Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Ali Salim Khamis

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mwanakwerekwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa nami ya kuweza kuchangia mawili/ matatu. Nataka nijielekeze zaidi katika masuala haya ya mafuta na gesi. Ripoti ya Kamati imeelezea wazi juu ya matatizo ya kisheria ambayo yanalikabili Taifa katika masuala ya miradi hii ya gesi ya SONGAS. Pia tatizo hilo hilo lipo katika suala baina ya Zanzibar na Bara kuna tatizo kama hilo ambalo liko katika mikataba hiyo ya SONGAS.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano, nyongeza ya kwanza, suala la mafuta na gesi ni suala la Muungano na kwenye Ibara ya 34 inaeleza wazi na Ibara ya 64 pia nayo inaeleza jinsi ya masuala ya mafuta na gesi ambayo ni mambo ya Muungano. Kama hiyo haitoshi mwaka 2015, Bunge hili lilipitisha Sheria ya Mafuta kuonesha kwamba nani hasa anastahiki kusimamia mafuta na gesi katika Tanzania. Sasa kilichojitokeza kwanza mwaka 2009 Baraza la Wawakilishi liliazimia kwamba suala la mafuta litolewe katika mambo ya Muungano, kwa sababu suala hili liliingizwa katika masuala ya Muungano mwaka 1968 katika Katiba ya muda ambayo kimsingi liliingizwa bila ridhaa ya Wazanzibari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiendelea Zanzibar sasa hivi imetunga sheria yake, Sheria Na.6 ambayo inasema kwamba mafuta ni mali ya Zanzibar na Zanzibar wao ndio wenye mamlaka ya kuchimba mafuta na Katiba ya Zanzibar iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010 imeeleza wazi mipaka ya Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiangalia katika sheria hii ya mwaka 2015 Kifungu cha 47, kimeleta marekebisho kumpa mamlaka Waziri wa Nishati wa Bara kwamba ndiye ambaye atatoa maelekezo jinsi masuala yote mazima ya mafuta. Pia Zanzibar nao katika sheria mpya ambayo imetungwa ya mwaka 2016, Sheria Na. 6 nayo vile vile imempa mamlaka Waziri wa Nishati wa Zanzibar kusimamia masuala ya mafuta. Sasa niombe kutokana na mkanganyiko huu wa kisheria na kikatiba nafikiri sasa ni wakati muafaka kuleta mjadala wa katiba ili suala hili la mafuta Zanzibar washughulike na masuala yao ya mafuta na Bara na wao washughulike na masuala yao ya mafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika,Leo ukiangalia masuala haya mafuta huko mbeleni yataleta mgogora sana. Matatizo haya haya ndio matatizo ambayo yanaikabili miradi hii mikubwa ya gesi sasa hivi, ukiangalia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haipati kitu katika suala zima la masuala ya gesi. Ndio maana leo kila mtu analizungumzia hapa kwamba mikataba ina shida, kwa hiyo sasa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Bunge hili imetengeneza sheria kama zile ambazo wametengenezewa wao na SONGAS…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele imeshagonga.

MHE. ALI SALIM KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeandika kwa maandishi pia mchango wangu.