Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

Hon. CAN.RTD Ali Khamis Masoud

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mfenesini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa kunipa nafasi kwa dakika hizi chache niweze kuchangia machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuwa na safari ya maendeleo au yako binafsi na ukajiwekea malengo, ukichelewa kufika kwenye malengo uliyokusudia hutakiwi kwa mtu mwenye busara kutoa lawama, kutoa ukali au kukaripia watu. Mtu mwenye busara atakaa kitako kufikiria kitu gani kilimkwamisha asifikie yale malengo aliyojipangia na baadaye kutatua ili safari yake atakapoianza tena aweze kufika alikokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano, imejikita kabisa katika kuleta maendeleo ya viwanda ili kwenda sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa, lakini safari hii kila taasisi imekabidhiwa jukumu lake. Kidogo nitaizungumzia SIDO ambayo kwa hakika nimeiona kwa macho yangu na kuwasikia watendaji wa sehemu hii wakizungumza mashaka na matatizo yanayowakumba. SIDO imepewa majukumu ya kukuza wajasiriamali, kutoa elimu, kutoa ushauri na mambo mengine kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu yote waliyopewa, jukumu kubwa ni elimu inayotakiwa iwafikie wajasiriamali ili waweze kuzalisha kwa tija. Uwezo walionao SIDO hivi sasa hauwezi kabisa ukafanikisha malengo haya waliyopewa, hivyo niiombe sana Serikali katika jambo hili wawaangalie wenzetu wa SIDO kuwawezesha kwanza wapate nyenzo zitakazowasaidia lakini pia fedha ya kutosha itakayowafikisha walipokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la viwanda vilivyobinafsishwa, limezungumzwa sana hapa na sisi katika kamati tumelizungumza sana hili. Nafikiri bado hatujawa serious katika hili, wapo watu wamepewa viwanda na hiki ni kipindi kirefu karibu miaka ishirini na, wamepewa mikataba hawajaitekeleza bado tunawaangalia tu, niiombe Serikali muda umefika sasa waliopewa viwanda wakavichukulia mikopo, waliopewa viwanda wakauza mashine sasa ni wakati wao wa kuanza kushughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo tumelijadili kidogo katika Kamati ni mkakati wa Serikali wa kuhakikisha sasa mafuta ya kula yanazalishwa nchini. Mikakati hi tumeiona kwa maandishi na ina lengo zuri, lakini mote nilimosoma, labda sikusoma vizuri, lakini mote nilimosoma sikuuona mkakati wowote ule ambao unazungumzia wazalishaji wa alizeti hapa nchini. Mkakati unazungumzia viwanda lakini haujalenga malengo gani yatafanywa, kipi kitafanywa, watasaidiwa nini wazalishaji ili zao hili lilimwe kwa wingi na viwanda vyetu vipate malighafi ya kutosha itakayowawezesha sasa kufikia lengo tulilolikusudia la Taifa la kuchakata mafuta hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nimekusudia kulizungumza kidogo, ni wafanyabiashara wa viwanda wanaosafirisha bidhaa zao hapa nchini kutoka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani. Nichukue nafasi hii kwanza kuwashukuru wenzetu wa TFDA kwa mashirikiano mazuri wanayoyafanya kati yao na wenzao wa ZFDA. Bado nataka kuzungumzia tatizo linalojitokeza hasa kwa kiwanda chetu kimoja kule Zanzibar ambacho kinafungasha kahawa, chai, sukari kwa ajili ya Mashirika ya Ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanaposafirisha mizigo kuja nayo Tanzania Bara wanapofika bandarini, custom wanasema hiyo ZFDA hawaifahamu, lakini mashirikiano kati ya ZFDA na TFDA, ni mazuri. Wanachofanyiwa hawa sasa wanatakiwa baada ya kufika na bidhaa bandarini waende TFDA wakachukue barua ya kuwatambua, wakishachukua barua wapeleke bandarini, baada ya kutoka bandarini ndio wanakwenda kufanya shughuli nyingine za kuhakikisha mzigo ule unafikishwa unakokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa la kushangaza zaidi watu hao hao kiwanda hicho hicho bidhaa hiyo hiyo, watakapopeleka tena mara ya pili wanatakiwa tena waende TFDA wakachukue barua ya uhakiki wa kuhakikisha kwamba hii ZFDA inatambuliwa. Niiombe sana Serikali katika jambo hili tuondoshe vikwazo hivi ili wenzetu wanaosafirisha bidhaa kutoka Tanzania Visiwani wanapozileta Tanzania Bara kusiwe na vikwazo vya kuwasumbua. (Makofi)