Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. William Vangimembe Lukuvi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ismani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa muda ulionipa. Nami nakupongeza sana kwa utendaji wako na usimamizi mkubwa wenye tija wa Bunge letu Tukufu, nawapongeza sana Kamati yangu ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa ushauri wao ambao wamekuwa wanatupa kila wakati, mimi na Naibu wangu tumefurahi, na tumenufaika sana na ushauri wa Kamati hii, tukiwa kwenye mikutano, tukiwa kwenye ziara, tumefaidika sana na Wajumbe wote kwa pamoja wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti. Kwa hiyo nawapongeza sana na tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika utendaji wa kazi ambazo tumekabidhiwa mara zote sisi tunatekeleza kwa malengo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Pili, tunatekeleza kwa maelekezo mahsusi, ya Mheshimiwa Rais na Viongozi Wakuu, Makamu na Waziri Mkuu maagizo ya Cabinet lakini pia maelekezo ya Bunge lako Tukufu. Maelekezo ya Bunge lenyewe lakini kupitia Kamati yetu ambayo tunayo kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizi nafikiri niseme machache ambayo yamesemwa kwenye Kamati, naunga mkono sana, Kamati hii na maoni yake, lakini niseme mambo matatu yaliyogusiwa ndani ya ripoti hii, la kwanza nataka niseme, kwamba pamoja na kutekeleza kwa misingi niliyoisema lakini tunatekeleza kwa mujibu wa Sheria. Kwetu sisi Wizara ya Ardhi, Sheria kuu zaidi tunazozisimamia ni mbili kwa upande wa ardhi; Sheria Na. 4 na Na. 5 za mwaka 1999. Sheria Na. 4 inahusu zaidi ardhi hizi ambazo mara nyingi sana zinasimamiwa na kila anayemilika ardhi kwa kutumia sheria hii huwa tunampa karatasi hii, hati ya namna hii. Hii ni hati inayotolewa kwa kusimamiwa na Sheria Na. 4 ya mwaka 1999, inaitwa ardhi ya jumla.

Mheshimiwa Spika, tunaposema habari ya ufutaji wa ardhi wa hati unaoanzia kutoka kwenye Halmashauri kama alivyoeleza Mbunge wa Korogwe Vijijini ni hati hizi ndizo zinahusika na utaratibu ule lakini pia tunayo Sheria Na. 5 ya Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999, inahusu ardhi ya vijiji. Kabla ardhi haijageuzwa haijahaulishwa kuja kutolewa hati hii, ardhi zote za vijiji zinatolewa hati ya namna inaitwa hati za kimila. Wanaopata ardhi hii hawana ukomo wa umiliki hawalipi kodi, lakini imeweka kiwango kila kijiji hakipaswi kutoa zaidi ya ekari 50. Kwa hiyo tuna ardhi zinatawaliwa na Sheria mbili, lakini na hati za utambulisho ziko mbili.

Mheshimiwa Spika, nimesema nianze na hii ili angalau Waheshimiwa Wabunge tuelewane. Sasa katika usimamizi wa sheria kama nilivyosema Sheria ya Ardhi hii inayotawala Sheria ya Vijiji, mamlaka makubwa zimepewa Serikali za Vijiji zenyewe, ila inapozidi 50 uhaulishaji sasa inabidi ngazi ya Wilaya izungumze, ije kwetu Wizarani, tumpelekee Mheshimiwa Rais, ikimpendeza anakubali kuibadilisha ile ardhi ya kijiji kuja ardhi ya jumla na ndipo mtu anaweza akamiliki ardhi kwa hati kama hii, kama ni ekari 50 kwa matumizi yoyote, kama ardhi iko kijijini.

Mheshimiwa Spika, sasa hati hizi ziko nyingi sana, hatutozi kodi lakini tunaamini masikini wa Tanzania wanaopendwa sana Serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli ndio wanatumia hati hizi na ndio maana hazitozwi Kodi. Wanaotumiwa hati hizi sasa hivi wanakaribia milioni moja katika vijiji vyetu, lakini hawa ni mashamba, wanakaribia milioni moja. Kwenye hati hizi wa mashamba wanakaribia 2,000, mashamba makubwa, wanaomiliki kwa hati hizi, yako mashamba yasiyopungua 2,000 yenye ekari zisizopungua milioni sita zinazotumika kwa shughuli mbalimbali za kilimo za ufugaji na wamilika hao 2,000 wanazo hati hizi.

Mheshimiwa Spika, sasa moja ya jambo ambalo tumeshauriwa hapa na ambalo limezungumzwa na ndugu yangu Mheshimiwa Msigwa hapa, alitaka kuzungumza kwamba utekelezaji wa Sheria hii una mashaka na amefika mahali mpaka amemhusisha Rais, lakini nashukuru Waheshimiwa Wabunge wengi mmechangia hapa, kwamba utoaji wa ardhi au ufutaji wa hati hizi unafuata Sheria na hata siku moja, haijawahi kutokea Rais akaniagiza mimi nifute hati ya mtu fulani au nimpelekee hati ya mtu fulani afute, hajawahi kuniambia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanaoanza kupendekeza ardhi hii kwanza, mnakumbuka tulipoanza Awamu ya Tano, mimi mwenyewe nilileta dodoso hapa kwa kila Mbunge kuuliza kero zenu, ninyi ndio mlijaza dodoso na kueleza kero zenu, tukatengeneza kitabu, asilimia 60 ya kero zile ilikuwa mashamba pori na migogoro ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, baada ya hapo tukatengeneza ratiba ya utekelezaji na …

MHE. ZITTO R. Z. KABWE: Mheshimiwa Spika, kuna ushahidi wa maagizo ya Rais.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Wewe Zitto una kelele sana, sikiliza wenzako waseme.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, achana naye huyo.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ninyi mlipoleta zile kero ndipo tukatengeneza ratiba ya utekelezaji, kwa hiyo kutokana na maelekezo yenu, tumefuatilia, tumerudisha yale maelekezo yenu kule Wilayani, wamefuatilia. Katika uhakiki wa mashamba haya 2,000 mpaka sasa katika miaka mitatu hii, tumeshafuta mashamba 46 kwa mujibu wa Sheria, lakini chanzo ni ninyi, lakini pia outcry ya wananchi na Viongozi mbalimbali wamepita kwenye Kampeni wamesikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sababu ni moja tu, watu katika hawa 2,000 tuliowapa hizi hati, wanayo mashamba makubwa kama walivyosema Wajumbe Fulani. Hati hizi ukipewa kuna masharti ya matumizi huku nyuma, umri wa matumizi umeandikwa kwenye hati hizi, hati hizi hakuna umri wa matumizi, lakini unatakiwa ukipata ardhi ya shamba, angalau uhangaike moja ya nane kwa mwaka uendeleze. Kwa hiyo matarajio ya hati hii angalau katika kipindi cha miaka minane utakuwa umejiendeleza kumaliza hili shamba, lakini wako watu wengi, wengi sana, ambao wamepokea mashamba haya, matokeo yake siku zote hizi za nyuma walikuwa wanatumia kwa ajili ya kuweka rehani kupata mtaji wa biashara na kufanya biashara nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa mbele yangu nimekuja na daftari hili, mimi nina privilege ya kujua siri zenu zote, humu ndani kuna watu ambao wamepewa ardhi na wamechukua mkopo, hapa kuna zaidi ya trilioni moja nimeshika, kuna zaidi ya dola mia tano hapa na kuna fedha tasilimu zaidi ya bilioni 800 watu wamekopa, kwa rehani na hii ni taarifa ya Benki kuu, kwa rehani ya ardhi, lakini ninyi wenyewe mnajua, hivi kama kweli kilimo cha Tanzania kingewekeza zaidi ya trilioni moja si nchi ingetikisika, fedha ziko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi tunao ushahidi baada ya kufanya uhakiki kwamba watu walichukua hizi fedha kwa sababu usimamizi ulikuwa hafifu, wamechukua kama kinga, wamechukua Benki, pamoja na kuandika madhumuni ya kuendeleza yale mashamba, lakini Benki hazifuatilii, Benki zinataka tu return ya biashara zao, wameenda kuwekeza Dubai, wamenunua apartment, wanawekeza biashara na kulipa papo kwa papo mashamba yamebaki pori, hayakuendelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi Wabunge mkisema kuna mashamba pori huku, watu wamekopa hela benki, lakini watu wanapambana kulima yale mashamba, halafu anatokea siku moja mtu anatishatisha hivi, miaka 10 au 20 yeye anaendelea kuongeza thamani ya Kampuni yake, kutokana na mtaji unaotokana na thamani ya ardhi, lakini kule kwenye shamba haendi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kuwahakikishia kwamba kwa maelekezo ya Ilani, Chama cha Mapinduzi kimetuelekeza tufanye uhakiki na tuchukue mashamba haya na ndiyo maana tumefanya hivyo. Kwa sasa tumechukua mashamba 46 katika mikoa ifuatayo: Arusha (2); Kilimanjaro (1); Dar es Salaam (2); Morogoro (18) na Kilosa peke yake ni 12; Iringa (1); Pwani (4); Simiyu (2); Tanga (17); Kagera (1); Mara (1); Lindi (1) alilotaja Mheshimiwa Nnauye. Shamba limetoka kwenye Jimbo lake na bado namba 38, umetaja namba 37 na 38 tumepeleka. Kwa hiyo, huu ni utekelezaji wa maelekezo yenu kumbe tufanye nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ndugu zangu wakati mwingine, Mheshimiwa Peter hayuko hapa, huna sababu ya kuunda Kamati Teule ya kwenda kuchunguza uhalali wa kazi aliyoifanya Rais kisheria. Ninyi mnaofikiria maneno haya hangaikeni na Majimbo yenu tu kwa sababu Mheshimiwa Rais ametimiza wajibu kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, aliyesababisha hii ni ninyi, wananchi wana shida na tumetekeleza. Fikiria tumefanya uhakiki wa mashamba 2,000 tumegundua 46, kumbe tungefanya nini? Mashamba haya mnaachiwa wenyewe ili muwapangie wale wananchi walioko pale wanaitwa wavamizi ili nao wawe wamiliki wa mashamba hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niseme tu kwa Waheshimiwa Wabunge tushirikiane, hili jambo ni jema, hakuna sababu ya kutafutiana maneno hapa, Mheshimiwa Rais anatekeleza wajibu wake na ni msikivu sana. Yeye hafuti, mapendekezo yanatoka huku.

Mheshimiwa Spika, mashamba yaliyotajwa ya Mohamed Enterprises Company hapa amesema Mheshimiwa Peter. Mohamed Enterprises anamiliki mashamba makubwa 21 nchi hii…

WABUNGE FULANI: Eeeee.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Yako Tukuyu, Rungwe, Mombo, Korogwe na Same.

MBUNGE FULANI: Efatha.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Hivi asipoendeleza tunafanyaje? Kwa hiyo, tumefanya uhakiki, kwanza niwaambie mashamba yaliyofutwa ni sita lakini onyo alipata mashamba 12. Baada ya kupata onyo, Afisa Ardhi pale akawa anachezacheza Naibu Waziri akamdhibiti amemuondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo nilipomwagiza Naibu Waziri, tumepiga na picha na vielelezo vyote tunavyo, tukagundua ukweli mashamba sita hana la kufanya. Nataka nimwambie hayo sita na yenyewe tumempa angalizo tunamtazamia, asipotekeleza tuliyomwambia nayo yako kwenye mstari mwekundu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kuwaambia sheria itasimama na itachukua mkondo wake bila kumuonea mtu lakini bila kumuogopa mtu. Sisi tumeelekezwa kulinda rasilimali za Taifa. Kwa hiyo, naomba kama Wabunge tushirikiane, haya maneno madogo madogo ya watu wamechukua rushwa sijui wamefanya nini hayana maana, tushirikiane katika kusimamia mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana wote mliochangia na najua wengi mmesoma kwenye mitandao kwamba katika kutekeleza mambo haya mimi na Naibu wangu tumechukua rushwa. Kama tunaweza kuchukua rushwa na tukafuta basi hiyo nzuri. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Bado Rukwa.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, kule Rukwa kulikuwa na shamba kubwa ambalo lina mgogoro mkubwa na Nabii wa Efatha, Mheshimiwa Mwingira, kwa hiari yake mwenyewe amekubali kutoa ekari 3,000 na kuwarudishia wananchi wa vijiji vitatu. Kule Same Mheshimiwa Mama Kilango tumekwenda wenye mashamba makubwa wamekubali kutoa mashamba yao. Ulanga juzi wawekezaji wamekubali kuweka ekari 9,000 kwa wananchi ili angalau na wenyewe wasitazame tu macho kwenye ardhi ambayo inamilikiwa na wenye mashamba makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka kusema kwa kweli Wabunge wote tushirikiane kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi hii kubwa anayoifanya. Anafanya kwa ajili yenu, Wabunge wa CCM wote tumeahidi kwenye Ilani kwamba tutafanya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, Mheshimiwa Rais mmempongeza sana ametangaza Wizara saba tushirikiane, tunataka kuwahakikishia kwamba Wizara saba tutafanya lile jambo ambalo ametuagiza Mheshimiwa Rais la kutokomeza migogoro. Nimemwomba Mheshimiwa Spika tuwashirikishe na ninyi Waheshimiwa Wabunge, mimi ndiyo Mwenyekiti. Tuwashirikishe na ninyi Wabunge kama mna ziada zaidi ya yale ambayo mlisema tuko hapa wiki hii. Mtu yeyote ambaye anafikiri ana kero ya ardhi ya ziada atuandikie ili tuongeze katika agenda tulizonazo na tumepewa muda mfupi sana tupeleke kwa Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, kwa niaba yake na kwa niaba yenu, tunashukuru sana kwamba angalau wazo hili la Mheshimiwa Rais mmelichukua na tumeona watu wote wananchi wenye nia njema wamefurahia jambo hili.

Mheshimiwa Spika, National Housing haina matatizo ya kulipa deni, ina uwezo wa kulipa deni na kila mwezi inalipa shilingi bilioni tano na milioni mia sita kutokana na fedha yake yenyewe. Kwa hiyo, ina uwezo wa ku-service madeni na ina mali ambayo zina thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 5.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, nawashukuru sana Wabunge wote kwa kunisikiliza na kwa kuchangia hoja hii. (Makofi)