesa yao. (Makofi)

Kwa hiyo, kwa vyovyote vile mpaka sasa hivi Serikali haina nia ya kufanya hicho kitu na badala yake imeamua kuwazungusha watu walio-deposit kule pesa, kwa hiyo, iamue kuacha au kutokuendelea na kukusanya hii pesa kwa sababu haina uwezo wa kurudisha na tunasababisha viwanda vinakufa, watu wanashindwa kuendeleza na kufanya mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda ukurasa wa 20 kwenye hili jambo tunalosema Mheshimiwa Rais ana nia njema ya kutaka kuhakikisha Tanzania inakuwa ya viwanda. Lakini soma tu pale, kwamba katika pesa za maendeleo zilizotengwa bilioni 80 zimekwenda bilioni nane tu ambayo ni sawa sawa na asilimia tisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi na ninyi tujiulize kwamba Mheshimiwa Rais anataka Tanzania iwe ya viwanda, lakini pesa za viwanda ambazo zinatakiwa zitolewe na Hazina, pesa za maendeleo haziendi. Kwanza zinakwenda kidogo, tunaambiwa hapa ni asilimia tisa tu. Hata hivyo katika hiyo asilimia tisa na yenyewe haiendi kwa wakati, matokeo yake, watu wanashindwa kufanya shughuli zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeongea hapa habari za SIDO, SIDO ndio tunataka iwe sehemu kubwa ya chachu ya viwanda Tanzania tuwaongezee SIDO nguvu, ili waweze hii sera ya viwanda iweze kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kimsingi hakuna lolote linalofanyika na awamu hii kuhusiana na masuala ya viwanda kwa sababu hawakujiandaa, wameamua kuja na kitu ambacho utekelezaji wake ni hauwezekani, labda waamue kutafuta namna nyingine ya kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo yanayohusiana na viwanda turudi sasa kwenye viwanda vikuu; na tumejadili hapa mambo mengi, nimeona watu wanajadili masuala ya korosho, Mheshimiwa Waziri pale naye kajibu. Sasa ukiingia upande wa biashara, kwa sababu
tunajadili masuala ya viwanda, pamoja na biashara, kimsingi Mawaziri hawa hawa ambao leo wanatoa maelezo kuhusiana na masuala ya viwanda vya korosho pamopa na bei za korosho kwa ujumla ndio hao ambao walikuja ndani ya Kamati. Juzi hapa Mheshimiwa Hasunga alikuwa anamjibu Mheshimiwa Bobali, anamwambia kwamba uzalishaji wa korosho gharama yake mpaka sasa hivi, kwa hiyo hata wakiuza kwa shilingi 4,180 haina maana kwamba wao wanapata faida kubwa. Ni Waziri huyu huyu na kitabu ni hiki, alipokuja ndani ya Kamati alisema hivi, kwamba mpaka sasa hivi wamepata watu wanaotaka kununua korosho kwa shilingi 3,500 lakini wamewakatalia, kwa sababu gharama za utaratibu wa uendeshaji wa zao la korosho kwa kilo moja mpaka sasa hivi, imefikia shilingi 3,850. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika shilingi 3,850 wao wanakwenda kuuza shilingi 4,180. Sasa tunataka watueleze ile gap kati ya shilingi 3,850 au shilingi 3,300 mpaka shilingi 4,180 hii pesa iliyozidi nani anakwenda kupewa? Kwa sababu haioneshi nia ya kutaka kuwarudishia Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hapa tulisema pia, tunachofanya sisi ni biashara na Serikali imeamua kufanya biashara kupitia benki zake hapa. Wanasema wenyewe kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko Serikali imeamua kufanya biashara ya Korosho sasa wanawazuia. Kilichokuwa kinafanyika mwanzoni, tuseme labda kwenye hili suala la Kangomba ambalo watu wanafikiri ni dhambi kubwa sana, na mimi sioni kama kuna dhambi yoyote inafanyika. Kangomba ni facilitators kama walivyo facilitators kama walivyo facilitators wowote kwenye mazao ya biashara, sawa sawa na watu walivyo kwenye pamba, sawa sawa walivyo watu kwenye mahindi, hata kwenye nyanya, wanasema wafuate mfumo unaotakiwa, hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunajiuliza hivi kutoa nyanya kwa Mkulima na kuipeleka sokoni ni dhambi? Kutoa mahindi kwa mkulima mmoja mwenye uwezo wa kuvuna wa gunia tatu, akaja kuniulizia mimi mwenye uwezo wa kujikimu pesa ya maisha lakini naweza kuvuna hata gunia mia nikazipeleka kwenye maghala makubwa, hii ni dhambi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndicho kinachofanyika kwa wauzaji au Wafanyabiashara wa korosho. Serikali kabla haijapeleka pesa maghala yanafunguliwa kuanzia mwezi wa kumi, korosho inaanza kuvunwa miezi ya nane, mwezi wa saba, wakati huo wote haya yote yanafanyika Serikali haijpeleka pesa. Sasa mtu anapoamua kujikimu kwa kutumia mali yake mwenyewe iliyoko ndani, anachukua korosho anapeleka kwa baba mwenye duka kijijini kwetu anakwenda kubadilishana na unga, anakwenda kubadilishana na sukari, anakwenda kuchukua pesa ili aweze kumtibu mtoto wake, leo Serikali hii sikivu inasimama hapa na kusema hawa watu ni wezi, tuwaombe radhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuwaombe radhi wachuuzi wa korosho kwa sababu wao sio wezi, kinachotakiwa kufanyika ni kurasimisha huu mfumo, na yatambulike kwenye mifumo huru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali inasema inakusanya korosho kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko, na wanakwenda kuziuza ni lini watakwenda huko chini? Sasa kwa nini tusirasimishe hawa kangomba wakakusanya korosho kidogo kidogo kutoka kwa watu wetu …

T A A R I F A

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja hapa kidogo kwenye suala hilo hilo kangomba, naomba niendelee kwamba tafsiri anayoitoa Mheshimiwa Mlinga ninamuomba kwa makusudi kabisa akae na wazee akiwemo Mzee Mkuchika na wengine wote wanaotokea upande huu, ukanda huu unaolima korosho halafu wamwambie kangomba kwa uhalisia ni nini, na si hicho anachokisema yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kama kangomba ni dhambi wasimame hapa watuambie, kwamba kufanya kangomba ni dhambi na kwamba hairuhusiwi. Vinginevyo kinachotokea ni kwamba Serikali inataka kwenda kufanya dhuluma kwa wafanyabiashara wadogo wadogo wa korosho; na ni kwa nini, korosho …

T A A R I F A

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru kaka yangu Mheshimiwa Zitto kwanza kwa kunikumbusha, na kuiomba Serikali ilete hoja Bungeni ya kurasimisha biashara hii na hawa watu wa katikati ambao wao watakwenda ku-bridge kati ya mkulima pamoja na mnunuzi mkubwa ambaye ni Serikali, kwa sababu wameamua wakafanye hiki kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nitoe tu angalizo kwenye hili jambo ….

WAZIRI WA KILIMO: Mheshimwia Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hapa sasa hivi Wakulima wanapewa adhabu…

T A A R I F A

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kujua tatizo la msingi linalozalisha kangomba Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sasa niiombe Wizara yake ikatoe leseni, ikarasimishe hizo biashara ili wawashauri hao watu walipe kodi, ndilo suluhisho la hili. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu elimu hii hamkuitoa wakati unaotakiwa muitoe niwaombe na Serikali hapa itoe tamko, korosho zote mlizozikusanya mzirudishe badala ya kuwadhulumu kwa sababu hamkwenda kuwaeleza kwamba wanatakiwa kuwa leseni. Kosa hili limeanzishwa na Serikali na mkiliacha litaendelea kujitokeza kwa sababu kangomba ni jina la kilugha la Kimakonde, Kiyao ni mchanganyiko, lakini kiingereza chake hawa watu ndio brokers. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mlichokifanya Serikali kwa kumwita yule INDO kampuni ambayo mnasema ni ya Kikenya inayomilikiwa na kijana wetu Mtembei ambaye ni muhaya wa Tanzania, anachokifanya yeye ni brokage kwa sababu Serikali imeshindwa kutafuta masoko ya korosho na yeye anakwenda kuziuza hizi korosho nchi za nje, jukumu ambalo lilikuwa lifanywe na Wizara ya Viwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo mmemruhusu kangomba INDO afanya hiyo kazi muwaruhusu na wale kangomba wengine, lakini kwa kuanzia hakikisheni kwanza korosho zao mlizokusanya mwaka huu mnazirudisha kwa sababu wao si wezi, there is no logic. Nimeona hapa kwene mtandao inasambaa Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Newala amekamata wafanyabiashara na wakulima, wa upande wa Mozambique kuja kuuzia Korosho zao Newala. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhambi gani walikuwa wanafanya kwenye uchumi wetu? Hivi mtu kutoa mali nje na kuzileta hapa ni dhambi? Watu wa kwetu sisi wa mipakani, mpaka wa Mozambique na Tanzania tunatenganishwa na mto Ruvuma, watu wa kwetu wanalima upande wa pili na watu wa huko Mozambique wanasoma upande wa huku, wanaita ng’ambo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna asiyejua hapa; Mkuchika na wengine…

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. CECIL D. MWAMBE: …babu zake walikuwa wanalima huko, wanakwenda kulima ng’ambo wanarudisha mazao yao pale.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila utaratibu)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Cecil kaa kidogo. Mheshimiwa Selasini, tulieni, Mheshimiwa Millya.

MHE. JAMES O. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti,...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Millya ni mwanasheria.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila utaratibu)

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti,...

MWENYEKITI: Mheshimiwa Millya.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila utaratibu)

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Zitto...

MWENYEKITI: Waheshimiwa.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila utaratibu)

T A A R I F A

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Zitto anatoka Kigoma, hamna korosho, lakini amechangia, sasa sijui hawa watu ambao …. national figure kutoka Kigoma.

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti,...

MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge,...

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachojaribu kusema ni kwamba...

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila utaratibu)

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Kubenea kaa chini.

MHE. JAMES K. MILLYA: Taarifa ninayotaka kumpa mzungumzaji…

MWENYEKITI: Kubenea kaa chini.

MHE. JAMES K. MILLYA: ..ni kwamba ….

MWENYEKITI: Waheshimiwa tutaanza kuandika majina.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila utaratibu)

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba mzungumzaji anatetea wauzaji wa Mozambique kuja kuuza korosho kwetu kwa sababu Serikali ya Magufuli imetoa bei nzuri, hao hao ndio wanasema haya makosa yaendelee. Wakati Serikali ya Magufuli inatoa bei nzuri kwa ajili ya wakulima wa korosho Lindi na Mtwara yeye anawatetea wa Msumbiji wakati Rais wetu anawatetea Watanzania, wewe ni mtu wa namna gani? (Makofi)

MBUNGE FULANI: Kweli kabisa.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila utaratibu)

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Cecil, hebu subiri kwanza.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila utaratibu)

MWENYEKITI: …subiri, kwanza, mimi si ndiye referee hapa? Mheshimiwa Anatropia, Mheshimiwa Magereli, hii ni mara ya mwisho mtatoa sauti zenu bila utaratibu humu ndani, niko very serious.

MBUNGE FULANI: Taarifa Mwenyekiti.

MWENYEKITI: …mjadala ni mzito kwa pande zote mbili. Ukitaka jambo lako Mbunge unasimama kwa mujibu wa Kanuni. Ukifikiri hapa ni kwenye viwanja vya michezo hapa sipo na tunaingia kwenye lala salama, nikikutoa hapa hutarudi mpaka mwaka ujao. Mheshimiwa Cecil! (Makofi/ Kicheko)

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Millya kwa kuliona tatizo linalofanywa na Serikali naipokea taarifa yake …. (Vicheko)

MBUNGE FULANI: Taarifa Mwenyekiti.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ni kwamba hata hiyo Serikali.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, huyo broker waliyompa kuuza hizo korosho ….

T A A R I F A

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mkuchika.

WAZIRI WA NCHI OFISI YA RAIS (MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Mwenyekiti, hili Bunge ni jengo linaloheshimika sana, ndiyo maana kabla hatujaanza kazi tunakula kiapo tutafanya kazi, tena tunamalizia Ee Mungu nisaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema uongo katika jengo kama hili, ni jambo la hatari. Mimi ni mkulima wa korosho, nina shamba la korosho. Neno kangomba ni neno la Kimakonde, mimi ni mzee wa Kimakonde, nimesimama hapa nieleze nini maana ya neno kangomba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kangomba ni ununuzi wa korosho kwa kutotumia kapani au kipimo kinachotambulika na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wabunge Wanaopinga Rushwa. Jumamosi iliyopita, acha hii ya jana, tulikuwa na semina pale Dodoma Hotel inayohusu weighs and measures; umuhimu wa vipimo katika biashara ya mazao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikao kile kililaani kangomba kwa sababu kangomba anasema tu kwamba bakuli hii ni shilingi saba, yule ambaye ana shida anayefanya biashara ya kangomba ni mtu ambaye ananunua korosho kwa mkulima, kwa kipimo ambacho si kidogo, ni kidogo ambacho anamnyonya ili baadae yeye aende apate faida kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sikutegemea mtu anayetoka eneo la korosho, anavyojua wapiga kura wake wanavyoichukia kangomba kule nyumbani, sikutegemea awepo hapa mtu anayetoka eneo la korosho anasema kangomba ni halali; kangomba is corruption, ndiyo maana Serikali inaipiga vita, na tutaendelea kuipiga vita... (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa wameshakuelewa, Mheshimiwa Cecil malizia dakika yako moja.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimwambie tu mzee wangu Mkuchika, namheshimu alisoma na baba yangu, kwamba…

MWENYEKITI: Changia suala ambalo liko kwenye mjadala.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, si najenga hoja.

MWENYEKITI: Haya endelea.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka nimweleze ni kwamba mpaka sasa hivi hiyo Wizara ya Kilimo, wana kesi ngapi Mahakamani za watu waliokwenda kulalamikia kangomba? Na anachokisema mzee si kwamba kangomba haifanyiki, ukimsikiliza kwa nyuma kwa nyuma anachosema irasimishwe ili wakae na mzani wakati wa kununua, ndicho anachokisema pale. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo na mimi nipokee taarifa yake na nimshukuru na ameliona hili wazo kwamba kinachofanyika watu wanakwenda kununua kwa vipimo visivyo sahihi. Kwa hiyo, ameshauri Serikali kwamba sasa hivi ipeleke mizani kwa wanunuzi wadogo wadogo vijijini ili waweze kuweka hili jambo likae sawa na ndicho kilio chetu, hicho ndicho kilio chetu. Sawa sawa na lile la Mheshimiwa Millya alikuwa analisema pale… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)