Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli kama makelele yangekuwa yanashinda kesi basi upande wa Upinzani wangeshinda sana, lakini ndiyo wamepoteza kesi zote ambazo walishtaki kwa sababu ya kushindwa kura, licha ya makelele yote ambayo wanafanya humu ndani, mahakamani hatushindi kura kwa kupiga makelele. Pia niungane na mwenzangu Mheshimiwa Tundu Lissu, aliposema asubuhi kwamba tunaposema sisi sikilizeni msiumie, tuseme mtusikilize.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu hawa hawajielewi kwa nini hawapewi Serikali, hawapewi Serikali kwa sababu wananchi hawawaamini, hawa ni ving‘ang‘anizi hawa kwenye madaraka. Tawi lao la CUF la UKAWA la CUF, Kiongozi wake ana miaka 20 anagombea yeye peke yake, vilevile hawajielewi wenzetu hawa kwa nini hawapewi madaraka.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema tukiumia tuvumiliane, neno la ufisadi lilikuwa ndiyo ajenda ya Upinzani kwa mwaka mzima mmetangaza ufisadi kwamba haufai. Imetokea nini?
Mimi nina orodha ya mafisadi ambayo mliitangaza ninyi UKAWA, lakini shemeji yangu huko umemchukua namba moja fisadi unaye wewe huko na jambo hili linafanya wananchi wasiwaamini. Mnawafanya watu waamini kwamba ninyi ni vinyonga, mnabadilika badilika, hatutaki sera ya namna hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uchaguzi wa Zanzibar. Hakuna mtu aliyewakataza kushiriki uchaguzi uliorudiwa na hasa tawi lenu hilo la CUF, siyo kosa la Chama cha Mapinduzi kushinda kura zote kwa sababu ninyi mlitia mpira kwapani.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, hawa UKAWA wanajua siri kwa nini hawakushiriki uchaguzi mbona hamuendi mahakamani? Mbona hamsemi kwa nini hamkushiriki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Mapinduzi ya Zanzibar ni kweli kwamba Tanzania Bara ilishiriki na kusaidia mapinduzi kwa nguvu yote na sababu kubwa tulijua kwamba mapinduzi yale ni haki, yanaleta uhuru kwa Wanzanzibar. Wale ambao wanapinga Mapinduzi sasa ni mikia au vitukuu vya wale watawala waliotawala Zanzibar. Najua inawauma sana na itawauma sana, lakini tunaendelea kusema Mapinduzi daima. (Makofi)
Mheshimwa Naibu Spika, nirejee katika hoja iliyopo mbele yetu ya Katiba na Sheria na kwanza nianze kwa ku-declare interest kwamba mwaka 2014 Shirika la Kazi Duniani liliipa fursa Tanzania kuwa Kiongozi wa Vyama vya Waajiri Afrika na huyo Mtanzania ni mimi Mbunge mwenzenu. Vilevile mimi ni Mwenyekiti wa Chama cha Waajiri hapa Tanzania na mwishoni Serikali ya Jamhuri ya Muungano inafanya kazi vizuri katika kujenga barabara na kujenga majumba mazuri kama hili tulilomo ndani kwa kutumia wakandarasi. Naomba ni-declare interest kwamba mimi ni mkandarasi daraja la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo naomba nirejee kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais alipohutubia humu ndani, kwamba kulikuwa na sheria anazozifahamu yeye na wanasheria wote wanazifahamu ni mbaya kwa Watanzania na angependa sheria zifanyiwe marekebisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na Sheria ya Manunuzi ya Umma. Sheria hii ina kasoro haitoi upendeleo kwa wazawa wale wanunuzi wanapofanya manunuzi kwa mali na kazi inayopatikana pia kwa Watanzania. Ninashauri Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie lini sheria hii italetwa hapa kwa marekebisho ili iweze kutoa fursa kwa Watanzania. Vilevile inatoa uhuru mkubwa kwa wanunuzi kuchagua mzabuni wanayemtaka na hiyo inasababisha mirejesho ya rushwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini ina mapungufu pia na ningependa Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria anapokuja kuleta majumuisho yake hapa atuambie lini Serikali italeta sheria hiyo hapa kurekebisha mambo yafuatayo; moja ni likizo ya uzazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la likizo ya uzazi limekuwa kero kubwa kwa waajiri. Waajiri wanapata taabu sana kuwahudumia akina mama wanaorudi baada ya kujifungua, kuna watu wanaenda kunyonyesha kwa muda wa masaa mawili, kwa mwaka mmoja, miaka mitatu mpaka miaka mitano, sheria haisemi mpaka wa muda wa kunyonyesha.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile sheria hii inaleta machungu makubwa wakati wa kuachana na wafanyakazi wabaya, wafanyakazi wakikaribia kutimiza muda wa kustaafu wanafanya makosa makusudi, aidha wanaiba na ukiwapeleka mahakamani kesi ikianzishwa mahakamani mwajiri hawezi kumfukuza huyu mfanyakazi na kesi itaendelea na kama alikuwa anapata marupurupu ya nyumba, gari na wafanyakazi nyumbani ataendelea kulipwa na mnavyojua sheria humu ndani na mahakama inachukua muda mrefu, mwajiri ataendelea kumlipa mfanyakazi huyu hata kama kesi itachukua miaka kumi. Tunaomba Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria utakapokuja ujaribu kutusaidia suala hili pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia lipo suala lingine ambalo ni sekta ya ulinzi binafsi, sekta hii haina sheria huu mwaka wa 36 tangu ianzishe hapa na matokeo yake sekta hii inajiendesha hovyo hovyo tu, na kuleta matatizo kwa watu ambao wanaendesha biashara hii. Sheria hii ikitungwa italeta udhibiti wa sekta ya ulinzi binafsi na kuwafanya watu hawa waweze kufanya kazi kama ambavyo Serikali itataka na kwa manufaa ya Watanzania. Watu wengi wameumizwa na makampuni ya ulinzi binafsi lakini hakuna sehemu ya kuyashitaki, napendekeza atakapokuja Mheshimiwa Waziri aje na majibu kwa nini asilete Bungeni humu Muswada wa kuanzisha sekta ya ulinzi binafsi, Sheria ya Ulinzi Binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, anisaidie pia kule kwetu Upuge iko Mahakama ya Msingi ambayo ni nzuri ina majengo yote, mahakama yenyewe lakini na majengo ya kukaa wafanyakazi imetelekezwa huu mwaka wa 12, majengo yale sasa wanakaa panya, wanakaa wanyama hovyo. Ningependa pia anieleze itakuwaje kuhusu majengo yale yaliyopo kule.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishie hapo na naunga mkono hoja. Ahsante sana.