Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa

Hon. Daniel Nicodemus Nsanzugwako

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kasulu Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa

MHE. DANIEL N. NSANZUGWANKO: Mheshimiwa Spika, nami nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja hii muhimu sana. Hata hivyo, nina mambo mawili. La kwanza ni kuwakumbusha wenzetu kwamba mapori haya ya Burigi na Biharamulo yako jirani na Mkoa wa Kigoma na pori letu mashuhuri sana la Kigosi Moyowosi. Nilitarajia katika kufanya Burigi, Biharamulo ziwe National Parks na Kigosi Moyowosi ingekuwa National Park kwa sababu haya mapori yanategemeana na yako jirani sana. Isitoshe katika Pori la Kigosi Moyowosi kuna eneo la Ramsar site, eneo chepechepe ambalo kwa kweli kwa wenzetu wa UNESCO wameshalitangaza kama ni urithi wa dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitarajia kwa muktadha huu na kwa dhamira hii njema kwamba Burigi, Biharamulo inge- incorporate na Kigosi Moyowosi National Park kwa sababu ikolojia ile ni moja sisi tunatoka maeneo yale tunafahamu. Hofu yangu ni nini sasa? Endapo Kigosi Moyowosi mtaiacha tafsiri yake ni kwamba wale majangili na watu wabaya wataacha Burigi na Biharamulo National Parks watashuka huku, ni kushuka tu pale, kwa sababu kutoka Biharamulo kuja Kigosi Moyowosi ni chini ya kilomita 60, ni jirani sana. Kwa hiyo, angalizo langu kwa nia njema hiihii, naomba sana Mheshimiwa Waziri na timu yako hata ikiwapendeza basi Kigosi Moyowosi na Malagarasi wet land iwe chini ya uangalizi wa TANAPA vinginevyo yale maeneo yanaharibika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ni kulinda Mto Malagarasi. Mto huu jiografia yake ilivyo unapita katikati ya Pori la Kigosi Moyowosi na umeharibika sana kwani umevamiwa sana. Kwa hiyo, nasema tena ni hoja njema sana, ni jambo jema sana tena isitoshe limechelewa kwa sababu mimi nimewahi kuhudumu kwenye Tume ya Wanyamapori katika mambo tuliyoyapendekeza miaka ya 2013 ilikuwa ni kufanya mapori haya yote yawe National Park ili kupunguza uhalifu, ujangili na kadhalika. Ombi langu na angalizo langu kwa Serikali ni kwamba angalieni namna bora sasa ya kuilinda Kigosi Moyowosi kwa sababu wewe Spika ni Mhifadhi ni ikolojia ile ile tu na wanyama ni wale wale tu, mkibana huku Biharamulo maana yake uhalifu utashuka Kigosi Moyowosi. Kwa hiyo, angalizo langu kwa Serikali lilikuwa ni hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nadhani Mheshimiwa Waziri anakumbuka kwamba wale ndege wasiopatikana popote duniani mwezi wa Juni na Julai wanakwenda Kigosi Moyowosi. Uwanja wa Ndege wa Kigosi Moyowosi ulijengwa na wawekezaji, kwa hiyo, Uwanja wa Ndege wa Chato utasaidia sana kwani watalii watatoka Chato wanashuka kwa ndege na ni dakika 20 au 15 wanakuja Uwanja wa Ndege wa Kigosi Moyowosi. Ule uwanja wa ndege bado upo na ni uwanja muhimu sana. Kwa hiyo, maeneo haya ni mazuri sana kwa ajili ya ku-promote utalii katika Taifa letu. Nina hakika kupandisha hadhi mapori haya na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Chato eneo lile sasa litaimarika katika tasnia hii ya utalii.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, nilitaka niongezee hayo kwa ajili ya umuhimu wa Kigosi Moyowosi. Ahsante. (Makofi)