Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kupata muda wa kuchangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza sana Serikali, lakini pia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa aliyoifanya pale bandarini. Kwa kipindi cha miezi ya nyuma pale, Waheshimiwa Wabunge wengi walilalamika humu ndani kwamba bandari yetu sasa watu wameikimbia wameenda Beira na Mombasa, lakini kwa jitihada za Serikali tumeweza kufanya vizuri, sasa hivi bandari yetu ipo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, nataka kutoa ushauri kwa Mheshimiwa Waziri. Bandari yetu ya Dar es Salaam wateja wetu wakubwa ni watu wa Congo, Zambia, Malawi na nchi nyingine. Tayari watu wengi wameshaingia mikataba na wasafirishaji wa Tanzania, nasi Watanzania wengi tumechukua mikopo tukanunua magari na miundombinu mingine kwa ajili ya kupata hiyo mikataba ya kusafirisha hayo makontena kutoka bandarini na kwenda huko Congo na Zambia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utaratibu aliouweka Mheshimiwa Waziri, ni kwamba sasa tunaenda kuiua kabisa Bandari ya Dar es Salaam, totally inaenda kufa. Watu wengi wa Congo na Zambia watakimbia bandari yetu ya Dar es Salaam watahamia Beira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfanyabiashara anapoenda kununua bidhaa kule nje, kontena linabeba uzito wa tani 33 na tayari nao wameshafunga mikataba na viwanda kule nje. Sasa ukija ukibadilisha ghafla, maana yake ni lazima akukimbie kwa sababu hawezi. Pia walio na mikataba, tayari wameshasaini mikataba ya kubeba tani 33. Sasa naona Serikali imeenda kusaini mkataba na nchi za East Africa kama Kenya, Burundi na Uganda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania hatuna biashara ya transport ya moja kwa moja na Kenya. Kenya ndiyo mshindani wetu mkubwa kwenye bandari. Kwa hiyo, kilichoingiwa hapa ni kutaka kututoa kwenye mood halafu watu watarudi Mombasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu Wakenya wao wana sheria hiyo ya magari yenye tairi mbili toka zamani, lakini sisi tunakopeleka kama Zambia na Malawi, wao wanatumia super single. Sasa Serikali inapokuja leo kusema tu ghafla tubadilishe kutoka kwenye super single twende kwenye tairi mbili, haiwezekani, utaua watu na pressure. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana, jitihada ambazo zimefanywa na Mheshimiwa Rais kuifufua bandari yetu ya Dar es Salaam, ni vizuri wataalam, tunaamini mmesoma vizuri, lakini hebu jaribuni kufikiri nje ya box, maana pengine hizi degree za makaratasi zinatusumbua, mtaua watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana wajaribu kukaa na wadau ambao wameweza kumiliki hivi vyombo watusikilize. Naamini wasafirishaji wengi, ukitafuta Tanzania nzima wenye degree nyingi, wengi ni Darasa la Saba. Sasa kwa style mnayoenda hii, hamjatusikiliza, wala hamjapata experience. Kwa hiyo, ni vizuri mkapata muda wa kuwasikiliza. Hizi sheria hamtungii magari, mnamaliza kutunga sheria, inaanza kutula sisi wenyewe na wengine wamo humu ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, ni vizuri tukaacha kubeza jitihada za Rais, hizi sheria ngumu ambazo zinaenda kuua bandari yetu, ni vizuri tukaziangalia upya na ikiwezekana tuziache, hazitusaidii katika Serikali inayotaka kukua kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ni-declare interest, mimi nafanya biashara ya mabasi, nazungumza kwa ajili ya watu wenye mabasi. Biashara ya mabasi ni kubwa sana na unaweza ukaona mtu anamiliki mabasi 30, lakini hakuna mtu anayenunua basi kwa cash, wote wanakopa. Hata hizo installments tu za shilingi milioni tano kuzipata kwa mwezi ni shughuli kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria zilizowekwa, mtu anafanya kosa moja, anapigwa faini ya shilingi milioni tano. Tafsiri yake sasa ninyi mnataka kumchonganisha Mheshimiwa Rais na wasafirishaji. Haiwezekani mtu kama alikuwa anapigwa faini ya shilingi 30,000/= na shilingi 250,000/=, ika- shoot kutoka hapo kwenda kwenye shilingi milioni tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri apate muda, aache kupuuza mawazo ya wadau, aanze upya kuzungumza na wadau wamweleze kero zao na awasikilize. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo la mabasi. Nampongeza Mheshimiwa Kangi alivyoanza alisema sasa mabasi yasafiri usiku wote. Unajua ni kitu cha kushangaza! Ukienda kwenye nchi tunazopakana nazo, watu wanasafiri usiku; na dunia hii imebadilika; na nchi hii inaenda kubadilika kuwa nchi ya viwanda. Sasa unataka watu walale. Najiuliza, ni kitu gani ambacho kinashinda Serikali kutengeneza utaratibu wa kuruhusu magari yasafiri usiku?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli hiyo ndiyo sheria kwamba mabasi yataleta matatizo? Mbona treni inasafiri usiku? Ina maana hata tukianza kutumia treni ya Stiegler’s Gorge hiyo, itasafiri mwisho saa saba? Si lazima ifanye kazi usiku na mchana? Watu wanataka kufanya kazi Dar es Salaam walale Morogoro au Dodoma halafu saa kumi waondoke kurudi Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba, kama tatizo ni usalama, afadhali kama Jeshi letu limepungukiwa Askari, tuchukue hata JKT wapewe semina wakae barabarani, gari zisafiri usiku na watu wawe na uhuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda nchi nyingine tunaona. Sisi tunasafirisha kwenye nchi za East Africa, wenzetu wamefanyaje? Mabasi hayaingii mizani. Mabasi kuyaingiza mzani ni ku-create tu rushwa, hakuna basi inayozidi zaidi ya shilingi 30,000/=, shilingi 15,000/=. Kwa nini, Serikali isione umuhimu wa kuondoa hii sheria ya mabasi kupita kwenye mizani? Kwanza mnaleta usumbufu kwa abiria, mnasababisha watu wanachelewa kwenye kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri Serikali ikaangalia vitu ambavyo vimetukwamisha tuviondoe, twende kwenye Serikali ya kuvutia na watu wengine waje kufanya kazi hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naona huko kwenye usafirishaji, pia Idara yake katika Wizara ya Miundombinu, sasa hivi ukienda Dar es Salaam wameondoa Hiace kule mjini, hata ukija Dodoma leseni ya Hiace ikiisha hawataki, ukienda Mwanza hawataki. Mimi najiuliza; na nilifanya research ndogo tu. Ukienda kule Dar es Salaam, pamoja na kuziondoa zile gari (Hiace) kule ndani, lakini watu wanasimama kwenye daladala, wanatoka safari wanasimama, gari zinabeba watu mpaka 110, lakini watu wanapanda bodaboda na bajaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti iliyofanyika ya kuziondoa Hiace mimi sioni kama ni halali. Sana sana ni kwamba tumewaonea wale wafanyabiashara. Ukiondoa Hiace ina matairi manne, mbona sisi gari zetu za Mawaziri zinaruhusiwa kupita kule? Kama ni hivyo na hizo gari ziondoke.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye nchi nyingine zilioendelea, magari yana umbali wake ya kuwekwa; yape magari ya binafsi, wote tuning’inie kwenye daladala moja ndio mwone huo uchungu wa kuziondoa hizo gari huko ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naishauri Serikali, pale ambapo tunakuwa hatuna umuhimu wa kushikiria sheria ambazo zimepitwa na wakati, leteni amendment humu tuziondoe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze kidogo kwenye ndege. Kwa bahati nzuri mimi ni captain. Unajua nikisema mimi ni Darasa la Saba watu hawaelewi! Mimi ni mtaalam wa kurusha helicopter. Kwa hiyo, lazima niwaambie kidogo hapa. Pamoja na huo ungo pia naweza kurusha. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilimsikiliza dada yangu, Mheshimiwa Ester Bulaya hapa, alilalamika kwamba marubani wetu wa Tanzania wanabadilishwa tu kutoka bombadier kwenda airbus kwenda dreamliner, jamani hili sio basi, ndege ni kitu kikubwa sana. Captain wa ndege hawezi kuruhusiwa kutoka kwenye ndege moja kwenda kwenye ndege nyingine bila kupewa training na kupewa leseni ya kuendesha ile ndege. Hata kwanza wale airbus wasingewaruhusu kuwapa ndege rubani wa bombadier akaendeshe ndege ya airbus au dreamliner. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ndiyo mabadiliko ambayo pia na wenzetu wanatakiwa wayakubali, kwamba zamani tulizoea kuona marubani wazuri ni Wazungu, sasa hivi vijana wetu wamesoma vizuri, tunawapongeza. Kwa hiyo muwe na imani kwamba hawa watu wamepita kwenye training na wana leseni za kuweza kuendesha hiyo ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia limezungumzwa suala la faida; ndege huwezi ukaona faida leo. Sisi tunafanya usafirishaji, ukitaka kujua faida ya ndege, asimame Mchumi hapa aniambie, kama hutaona kuingiza kwenye hela uniambie wale ile ndege iliyowabeba, wale waliowahi Dar es Salaam wamepata faida gani na kule walikoenda kununua. Kwa hiyo ina components nyingi, lazima tuvumiliane tu, mtakuja kupata utaalam zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)