Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba kuchangia hizi Kamati mbili, lakini nitajikita zaidi kwenye Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji. Naomba nianze kwa kusema kwamba Sekta ya Kilimo imeajiri zaidi Watanzania kwa asilimia 70, lakini pia inachangia zaidi ya asilimia 30 ya GDP, lakini sekta hii pia inachangia chakula kwa nchi yetu kwa zaidi ya asilimia 100, lakini pia Sekta ya Kilimo inatoa malighafi za viwandani kwa zaidi ya asilimia 65.

Mheshimiwa Spika, pamoja na umuhimu wa Sekta ya Kilimo lakini imesahauliwa na Serikali hii ya Awamu ya Tano, leo hakuna masoko ya mazao ya wakulima. Leo Serikali inakwenda kununua kwa mfano, korosho. Badala ya kutafuta masoko ya mazao, kama masoko ya korosho, mahindi, pamba, mbaazi, tumbaku na kahawa, leo Serikali inakwenda kununua mazao. Haitaweza kununua mazao yote kwa sababu nchi hii tuna mazao mengi sana ambayo kwa kweli bei yake iko chini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba mimi naishauri Serikali ijikite kutafuta masoko ya mazao. Huu ndiyo utakuwa mwarobaini kuliko kwenda kununua mazao, haitaweza, zoezi hili ni gumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunafahamu kwamba mahindi tuna miaka miwili sasa hali siyo nzuri, bei iko chini; tumbaku iko kwenye maghala kwa mura mrefu hainunuliwi; mbazi kutoka kilo shilingi 2,000/= tunafahamu kwamba shilingi 80/= hadi shilingi 100/= hali ni mbaya. Leo wakulima nchi nzima wanalia. Kwa hiyo, Serikali imejikita zaidi kwenda kutafuta masoko ya mazao kuliko kwenda kununua mazao kwa sababu haitaweza.

T A A R I F A

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ngoja nimwache nisimjibu, kwa sababu wakati mwingine unaacha wafu wazikane wao wenyewe. Kwa hiyo, naomba nisimjibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimekuja kuzungumzia maslahi ya Watanzania. Leo ninavyozungumza nawe kwa mfano kwenye zao la kahawa, nami nilileta hoja binafsi japokuwa haikupata kibali cha kuingia Bungeni, lakini nilileta hoja binafsi ya kuhusu zao la kahawa. Kinachoendelea kwenye kahawa, hali ni mbaya kuliko kawaida.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba kuna watu wengine hawafahamu misemo na methali na kadhalika. Kwa hiyo, naomba niendelee. Labda ni vizuri tu kwa sababu nafahamu yeye alikuwa ni Mtangazaji, nadhani vitu hivyo anavifahamu vizuri sana. Haitakiwi tupoteze muda mwingi sana kwenye hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kungumza hivyo, naomba niendelee sasa kwa ruhusa yako.

SPIKA: Tuvumilie.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Naomba niendelee kwa sababu alikuwa wanatupiga, sisi hatuwapigi, tumeamua kuwasemehe.

SPIKA: Endelea, ila kuna neno moja umesema ulileta hoja binafsi.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Halafu ikakataliwa. Nikuhakikishie mezani kwangu sijawahi kuona hoja binafsi kutoka kwako.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, nita…

SPIKA: Endelea tu kuchangia, lakini sijawahi kuiona.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Ahsante. Nikimaliza nitakuletea zile nakala ambazo nilikuwa najibiwa kutoka kwenye Ofisi ya Katibu wa Bunge. Nitakuletea Ofisini kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo kwa mfano kwenye zao la kahawa, Serikali imeamua kuyakataza Makampuni yaliyokuwa yananunua kahawa yote, yamezuliwa, badala ya kuruhusu soko huria; kwa sababu tunaamini kwamba soko huria ndilo ambalo linaleta bei nzuri kwa wakulima. Tungeruhusu Makampuni yanunue, yashindane na hivyo Vyama vya Msingi vya Ushirika vilivyoanzishwa ili mwisho wa siku mkulima aweze kunufaika na bei nzuri ya kahawa.

Mheshimiwa Spika, kabla hatujawa na AMCOS (Vyama vya Msingi vya Ushirika) bei ya kahawa mwaka 2017 tuliuza shilingi 4,000/= na kitu, hadi shilingi 5,000/= kwa kilo moja, lakini baada ya kuanzisha, tumeuza kilo moja ya kahawa hadi shilingi 1,800/=. Kwa hiyo, nashauri, ni vizuri Serikali ikaruhusu soko huria kwenye zao la kahawa na wakati mwingine kwa sababu pembejeo ziko juu, mkulima analima kwa jasho sana, anapouza ndipo Serikali inapojitokeza inasema usipeleke kahawa yako Uganda, sijui usipeleke wapi. Nchi hii kuna matatizo makubwa sana ya kilimo. Naiomba Serikali kwa sababu tayari ndiyo inayoongoza, ijitahidi kutatua matatizo ya Watanzania. Kama haiwezi, basi iwaachie wengine ambao wako tayari kuongoza nchi hii. (Makofi)

Mheshimia Spika, jambo lingine, ili tuweze kuondokana na bei ndogo; badala ya Serikali kwenda kununua mazao ambayo haitaweza, ni vizuri Serikali ikatengeneza utaratibu wa kuweka ruzuku kwenye mazao ya mkakati yale ambayo yako matano. Mazao ya mkakati kuna kahawa, pamba, chai, tumbaku na mazao mengine yale matano ya mkakati, Serikali ingeweza kuweka utaratibu kwamba bei inaposhuka, Serikali iweze kuongeza kile kiasi ambacho inaamini kwamba itamparia faida mkulima na siyo kwenda kununua. Kununua, hawataweza kutoa fedha za namna hiyo, lakini kuweka ruzuku inawezekana kabisa. Baadhi ya nchi zimefanikiwa, Indonesia wamefanikiwa na maeneo mengine mbalimbali wamefanikiwa kwenye suala hili la kuweka ruzuku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu kujenga viwanda vya mbolea. Nataka kuuliza, hii ilikuwa kwenye mpango mkakati wa viwanda wa 2025, lakini pia hata kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi hili lipo. Ujenzi wa viwanda, kiwanda kile cha mbolea kule Kilwa Masoko tumefikia wapi? Pale hamna tofali hata moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashauri, Serikali ambayo tunasema kwamba Watanzania asilimia 70 wanategemea kilimo, hawa watu wanahitaji kuwa na kiwanda. Sasa mpango wa Kiwanda cha Mbolea pale Kilwa Masoko tumefikia hatua gani? Mbolea tunayoagiza nje ya nchi ni zaidi ya asilimia 95.

Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Minjingu ameongea Mheshimiwa Jitu Soni pale. kinazalisha asilimia tano tu. Sasa Serikali iangalie namna ya kuweza kujenga kiwanda cha mbolea na mbolea itashuka bei na baada ya hapo mwisho wa siku tutazalisha chakula cha kutosha, tutazalisha mazao ya kutosha na wakulima wetu watakuwa na hali nzuri kuliko wakati mwingine wowote ule. Kwa hali jinsi ilivyo sasa, tukiendelea kuagiza mbolea, hatutafika popote pale.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, naomba nizungumzie suala la kupeleka fedha kidogo za miradi hasa kwenye miradi ya maji. Kuna fedha zilikuwa zimetengwa, shilingi bilioni 299.9 zilitakiwa zipelekwe kwenye miradi ya maji. Hadi sasa zimepelekwa shilingi bilioni 1.67 sawa na asilimia 0.6 kutoka Hazina kwenda kwenye miradi ya maji. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Du!

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Kutekeleza kwa asilimia 0.6 hili ni anguko kubwa sana kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Niseme tu kwamba, ni vizuri Serikali iangalie yale mambo ya muhimu, ione namna ya kuweza kupeleka fedha. Kwa mfano, kulikuwa na…

SPIKA: Mheshimiwa Pascal huwa ni vizuri sana ukitumia data ukaweka na reference yako, yaani umezitoa wapi. Itasaidia sana. Endelea tu kuchangia, lakini huwa ni vizuri ukisema reference yako.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Hizi ni takwimu kutoka Kwenye Kamati ya Bajeti na zimetolewa Bungeni hapa na Wajumbe wa Kamati ya Bajeti wapo, nataka kwenye hilo nikuondolee hofu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwenye mambo ya muhimu kama haya, kama tunaweza kutenga shilingi bilioni 299.9 kulepeka shilingi bilioni 1.67 sawa na asilimia 0.6 huku ni kuwachezea Watanzania na mchezo huu wa kuwachezea Watanzania ni vizuri tukaacha. Kuna haja gani ya kuhangaika na SGR Watanzania hawana maji? Kuna haja gani ya kuhangaika na Stiegler’s Gorge Watanzania hawana maji?

Mheshimiwa Spika, ni vizuri tukaanza kugusa maisha ya Watanzania moja kwa moja kwa sababu kama mtu hana maji, huyo mtu leo unamwambia apande ndege inakuwa ni vigumu sana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Pascal, hiyo ni kengele ya pili.

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie dakika moja kwa sababu nimeingiliwa sana, naomba kwa hekima yako, kwa kiti chako…

SPIKA: Ni kengele ya pili Mheshimiwa, muda hauko upande wako tunashukuru. (Makofi)