Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Ruth Hiyob Mollel

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyoko mezani. Naomba ku-declare interest kwamba mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na naunga mkono moja kwa moja hoja iliyowasilishwa hapa mezani. Nitazungumzia maeneo matatu, nitazungumzia suala la Magereza, economic diplomacy na diaspora.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kwenye Kamati kwamba Magereza yetu yana msongamano mkubwa sana na ilipofika Desemba, 2018 Gereza la Segerea lina wanaume 1,723, lakini wafungwa ni 158 tu wafungwa, kwa hiyo walioko rumande ni 1,565. Wanawake wako 313 na waliofungwa ni 66, kwa hiyo rumande wako 247. Kwa hiyo tuseme jumla pale Segerea kuna Mahabusu 1,812. Hii ni namba kubwa sana kwa watu ambao wako Mahabusu, upelelezi unaendelea haujakamilika, wako Mahabusu wanatumia pesa za walipakodi kula, wako Mahabusu badala ya kuweko uraiani wakifanya kazi na kuongeza juhudi za kusukuma gurudumu la maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna haja kubwa sana sasa Serikali ya Awamu ya Tano kuangalia mfumo wa kutoa haki, ukianzia na TAKUKURU, ukija na DPP mpaka na Polisi kuhakikisha kwamba upelelezi unafanyika kwa wakati kusudi hawa Mahabusu waweze kuhukumiwa watoke, kwa sababu wanapoendelea kukaa Mahabusu huu ni ukiukwaji wa haki za binadamu na si sahihi na hata Mungu hapendi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napendekeza kwamba upelelezi ukamilike kwanza kabla ya kupeleka watu Mahakamani, wapelekwe upelelezi ukiwa umekamilika, kesi inasikilizwa, wanatoka na endapo kuna umuhimu wa kumweka mtu Mahabusu, tunayo best practice Zanzibar ambapo Zanzibar unakaa Mahabusu tu miezi tisa kama upelelezi haujakamilika unaachiwa huru. Kwa hiyo, hili jambo ni jambo la kufanyia kazi na namshauri sana Mheshimiwa Waziri, liweze kufanyiwa kazi…

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. RUTH H. MOLLEL: Kabisa ili haki iweze kutendeka….

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ruth Mollel kuna taarifa, Mheshimiwa Mchengerwa.

T A A R I F A

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi siipokei hiyo taarifa, naomba aende Segerea, aende Keko akaangalie halafu aje na data hapa. Watu wanakaa mpaka miaka mine, miaka sita upelelezi unaendelea, hiyo siyo sahihi, hata mbele ya Mungu si sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hizi kesi zingine ambazo pia zinakalisha sana watu Magerezani, ni hizi kesi za utakatishaji fedha. Nashauri Serikali ya Awamu ya Tano iangalie tena hii sheria kwa sababu watu wabaya wanaweza kutumia huu mwanya kubambikizia watu kesi za utakatishaji pesa kwa makusudi, kusudi waweze kuendelea kukaa upelelezi unaendelea miaka na miaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo liweze kuangaliwa na kufanyiwa kazi, tukienda kwenye suala hili maana yake tunasema kwamba kama ikiwa watu wanakaa muda mrefu, kesi zao hazisikilizwi, upelelezi unaendelea, tunasema justice delayed is justice denied. Kwa hiyo mtu hajapewa nafasi ya kusikilizwa na saa nyingine anaachiwa hata kufidiwa hafidiwi, anakuwa amepoteza miaka yake jela, mahabusu, amepoteza watoto, amepoteza mke na kila kitu. Kwa hiyo hilo lifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakuja pia kwenye suala la economic diplomacy. Kwa trend ya hivi karibuni hata kwa miaka mingi Ubalozi inakuwa kama ni zawadi au ni adhabu unasukumwa ukakae huko usionekane. Inabidi sasa kubadilisha huu utaratibu kusudi Ubalozi uwe ni shughuli ambayo mtu anakwenda kuifanya na waweze kupata elimu either trade au marketing au uwezeshaji kusudi wanapokwenda kule kwenye zile Balozi waende na utaalam ambao watakwenda kuutumia kutafuta miradi, fursa na mitaji kwa ajili ya kuiendeleza nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi tumesikia Dokta mmoja anapelekwa Cuba, huyu ni mtaalam mzuri sana nafikiri wa anesthesia anajua economic diplomacy ni kitu gani? Atakwenda kufanya nini kule? Kwa hiyo, inabidi watu wapate elimu waweze kujua wanapokwenda kule siyo kugonganisha glass za wine, ni kutafuta fursa, fedha na mitaji kwa ajili ya nchi hii. (Makofi)

MHE. DKT. SUSAN A. KOLIMBA: Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ruth Mollel, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Susan Kolimba.

T A A R I F A

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge kwamba mimi ni Katibu Mkuu Mstaafu wa Utumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee. Pia katika kupeleka Mabalozi nje ya nchi kuwepo na vigezo vya kuweza kupima utendaji wao wa kazi na upimaji wao utakuwa ni kuweza kuleta mitaji, fursa za biashara na wale ambao wanashindwa warudishwe…

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napendekeza katika ku-strengthen hii carrier ya diplomats katika mambo ya economic diplomacy hata mitaala ya Chuo Kikuu ya Political Science na International Relations iingizwe watu waweze kutoka kule wakijua kwamba sasa tunakwenda kuingia kwenye uchumi wa nchi na kuboresha maendeleo ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zamani kulikuwa na Siku ya Mabalozi ambayo sidhani kama siku hizi ipo. Siku hii ilikuwa muhimu ambapo Mabalozi walikuwa wanakutana na kubadilishana uzoefu na kusaidia katika kutafuta mitaji kwa ajili ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hili suala pia la Diaspora, tukubali kwamba tunao Watanzania wengi sana ambao wako nje ya nchi wanafanya kazi kule. Kulikuwa na ajenda ya kutengeneza kanzidata ya Diaspora, napenda Waziri atakapokuja kuzungumza hapa atuambie kwa mfano kule Diaspora tuna Watanzania wangapi. Kwa nini nasema hivyo?

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Taarifa.

MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu ni muhimu kwa ajili ya kuona ni jinsi gani ya kuwawezesha kuleta mitaji na pesa nyumbani ili kuongeza nguvu ya uchumi na kupunguza umasikini nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiangalia katika nchi zingine, kwa mfano, kwa mujibu wa statistics za Benki ya Dunia, kwa mwaka Kenya wanaingiza 2 billion USD kwa mwaka kutoka Diaspora; Uganda wanaingiza 1.2 billion USD; Somalia wanaingiza 1.4 billion USD; Nigeria wanaingiza 21 billion USD, Tanzania tunaingiza ni milioni 456 USD. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)