Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manonga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika majadiliano haya. Kwanza nipende kutumia nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anazozifanya katika taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri sana, naamini Watanzania walio wengi wanaona; na katika kazi hizi Mheshimiwa Rais lengo lake ni kupunguza matatizo ambayo yalikuwepo ambayo yalikuwa yakileta changamoto mbalimbali katika sekta ya madini na sekta mbalimbali ambazo ziko ndani ya nchi yetu. Juzi tumeona amekutana na wadau wa madini nchini, amejadiliana nao na ameona changamoto ambazo zipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweza kuona hata baadhi ya wadau ambao wameweza kuchangia wameweza kuchangia, wameweza kuionesha Serikali sehemu ambazo kuna mianya inavyopoteza mapato katika nchi yetu. Hata kule Tanga wameweza kuzungumza habari ya maeneo yenye migodi ambayo watu wanaitumia migodi ile kwa ajili ya kujinufaisha binafsi. Vilevile pia wameonesha namna gani ambavyo baadhi ya watumishi wetu katika Serikali hawawajibiki ipasavyo. Kwa hiyo mimi binafsi nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazozifanya na hatuna sababu ya kuacha kumpongeza kwa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine ambalo ningependa kuzungumzia; ni kuzipongeza Wizara za Nishati na Madini, kazi kubwa sana wanazifanya pia. Tumeweza kuona hata Wizara hii ya Nishati kupitia Mheshimiwa Medard Kalemani pamoja na Mheshimiwa Subira Mgalu, wanapambana sana ili kuhakikisha kwamba vijiji vyetu vinapata umeme. Katika maeneo yetu, tumeona wakitembelea vijiji. Mimi binafsi kwa kweli nisiseme uongo, wamekuja mpaka jimboni kwangu mara mbili, mara tatu. Hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri na kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, hata Kamati ilifika maeneo ya vijiji vyetu na baadhi ya vijiji vimeanza kupata umeme katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo zipo jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha kwamba vijiji vyetu vinapata umeme. Zipo changamoto ambazo zimezungumzwa hapa. Katika utekelezaji wa miradi ya aina yoyote changamoto huwa hazikosekani, tuangalie namna gani ya kuweza kutatua hizi changamoto zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya hizo changamoto lakini miradi inatekelezwa vizuri na mambo yanakwenda, hata kama zipo lakini ni ambazo zinaweza kuzungumzika na kuweza kutekelezeka. Kwa mfano, niishauri tu Serikali, kwamba itoe fedha kwenye Wizara hii ya Nishati ili iweze kutimiza kazi zake kwa wakati. Wanapotoa fedha hizi zitakwenda kulipwa hawa wakandarasi ambao wanatekeleza miradi hiyo, wakandarasi wataweza kupata fedha ambazo zitawasaidia kununua vifaa ambavyo vitakuja katika utekelezaji wa umeme vijijini. Jitihada kubwa zinafanyika, lakini niiombe Serikali iweze kuongeza fedha katika miradi mbalimbali inayotekelezwa ikiwa chini ya Wizara hii ya Nishati. Kwa hiyo hilo nilikuwa napenda kulizungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Serikali ipeleke fedha katika taasisi zake, kwa mfano TANESCO, TPDC, STAMICO, wawape fedha ili waweze kuhakikisha kwamba yale malengo waliyokuwa wemejiwekea waweze kuyatekeleza kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo naliona, Serikali iangalie namna ya kuongeza rasilimali watu. Rasilimali watu imekuwa ni changamoto sana katika taasisi mbalimbali za Serikali na hii inasababisha kupunguza uwezo wa Serikali kukusanya mapato kwa wakati. Tunaweza kuona katika sekta za madini, gesi pamoja na mafuta. Kwa hiyo niiombe Serikali iweze kuongeza rasilimali watu ili waweze kuhakikisha kwamba majukumu ambayo Serikali imejiwekea yaweze kutimizwa kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ambacho ningependa kuchangia ni katika suala zima ambalo Kamati imezungumzia; masuala ya flow metres. Tunaweza kuona flow metres zetu katika maeneo yetu ya bandari. Kuna bandari ya Mtwara, bandari ya Tanga, lakini kuna Bandari hazina flow metres. Kwa hiyo, tunaweza kuona kwamba tunapata mafuta ambayo hayapo katika utaratibu mzuri wa mahesabu. Kwa hiyo tunapofunga flow metres zetu inatusaidia kuweza kupata exactly figure ambayo itatusaidia kupata mapato katika Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niiombe Wizara na pia Serikali ihakikishe kwamba inafunga flow meters katika maeneo ambayo yana uhitaji hasa kwa sababu ni faida kwa Taifa letu. Kwa hiyo walichukulie kama sehemu ya mojawapo ya kudhibiti kuingizwa kwa mafuta pasipo kupata data kwa sababu wanaweza kuchakachua taarifa ambazo zinakuwa zimeandikwa japo zinaandikwa na watumishi wetu. Sasa tukipata flow meters zitatusaidia kurekodi na kupata amount sahihi ya mafuta yanayoingia na vile vile itatusaidia kupata kipato, ambacho nchi inahitaji kukipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo…(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa, muda wako umekwisha. Mheshimiwa Hussein Amar atafuatiwa na Mheshimiwa Joram Hongoli na Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani ajiandae.
MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)