Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kwa masikitiko makubwa sana nikutaarifu tu kwamba taarifa ambayo umesomewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Wajumbe wa Kamati hatujapata fursa ya kuipitia; na sijajua lengo hasa ni nini, taarifa tumekuja kukutana kama ambavyo wewe umeisikia hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasimama mbele ya kiti chako kwa dakika kumi ambapo dakika zote hizi kumi nakwenda kuzungumzia suala moja tu na suala hili leo ninazungumza ni mara ya tano na sio lingine ni juu ya SONGAS.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashindwa kuelewa ni kwa nini suala hili limekuwa ni gumu sana kuchukuliwa hatua. Nashindwa kuelewa ni kwa sababu gani Serikali imekuwa ikisuasua kuchukua hatua kwenye suala hili la ubadhirifu wa rasilimali za wananchi wa Tanzania. Waheshimiwa Wabunge nafikiri hawajapata fursa ya kuelewa vizuri suala hili ndiyo maana wanashindwa kujua uzito wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufupi sana, utafutaji wa gesi asilia kwenye visima vya SONGAS ulianza mwaka 1969, mpaka kufikia mwaka 1990 Serikali ilikuwa imeshatumia zaidi ya dola milioni 150. Baada ya tafiti kuonesha kwamba gesi inaweza kutumika kuzalisha umeme, Serikali kwa haraka sana ikatangaza zabuni na wakampata mzabuni ambaye ni SONGAS.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mpaka hatua ya mzabuni kupatikana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TPDC ilikuwa inamiliki visima vitano vya gesi ikiwepo kisima namba tatu, nne, tano, saba na tisa. Pia TPDC walikuwa wanamiliki mitambo ya kuchakata gesi ambayo pia ilikuwa ni mali ya Serikali. TANESCO walikuwa wanamiliki mitambo ya kuzalisha umeme ambayo yalikuwa ni majenereta manne, yapo pale Ubungo Dar es Salaam. Pia eneo la Songosongo ambapo visima hivi vinapatikana, lilikuwa ni eneo ambalo lipo chini ya TPDC kwa maana hiyo lilikuwa ni eneo la Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zaidi, Serikali ikaona ili mradi uweze kuanza ikaenda kuchukua mkopo kutoka World Bank Dola za Kimarekani milioni 216, sasa viini macho vinaanzia hapo. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliwapa SONGAS visima vyake vyote vitano bure bila gharama yoyote kulipwa! Kiini macho namba mbili, Serikali iliwapatia SONGAS mitambo ya kuchakata gesi bure bila gharama yoyote kulipwa. Kiini macho namba tatu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliwapatia SONGAS zile jenereta nne za TANESCO ambazo zipo pale Ubungo bure bila gharama yoyote kulipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ile asilimia tisa ambayo kwenye mkataba inaonesha kwamba ndio hisa za TANESCO walikisia tu kwamba tathmini ya eneo zima lile la TANESCO ni dola milioni moja, huu ni wizi wa mchana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hisa ambazo zinamilikiwa na TPDC asilimia 29. Hisa hizi wamefanya makisio bila kuwa na evaluation report. Wanasema eneo la Songosongo na njia yake ya kupitisha bomba la gesi linakadiriwa kuwa na thamani ya dola milioni tatu lakini ukiuliza evaluation report iko wapi, haipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kiini macho cha mwisho, japokuwa mitambo na kila kitu SONGAS walipatiwa na Serikali, lakini bado Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia TANESCO tunawapa fedha za fidia SONGAS na wakati katika uwekezaji Serikali ndiyo imewekeza kwa kuwapa mitambo na kila kitu kwa maana ya capacity charge tunatoa sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa kuliko yote, ningependa Serikali ituambie, kwamba dola milioni 60 za kwenye ESCROW akaunti zimekwenda wapi? Hii ni kwa sababu Serikali pamoja na mbia wakati wanakubaliana kufanya mradi huu, walikubaliana kuweka dola milioni 60 kwenye akaunti ya ESCROW ilikuwa ni kama kinga kwamba ikitokea mradi usipotekelezeka, basi mwekezaji hiyo pesa anaichukua. Hii pesa ilitokana na kodi ambayo walikuwa wanakatwa wananchi wa Tanzania kwenye petroli na dizeli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mpaka hivi ninavyozungumza na wewe hizi fedha kwenye akaunti hazipo na kibaya zaidi unapowauliza wahusika wanasema kwamba zimetumika kununua mtambo namba tano na vielelezo hawana. Sasa unaweza ukaona ni kwa namna gani katika mradi huu wa SONGAS kuna wizi mkubwa kiasi hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Menejimenti ya Songas ilipata fursa ya kukutana na Kamati. Niliona kwenye taarifa ya Gazeti la The Citizen la tarehe 2 ambalo linaonesha Katibu Mkuu wa Nishati na Madini anaelezea kwamba mapendekezo yaliyokuwa yanatolewa na Kamati iliyoundwa na Mheshimiwa Spika, yameshaanza kufanyiwa kazi miezi miwili iliyopita. Huu ni uongo uliopindukia. Kwa sababu baada ya kukutana na wahusika, Menejimenti nzima ya Songas wanakiri, wanasema hata hiyo ripoti hawajawahi kuisikia wala hawaijui. Sasa ni bahati mbaya tunakuwa na aina ya watumishi Serikalini ambao wanakuwa wanatoa taarifa za uongo bila hata kuwa na aibu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua ni kitu gani...
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
MHE. JESCA D. KISHOA: …ni kitu gani ambacho…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kishoa kuna taarifa. Mheshimiwa Subira Mgalu.
Hii hoja ni ya Kamati, siyo hoja ya Serikali. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, mnafahamu, atakayehitimisha hoja hapa ni Mwenyekiti wa Kamati na sio Mawaziri. Kwa hiyo, yeye hapo ni kama Mbunge mwingine kwenye hili. Mheshimiwa Subira Mgalu.
TAARIFA
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vyovyote vile siwezi kupokea taarifa hii, maana hata Wabunge humu ni mashahidi. Hakuna mtu mwenye uwezo wa kuwa na access na hiyo taarifa. Uwezekano wa kupata taarifa hiyo na kuipitia ni mgumu kuliko kawaida. Nami niseme tu, kama tutaendelea kuwa humu ndani na kuendelea kudanganyana kwamba taarifa imekabidhiwa kwenye Umma na kwa hiyo, mambo yanaenda sawasawa, tunakuwa hatutendei haki nafasi zetu kama viongozi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee…
MHE. SAED A. KUBENEA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kubenea.
TAARIFA
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea kwa mikono yote miwili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, udhaifu mkubwa unaoonekana kwenye mikataba ni sawasawa na baba ameshikwa na mtoto wake, amefungwa mikono na miguu, halafu mtoto anamwita jirani amcharaze viboko baba yake.
Hicho ndicho ambacho kimefanyika. Watoto wa Tanzania…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kishoa malizia dakika moja, kengele ya pili imeshagonga.
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina jambo moja tu na ninaomba popote pale alipo Mheshimiwa Rais anaposikia sauti hii, achukulie hatua suala hili, kwa sababu Serikali yoyote inayojinasibu kama ni Serikali inayopinga ufisadi, haiwezi kwa namna yoyote ikaruhusu mkataba wa Songas ukaendelea kuwepo. Ahsante. (Makofi)