Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Selemani Said Bungara

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Kilwa Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. SULEMANI S. BUNGARA: Mheshimiwa Spika, dakika tano ni kidogo sana. Kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi hii, nitaongelea mambo mawili tu kuhusu uvuvi na kilimo.

Mheshimwa Spika, Wilaya ya Kilwa ni wavuvi wakubwa wa daga, hususan dagaa mchele na dagaa lumbunga. Kwa kipindi kifupi tumepata mtafaruku mkubwa tulipoingiliwa na operesheni, ikiongozwa na Wanajeshi na kuambiwa kwamba uvuvi tunaotumia ni uvuvi haramu na nyavu tunazotumia ni nyavu ambazo hazitakiwi kuvulia.

Mheshimiwa Spika, wavuvi hao walikuwa na leseni na nyavu zao zilikuwa zinakaguliwa tangu mwaka 2009 mpaka leo. Cha kusikitisha sana nyavu hizo zimeambiwa zisivue. Katika ukurasa wa 37 wa kitabu hiki, wanasema unaweza kumtambua mvuvi anayeshughulika na uvuvi haramu ikiwa mvuvi huyo atatekeleza shughuli zake za uvuvi bila kuwa na leseni. Kwa hiyo, mvuvi haramu ni yule ambaye anavua bila kuwa na leseni lakini wavuvi wetu waliokamatwa waliokuwa na leseni wanaambiwa wavuvi haramu.

Mheshimiwa Spika, naomba jambo hili liangaliwe upya na wale wavuvi waruhusiwe kuvua na nyavu zile kwa sababu leseni wanazo na nyavu zao zilikaguliwa. Hata kama sheria zinasema zile nyavu ni haramu, lakini wananchi walinunua zile nyavu wakapewa leseni. Siyo chini ya wavuvi 3,000 katika Wilaya yangu ya Kilwa wameambia wasivue kuanzia sasa wakati leseni wanazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kwamba pengine zile nyavu ni haramu, lakini leseni wanazo na waliotoa ni Serikali. Naiomba Serikali itumie hekima ili wale wavuvi waendelee kuvua kwa nyavu zile mpaka hiyo sheria itakaporekebishwa. Kwa sababu sisi wengine Waislamu tunasema, nguruwe haramu lakini dharura ikitokea ni halali kula kidogo ili mambo yaendelee. (Kicheko/Makofi)

Mheshimwa Spika, naomba Serikali sikivu ya …

SPIKA: Mheshimiwa Bungara aya ya ngapi hiyo?

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Aya ya 150 Surat Maida. (Kicheko/Makofi)

Mheshimwa Spika, kwa hiyo, kwa heshima na taadhima, kwa kuwa Serikali hii sikivu na wale wananchi wavuvi watakuwa hawana kazi, hali zao za kimaisha zitakuwa mbaya, nakuomba Mheshimiwa Mpina uongee na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa wanyonge na hakuna wanyonge nchi hii kama wavuvi, waruhusiwe kuvua ili waende na maisha yao. Hilo moja. (Kicheko/Makofi)

Mheshimwa Spika, pili, nguruwe haramu lakini katika dharura unakula. Basi na nyavu hizo haramu lakini wapewe wavue.

Mheshimiwa Spika, nakuja katika korosho. Sisi tunaishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiongozwa na Mheshimiwa Magufuli kwa kutuambia mtanunua korosho kwa shilingi 3,300; wakulima waliandamana wakafurahi, lakini kilichotokea hali ni mbaya sana. Mpaka leo wakulima bado hawajalipwa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Dakika zako zimeisha Mheshimiwa.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Allah!! (Kicheko)

SPIKA: Zimeisha kaka.

MHE. SELEMANI S. BUNGARA: Namalizia tu. Ninachoomba watu wa Kangomba nao walipwe kwa sababu na wao walipeleka korosho AMCOS zikapokelewa na Serikali wanazo. Kwa kuwa wanazo korosho, za Kangomba walipwe, ndio hoja. Kwa sababu muda wangu umeisha, nilitaka nifafanuliwe sana hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)