Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Ally Mohamed Keissy

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nichangie hizi Kamati zote mbili na naziunga mkono. Kwanza kabisa mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt. John Joseph Magufuli kwa uwezo na ujasiri wa kufanya bwawa la Rufiji kwa ajili ya umeme. Ni ajabu kabisa Wabunge wote wakikaa wanadai umeme kwenye vijiji vyao, wadai maji kwenye vijiji vyao, maji huwezi kupata bila umeme, hakuna chochote kinachofanyika kwenye kijiji chako bila umeme, wanadai REA awamu ya tatu kwamba wanataka vijijini umeme, vitongojini umeme, sasa bila ujasiri wa Rais Magufuli kupata umeme, nyie mtapata umeme?

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Ethiopia wanachanga pesa wanakata mishahara kwa ajili ya kujenga bwawa kubwa wapate umeme. Nyie Wabunge tukisema tuanze kuchanga pesa mtaanza kuruka ruka. Nchi nzima Ethiopia na umaskini wao wanachanga pesa kujenga bwawa kubwa la umeme, je, tukiamua watu hapa tuanze kuchangia bwawa la Rufiji kule mtakubali nyie?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais anakubali kutoa fedha kujenga bwawa la umeme tupate umeme nchi nzima mpaka vijiji vyenu, leo mnakaa mnapiga kelele, mazingira, Marekani ndio baba wa Taifa kwa viwanda, anakataka kutia mkataba kwa ajili ya mazingira, mbona hamumchukulii hatua? Mnapiga kelele, Mheshimiwa Zitto, Kigoma hakuna grid ya Taifa kama kwangu Nkasi, tuache kelele tupate grid ya Taifa katika vijiji vyote. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Rukwa unaitia hasara TANESCO umeme hautoshi mnatumia majenereta na mnachafua mazingia moshi kule kwenu. Ndugu zangu lazima tumtie nguvu Rais ajenge bwawa, kelele za hawa jamaa…

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Mollel, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa hiyo mimi nawafahamu. Ukiona mti wako hauzai, ujue ni hatari kata panda mwingine, sasa ndugu zangu hawa wanapungua siku hadi siku, Madiwani wamepungua, Wabunge wanapungua mpaka ifike 2020 hali ni ngumu, tumuache Rais afanye kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachangia habari ya mkataba wa SONGAS na Serikali yetu. Hapo fungueni masikio vizuri sana, hapo tuelewane huu mkataba, ujasiri wa Rais auvunje, hatuweeze kwenda nao mpaka 2024, tutakufa. Huu mkataba ni adui mkubwa wa nchi hii, ni wizi wa hali ya juu na namwomba Rais walioshiriki wote Mkataba huu wakamatwe mara moja kuanzia sasa. Mkataba huu Serikali yetu ilichangia 73% dola bilioni 285 milioni, hawa jamaa wa SONGAS walichangia dola 106.3 milioni, sawa na 27%, bado haikutosha, hizi pesa sio zao, Serikali yetu ilikwenda World Bank kukopa na kuwapa. Badala ya wao watulipe sisi, lakini sisi ndio tunawalipa wao, jamani ndugu zangu ni hatari kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, cha ajabu kiningine kibaya katika Shareholder wakati sisi tuna 73% wenyewe 27% sisi tukapata 46% wenyewe 54%, ndugu zangu! Kingine cha ajabu, tukaingia mkataba nao kwa ajili ya kuweka capacity charge dola milioni tano kwa mwezi, sawa na shilingi kwa sasa 11, 475, 000,000 wakati sisi tuna 73% tunapunjwa kila mwezi capacity charge tunapunjwa 8,668,750,000.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ally Keissy kuna taarifa, Mheshimiwa Ally Keissy.

(Hapa Mheshimiwa Ally K. Mohamed aliendelea kuzungumza bila kutumia kipaza sauti)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ally Keissy microphone yako ilikuwa imezima kwa hiyo yatakuwa hayajaingia hayo uliyosoma baada ya kipaza sauti kuzimwa. Mheshimiwa Kubenea taarifa na Mheshimiwa Ally Keissy itabidili hayo uliyokuwa unasema urudie ili yaingie kwenye Hansard.

T A A R I F A

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, naona Mheshimiwa Kubenea hanielewi, mikataba mibovu tunazungumzia yote na wewe mwenyewe labda ulikuwa chama mtumishi wa Vyama vya Upinzani.

Mheshimiwa Naibu Spika, narudia haikuingia kwenye Hansard, nyamazeni.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Musukuma muache Mheshimiwa Keissy achangie kidogo ndiyo unaweza ukasimama kwenye taarifa, la sivyo utakuwa unampa Mheshimiwa Kubenea. Mheshimiwa Ally Keissy.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, labda niongee taratibu, nazungumzia mkataba wa SONGAS na Serikali. Huu mkataba ni ufisadi wa hali ya juu, namuomba Rais anisikilize na waliopo wakamwambie mkataba huu haufai kuanzia leo waufute. Huu mkataba Serikali ilichangia dola 285.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ally Keissy kuna taarifa nyingine huko.

T A A R I F A

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa ya Mheshimiwa Musukuma moja kwa moja. (Makofi)

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea. Hawa Songas capacity charge wakati sisi TPDC tumechangia asilimia 73 wanachukua 100% capacity charge wakati sisi tungepata asilimia 73 capacity charge na wenyewe wangepata asilimia 27. Wakati huo huo mitambo ikiharibika gharama ya kutengeneza mitambo yote ni juu ya TANESCO. Mpaka sasa TANESCO wameshagharamia matengenezo ya mitambo shilingi bilioni 3.22 pamoja na VAT shilingi bilioni 90 wakati wale Songas wamekaa starehe huko kwao wanakula tu zile capacity charge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi hao Songas na PanAfrica; PanAfrica wenyewe wamekaa katikati hata kodi hawalipi. Tangu Awamu ya Nne tumesema sisi hapa Bungeni kuhusu PanAfrica kulipa kodi, kodi walikuwa hawalipi, wanachukua net pesa vizuri kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukichunguza mikataba TANESCO haiwezi kupata chochote na itaendelea kufifia. Songas amechukua baadhi ya Watanzania ambao walikuwa madarakani TPDC na kuingia mikataba hii mibovu, ndiyo Wakurugenzi wake. Baadhi ya viongozi wa Serikali waliokuwa Wakuu wa Mikoa ndiyo washauri wake. Juzi walikuja kwenye Kamati niliwahoji ninyi kweli ni wazalendo? Mzungu alibadilika rangi. Nikawauliza ninyi ni wazalendo kuangamiza nchi namna hii? Mpaka tarehe ya leo wametudhulumu shilingi trilioni 1.3 73 ya asilimia zetu 73.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ndugu zangu tunakalia kudai watu nyanya sokoni kule ushuru na mambo madogo madogo wakati hela zinakwenda kuliwa na Wazungu. Nilimwambia yule Mzungu kama Tanzania kwa wajanja mnaifanyia hivi, je, DRC Congo kule? Belgium imekaa inanyonya DRC Congo inakuwa tajiri mpaka watupe masharti ya ajabu ajabu tuoane ndiyo watupatie pesa wakati hawana chochote si lolote, wananyonya nchi za Kiafrika mchana kweupe tena ni Mabeberu wana ndevu ndefu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kuhusu mambo ya nje, tuelekeze nguvu zetu DRC Congo, tuweke jicho letu DRC Congo. Congo ni nchi ambayo imekaa kitajiri kuliko nchi zote za Afrika Mashariki. Tuienzi DRC Congo tupeleke macho yetu DRC Congo. Tunakaa chini ya ua la waridi, Congo itatusaidia sana kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapitwa na nchi kama Rwanda inayoegamia Congo leo inasifika dunia nzima kwa kupora Congo. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

WABUNGE FULANI: Aaaaa.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, jicho letu tupeleke Congo. Nashangaa wanasema wameshindwa kupeleka mahindi kule kupitia Zambia wakati Lake Tanganyika kuna barabara ya kutosha kwenda DRC Congo kupitia Ziwa Tanganyika. Ndugu zangu tubadilike, tuwe na wachumi na wafanyabiashara katika Serikali yetu.

MBUNGE FULANI: Kabisa.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Tuondokane na mambo ya ajabu ajabu haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashangaa kitu kimoja, Rais Magufuli aliwaita Wachungaji, Mashekhe na Maaskofu badala ya kuzungumza mambo ya maana akatokea jamaa mmoja akamwambia wewe mzee wakikushauri kuongeza muda usikubali, alitumwa na nani? Ukienda kila sehemu wanataka Rais Magufuli bila Rais Magufuli ndugu zangu nchi ilikuwa imeoza, tukubaliane kabisa nchi ilikuwa imeoza. Wabunge wanasafiri kama wakimbizi kwenda nchi za nje na impact hakuna leo, Rais kawabana wanabaki wanatapatapa wanahangaika. Hilo wazo alimtuma nani kwenda kumwambia Rais kwamba asiongeze muda, mlimtuma nyie. Wenyewe Wachungaji, Maaskofu na Mashekhe wana muda wa kuongoza, Shekhe ni mpaka achanganyikiwe akili au afe.

MHE. GODBLESS J. LEMA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Keissy, kuna taarifa.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Haya, nipe taarifa nikujibu. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Lema.

T A A R I F A

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimesema lilikuwa limeoza siyo sasa limeoza, hiyo taarifa sipokei, napokea nusu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia habari ya TANESCO, mpaka leo TANESCO inadaiwa zaidi ya bilioni 600 na hao jamaa wa Songas. Songas wanawauzia umeme TANESCO senti sita, TANESCO wanauza senti 11, tukamuuliza anasema eti mimi nauza bei ya chini sana, wewe unauza huna gharama kama TANESCO. TANESCO wanagharamia kusambaza umeme nchi nzima wewe Songas una gharama gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, nashangaa tunawaogopa vipi hawa Songas, tunawaogopa nini hawa PanAfrica? Lazima tuongoze kijasiri ili kujikomboa, tunaibiwaje shilingi trilioni 1.3 halafu tunaenda kuwaomba tena hela Wazungu? Hicho ni kitu cha ajabu mpaka Rais wa Marekani na mke wake wakaenda kutembea pale Ubungo, hamkusikia au mlisikia? [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

WABUNGE FULANI: Tulisikia.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Ni kwa sababu ya maslahi yake. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujasiri Rais Magufuli namwomba anisikilize aingilie upya mikataba hii ya Songas, asilale usingizi, awatafute wote waliotia saini kwanza awalundike magereza mara moja. Kama walipata mali kwa njia ya rushwa kuingia mikataba ya namna hii, mali zao zitaifishwe mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lililopita nilizungumza mara nyingi watu kama hawa ndugu zangu wanaoingia mikataba mibovu dawa yao ni kuwanyonga. Leo ukiwanyonga watu 200 Muhimbili wanazaliwa 500 kuna hasara gani? (Kicheko)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)