Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Napenda kutumia nafasi hii, kipekee kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kauli yake ya kusaidia wananchi wanaoishi katika maeneo ya hifadhi kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu wewe ni mzoefu katika nchi hii, Bunge hili limejadili mara nyingi operesheni mbalimbali zilizofanyika katika hifadhi ambazo ziliwaumiza wafugaji wa nchi hii kwa kiwango kikubwa sana, ni mtu tu asiye na akili timamu atakayeacha kumpongeza Mheshimiwa Rais Magufuli kwa jambo hili jema na la kiutu alilofanya katika kusaidia wafugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wako watu ambao hawataki kuona jema analofanya Mheshimiwa Rais katika kipindi hiki cha miaka mitatu, lakini hao hao ndio wanaoomba viwanja vya ndege katika maeneo yao viboreshwe lakini wakati huo huo wakipinga uagizaji wa ndege katika nchi yetu. Hao hao ndiyo wanaosema tupunguze deni la Taifa lakini wanachukua Rais akinunua ndege kwa cash ya fedha ya walipa Kodi wa Watanzania hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipindi hiki cha Mheshimiwa Rais Magufuli cha miaka mitatu tumeshuhudia vituo 360 vya Afya vikijengwa katika nchi hii, ambayo ni historia, haijawahi kuitokea. Ndiyo maana wengine tunasema lazima tupongeze na kutambua kazi kubwa ambayo Rais huyu amefanya, katika muda mfupi ambao amekuwa katika madaraka haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazo Hospitali 60 zinajengwa kwenye nchi hii, nani ambaye haioni katika utawala huu wa Rais Magufuli. Nataka tuyaseme haya kwa sababu Watanzania wengi wanatambua na wako wengi wanaopambana kufifisha ndoto ya Rais, lakini nataka tumtie moyo kwamba hata wakati ule Yesu alivyokuwa amepingana na matendo yake, akawaambia hata kama hamniamini aminini kazi ninazozifanya. Kwa kazi hizi ambazo Rais anafanya tunazitambua na kumpongeza na kumtia moyo, asonge mbele Watanzania wako nyuma yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili la kumpongeza Rais, kwa dhati kabisa, naomba niipongeze Wizara ya Mifugo kwa mara ya kwanza wamesimama na wafugaji wa nchi hii na kutambua kwamba na sisi ni Watanzania walio huru katika Taifa hili na kutetea maslahi ya Wafugaji. Pamoja na changamoto zingine lakini katika hili tuko pamoja na Mheshimiwa Waziri, asonge mbele, tutamsaidia katika kusimamia Wizara ya Mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukijiuliza maswali mengi kwa nini katika nchi hii, hatujawahi kuona oparesheni ya wakulima katika maeneo ya hifadhi isipokuwa operesheni ya wafugaji. Ni kwa sababu wafugaji mara nyingi wana cash mkononi kwa sababu wana ng’ombe, kwa hiyo viashiria vinafanyika wakati mwingine sio halali, ni operesheni za kutafuta rushwa na kunyang’anya wafugaji wetu mali zao. Katika hili ndio maana nasema tunampongeza Rais na Wizara kwamba angalau sasa ile mianya ambayo watu wachache waliitumia kuwaumiza wafugaji imefungwa na ndio maana wengine wanapiga kelele, lakini sisi tuko nyuma ya Rais kwa kazi kubwa ambayo ameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niseme mambo machache, nataka niombe Serikali watusaidie, wanazuia wafugaji wetu wasipeleke ng’ombe Kenya wanafanya operesheni ambayo sio halisia katika mipaka ya nchi yetu, lakini nataka niwauze Wizara ya Mifugo, Viwanda vyetu 82 vya maziwa nyakati za Nyerere mpaka kipindi cha Mwinyi kidogo, viko wapi? Viwanda vya nyama vilivyokuwa vinafanya kazi katika nchi hii, viko wapi? Kama ndani ya nchi yetu hakuna soko la uhakika kwa nini watuzuie sisi kwenda kutafuta soko huko linakopatikana na kama wanafikiri kuweka kodi kubwa kwa mifugo ni kuzuia mifugo isiende nje ya nchi, tunataka Wizara watuambie masoko ya kupeleka bidhaa yetu yako wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni aibu, ni aibu kwenye Taifa linalozalisha ng’ombe nchi ya tatu Afrika, mali zetu za ng’ombe zinaenda nje bila kuongezwa thamani, tunapeleka kwato, maziwa, ngozi na nyama, halafu tunasema ipo Wizara inayojali mifugo, tunataka Serikali ituambie iko wapi mikakati ya Wizara ya kuhakikisha rasilimali hii ya Taifa ambayo ni neema kwa nchi yetu, inabaki kwa maslahi mapana ya Taifa letu na kuongeza pato la Taifa. Ni aibu kwa nchi ambayo ni ya tatu kwamba pato la Taifa halilingani na mifugo tuliyonayo na wakati mwingine tunasema mifugo yetu inaharibu mazingira, tunataka Serikali itupe mikakati ambayo Waziri wa Viwanda jana alituambia, kwamba wamepanga kuhakikisha kwamba tunachakata mazao ya mifugo, tunataka frame time, ni lini viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo kwenye nchi vitasimamiwa na kuonekana kwamba vinakidhi matakwa ya wafugaji wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka Serikali kwa kweli katika hili ituambie, tunaridhika na pato la Taifa linalochangiwa na mifugo yetu, tunaridhika na upekaji wa ng’ombe zetu Kenya bila kuongeza thamani. Hivi Wakenya wanatuzidi nini? Tunaridhika na uamuzi wa Afrika Mashariki wa kuweka vikwazo vya ngozi na nchi kama Rwanda na Burundi ambayo hawazalishi ng’ombe lakini wanatuletea ngozi, wakati tulikuwa tukizalisha ngozi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ipo Mikataba tunaingia na nchi, lakini kwa kweli haina manufaa kwa nchi yetu, nchi zile zingine hazizalishi ng’ombe, hazina ng’ombe, lakini wanaamua, wao ukipeleka ngozi Uganda, Rwanda inaenda kama reject kwa hiyo, sisi tunakosa mapato na ngozi zetu zinakuwa useless. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ituambie kuwepo kwa Wizara hii, ni kutafsiri ndoto ya Rais ya Tanzania ya viwanda ambayo kila mwananchi ataona umuhimu wa kuwepo kwenye Taifa lake na umuhimu wa kuwa na rasilimali katika nchi yetu. Haiwezekani tukasema tuna viwanda kadhaa, lakini kama viwanda hivyo havibadilishi maisha na uchumi wa nchi yetu viwanda hivyo havitakuwa na maana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naomba kabisa, wakati Waziri wa Mifugo anakuja kuchangia baadaye atusaidie ni kwa namna gani nchi yetu inaondokana na hili tatizo la kupeleka rasilimali na bidhaa ambayo haijachakatwa katika nchi zingine za wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, tunalo tatizo pale Namanga, mfugaji akitaka kuvusha ng’ombe zake kwenda Kenya analipa si chini ya elfu 70 kwa kichwa cha ng’ombe, ipo Sh.30,000 wanaita ni fedha za ushuru wa Wizara, lakini ipo Sh.2,500 ya movement permit na kodi zingine za Halmashauri, hivi kwa nini ng’ombe peke yake tuyaangalie na mazao mengine tunayozalisha, wanakuwa na kodi kubwa kuliko mazao mengine yoyote kwenye nchi yetu? Tunaomba Waziri atuambie wakati wa bajeti hii ni kwa namna gani Serikali itapunguza kodi ambazo zimewekwa kwenye mifugo ya nchi yetu kwa sababu kuzuia tu isiende nje kwa kuweka kodi kubwa wakati huku ndani hakuna viwanda vya kuchakata, ni uonevu kwa wafugaji. Kwa hiyo naomba kwa kweli, kodi hizi zipunguzwe kwa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Spika, suala la ardhi, ni kweli tumesikia ushauri wa Kamati, lakini nami nampongeza Rais na nimpongeze Waziri wa Ardhi kwa dhati ya moyo wangu kabisa. Moja ya Wizara zinazofanya kazi na zinafanya vizuri katika nchi yetu, ni Wizara ya Ardhi na faida yake ni kwamba, wamekataa rushwa, sio kwamba hakukuwahi kuwepo Wizara katika nchi hii, lakini Wizara hii ina mchakato mkubwa sana wa rushwa. Sisi tunaamini hawa wamekataa rushwa ndio maana migogoro ya ardhi imepungua katika nchi yetu. Kwa hiyo tunawatia moyo, msikate tamaa, tunahitaji ardhi yetu kwa sababu imekaa muda mrefu haitumiki na sisi tunaihitaji.

Mheshimiwa Spika, tunajua wako wachache watakaotumiwa na watu wenye ardhi hiyo, lakini sisi tuko tayari kuungana na nguvu na shughuli za Wizara katika kurejesha rasilimali ardhi kwa nchi yetu na kwa Watanzania wanyonge ili waweze kutumia katika kuzalisha. Haiwezekani tukawa na ardhi lakini Watanzania walioko maeneo hayo hawana uhalali wa kutumia ardhi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeenda Misenyi wakati wa Kamati, ardhi kubwa iliyoko kule, Watanzania wamenyimwa kutumia, lakini Waganda wanaingiza mifugo, wanatoa jioni lakini ukienda Tanzania wanakwambia ni hifadhi. Hii si sawa, lazima ardhi yetu itumike kwa maslahi ya Watanzania ambayo Mungu ametupa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara songeni mbele, lakini tunaomba mtuletee modality ya mchakato mzima wa kutatua migogoro ya ardhi katika nchi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.