Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KIZA H. MAYEYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika ripoti hii ya Kamati. Kwanza kabisa, nianze kwa kumpongeza Waziri wa Nishati pamoja na Waziri wa Madini kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze katika suala la REA, bado kumekuwa na changamoto kubwa Mheshimiwa Waziri katika suala la REA III. Vijiji vingi katika maeneo mengi bado umeme haujafika. Kwa mfano tu, katika Mkoa wangu wa Kigoma kuna Vijiji kwa mfano Msimba na Kamara umeme umepita katika eneo moja lakini eneo lingine umeme haujafika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna vijiji kwa mfano, Kamanyangwe, Kihinga, Kalongolonge na Kingungo, bado hawajapata umeme lakini umeme umepita barabarani. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri pamoja na kazi nzuri ambayo mnaifanya, lakini mhakikishe kwamba vijiji vyote vinaweza kupata umeme huu wa REA III. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee tena suala la gridi ya Taifa. Sote tunajua kwamba Mikoa ya Kigoma na Katavi mpaka sasa hatujaingia katika gridi ya Taifa. Tunatumia umeme huu wa Diesel TANESCO ambao ni gharama kubwa na kusababishia Serikali yetu hasara kubwa. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, kwa sababu tayari mmeanza sasa mchakato, basi hiyo Februari, 2020 gridi ya Taifa iweze kukamilika katika Mikoa hii ya magharibi, Kigoma na Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie tena suala la mradi wa Mto Malagarasi. Nniseme kwamba wananchi wa Kigoma tumeupokea vizuri mradi huu na tunaunga mkono juhudi za Serikali kwa kuanzisha mradi huu wa Malagarasi Megawati 45 kutoka Malagarasi kwenda Kidahwe. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri pesa ziende kwa wakati, Wakandarasi wamalize kazi kwa wakati. Wananchi ambao wamepisha mradi huu, waweze kupewa fidia zao kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilimwuliza Mheshimiwa Waziri kwenye Kamati akaniambia tayari wameanza kuthaminisha. Naomba sana wananchi hawa kwa sababu wamejitoa na kupisha mradi huu waweze kupatiwa fidia zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nigusie katika suala madini. Wachimbaji hawa wadogo wa madini, wengi ni vijana wa Kitanzania ambao wameamua kujiajiri kwa kufanya kazi, lakini bado wamekuwa na changamoto kubwa, kwamba kwanza hawana elimu ya kutosha, lakini hawana vifaa na hata pesa hawana. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, kaka yangu, Mheshimiwa Doto awaangalie hawa wachimbaji wadogo kwa jicho la pili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tozo nyingi sana za ushuru. Tumeona hapa katika ukurasa wa 22 wa Kamati, kuna VAT asilimia 18, withholding tax 5%, service levy 0.3, inspection 1% na mrahaba wa madini ghafi ya vito 6%. Michango hii imekuwa ni mingi. Tozo zimekuwa nyingi kwa hawa wachimbaji wadogo wadogo. Kwa hiyo, kama tozo zitakuwa ni nyingi bado hatutaweza kuepuka tatizo hili la wachimbaji kutorosha madini. Naomba Serikali iangalie iweze kupunguza hizi tozo kwa wachimbaji wadogo wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukiona kwamba wachimbaji hawa wadogo wadogo mara kwa mara vifo vimekuwa vikitokea katika maeneo yao. Najua ni kwa sababu hawana uelewa wa kazi ambayo wanaifanya. Naiomba sana Wizara itoe elimu ya kutosha kwa wachimbaji wadogo wadogo ili waweze kuondokana na madhara haya ya vifo ambayo wamekuwa wakipata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, nizungumzie suala la GST. Hawa wanajiolojia ni watu muhimu sana ambao wanaweza kutusaidia kutambua madini mbalimbali katika maeneo mbalimbali, lakini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kukosa bajeti na fedha za kutosha. Naiomba sana Serikali iwapatie watu hawa pesa waweze kuzunguka katika maeneo mbalimbali, waweze kutuambia ni madini gani yanapatikana katika maeneo hayo hususan ukiwepo Mkoa wangu wa Kigoma ambao naamini kuna madini ya chokaa na hata dhahabu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)