Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Mahmoud Hassan Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. MAHMOUD H. MGIMWA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KILIMO, MIFUGO NA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii tena kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuhitimisha hoja yangu ya taarifa ya mwaka ya Kamati ya Kudumu ya Kilimo, Mifugo na Maji. Pia naomba nichukue fursa hii kuwashukuru sana Wajumbe wa Kamati yangu ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa kuandaa taarifa nzuri ambayo imeungwa mkono na wachangiaji walio wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa jinsi walivyokuwa wanafuatilia mijadala iliyokuwa inaendelea hapa Bungeni. Wabunge waliochangia walikuwa 19; 6 wamechangia kwa maandishi na 13 wamechangia kwa kusema.

Mheshimiwa Spika, katika michango ya Waheshimiwa Wabunge, wote wameonekana kuunga mkono mapendekezo na Maazimio ya Kamati. Kwa hiyo, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwamba kwenye mambo yote tuliyowasilisha wametuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya kipekee, niwashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri; Mheshimiwa Hasunga, Mheshimiwa Prof. Mbarawa na Mheshimiwa Mpina, wote walipokuja kutoa maelezo yao hapa walionyesha hawana tofauti na Kamati na wamekubaliana na hoja zilizowasilishwa na Kamati. Wametuahidi mbele ya Bunge lako Tukufu watakuwa tayari kuzifanyia kazi hoja zote zilizowasilishwa na Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba nijielekeze katika maeneo machache kabla sijahitimisha hoja ya mjadala huu. Eneo la kwanza, Kamati yangu inakuomba wewe kupitia Bunge lako Tukufu uandae Kamati Maalum itakayokuwa inashughulikia Maazimio yanayotokana na taarifa za Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kwa nini sisi kama Kamati tumeliona jambo hili? Hii ni kwa sababu kila mwaka tumekuwa na tabia ya kurudia hoja za Kamati, kwa hiyo, tunashindwa kuelewa ni hoja zipi ambazo zimeazimiwa na Bunge lako Tukufu zimetekelezwa na kama tungekuwa tunapata taarifa ya utekelezaji wa hoja hizo tungekuwa kwenye position ya kutozirudia tena. Kwa hiyo, sisi kama Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji tunakuomba sana uunde Kamati Maalum itakayokuwa inashughulikia hoja mahsusi kama ambavyo tunawasilisha wakati huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo napenda kulitolea maelezo kidogo ni kuhusu Bodi ya Mazao Mchanganyiko. Tunaomba Bodi hii ipewe pesa ya kutosha kwa sababu ni eneo pekee ambalo Serikali imejiingiza kufanya biashara kisheria. Malalamiko yaliyokuwepo kwenye maeneo mengi ya wakulima wa mahindi, mbaazi na nafaka mbalimbali kama Bodi ya Mazao Mchanganyiko itapewa pesa za kutosha matatizo ya wakulima kwenye hayo maeneo hayatakuwepo.

Mheshimiwa Spika, pia pesa hizi wapewe kwa wakati. Unakuta safari hii Bodi ya Mazao Mchanganyiko imepewa pesa mwezi Desemba wakati mazao yanavunwa mwezi wa Juni, kwa hiyo, tunaweka wakulima katika kipindi kigumu. Kwa hiyo, hata kama sasa hivi wanapata nafasi ya kwenda kununua mazao kwenye maeneo hayo, wakulima watakuwa na shida ya kuanza kulima upya katika msimu wa kilimo. Kwa hiyo, tunaomba Bodi ya Mazao Mchanganyiko ipewe pesa ya kutosha au itengenezewe utaratibu wa kupata mikopo kwa njia rahisi kusudi kuweza kununua mazao kutoka kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili kwenye eneo la Bodi ya Mazao Mchanganyiko wawe na wafanyakazi wa kutosha. Sasa hivi asilimia 95 ya wafanyakazi wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko wapo Mtwara, kwa hiyo, maeneo mengine hawawezi kupata zile huduma za Bodi ya Mazao Mchanganyiko. Hata utaratibu wa kununua nafaka kwenye maeneo mengine sasa hivi haupo, wamefanya concentration kwenye eneo moja tu la korosho, hakuna wafanyakazi wowote ambao wamewaweka kwa ajili ya kununua nafaka kwenye maeneo mengine. Naomba hili tuliangalie na waongezewe vifaa kwa maana ya magari. Mara ya mwisho wamepewa magari nane (8) lakini hayakidhi kutokana na hali halisi kwa sababu ni eneo pekee ambalo litamsaidia mkulima aweze kufanya kazi zake ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Benki ya Maendeleo ya Kilimo ilianzishwa kwa ajili ya kuwasaidia wakulima, kwa hiyo, ifanye kazi specific kwa sheria iliyoanzisha benki hii. Pale katikati Benki ya Kilimo nayo ilikuwa inaanza kutengeneza utaratibu wa kukopesha hela kwa watu wengine, ifungue matawi kwa ajili ya wakulima, wavuvi pamoja na wafugaji waweze kupata hela kwa riba nafuu ingeweza kuwasaidia sana watu kwenye maeneo yetu. Kusudi twende kwenye viwanda lazima tuhakikishe tunawawezesha sana watu wetu kwenye maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mpina na Naibu wake Mheshimiwa Ulega, kwanza wamekuwa wasikivu sana. Kutokana na changamoto zilizojitokeza katika Operesheni Sangara wameamua kuanzisha mchakato wa marekebisho ya Sheria Na.22 ya mwaka 2003 pamoja na Kanuni zake za 2009. Kama tutaendelea kuwa na malalamiko bila kurekebisha sheria tutaendelea kuwalaumu Mawaziri hawa lakini nawashukuru wamekubali, wamesikiliza hoja za Wabunge na leo hii Waziri ametamka wazi kwamba watahakikisha huo mchakato wa kubadilisha Sheria Na. 22 ya mwaka 2003 pamoja na Kanuni zake unafanyika kabla ya mwezi Julai, 2019. Kama sheria zile zitarekebishwa mapema, malalamiko yote ambayo yapo kwa wavuvi hayatakuwepo kwa sababu wavuvi nao watakuwa wana haki ya kusema zile changamoto ambazo zinawakuta kwenye maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo napenda niwapongeze wenzetu hawa sekta ya mifugo na uvuvi ni kuanzisha Dawati la Sekta Binafsi. Hapa wananchi wanapata nafasi ya ku-chip in. Taasisi nyingi zimejihusisha kwenye sekta hii, kwa hiyo matatizo yote ya wafugaji na wavuvi yanaweza kutatuliwa kwenye Dawati hili na tumeliona hili jambo, ndiyo maana wamekuwa tayari hadi kuanzisha mchakato wa marekebisho ya sheria.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii tena kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa kuleta Bungeni Muswada wa Sheria ya Huduma ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya mwaka 2018. Sheria hii itakaposainiwa na Mheshimiwa Rais itaboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi na majitaka ambalo lilikuwa tatizo kubwa katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni imani yangu kuwa safari hii Serikali itakubaliana na mapendekezo ya Wabunge ya kuongeza shilingi 50 kwenye kila lita ya mafuta kwa maana ya petroli pamoja na dizeli. Tukiongeza shilingi 50 kwenye huu Mfuko wa Maji wa Taifa tutaweza kutunisha fedha zake ambapo utasaidia watu wengi katika vijiji waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii tena kuipongeza Serikali chini ya Rais wetu mzalendo Dkt. John Pombe Magufuli kwa hatua madhubuti alizochukua katika kuimarisha tasnia ya korosho. Ni matumaini yangu kuwa Wizara yenye dhamana itaendelea kushughulikia changamoto zilizobainika pamoja na ushauri wa Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hakuna jambo lolote muhimu katika nchi linaloweza kuendelea bila research. Ni wakati muafaka sasa hivi wa Serikali kutenga asilimia 1 ya DGP kwa ajili ya research. Kwenye eneo hili tunaiomba sana Serikali iondoe kigugumizi kwa sababu kumekuwa na malumbano katika research. Hakuna mtu anayekataza research, wafanye research na watuasaidie kuweka wazi kusudi tuweze kuwasaidia wakulima wetu katika maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, sasa naomba Bunge lako Tukufu liazimie hoja na Maazimio ya Kamati kama yalivyowasilishwa na Kamati.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Spika, naafiki.