Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia katika mada muhimu ya Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze pia kuwapongeza sana Kamati ya Kudumu kwa mapendekezo waliyoyatoa. Sisi kama Serikali tumeyachukua tutayafanyia kazi na kufanya maboresho zaidi. Kwa hiyo, napenda sana kumshukuru Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawapongeze sana Waheshimiwa Wabunge, wametoa michango mizuri, mingi na yenye ushauri. Bado naendelea kusema, kama Serikali, tutaichambua tutaifanyia kazi na kufanya maboresho ambapo lazima pafanyike maboresho.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nami basi niseme machache kuhusiana na ajenda ya leo. Kuhusiana na mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa megawatt 2,115, bila shaka Watanzania wote tunashuhudia, ni mara ya kwanza Tanzania kuingia kwenye ulingo wa kidunia kuwa na miradi mikubwa ya kuzalisha umeme. Kwa hiyo, tuipongeze sana Serikali yetu kupitia kwa Mheshimiwa Rais kwa kutekeleza mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwakumbushe tu Watanzania na wananchi kupitia Waheshimiwa Wabunge; miradi mikubwa duniani inahesabika mnapokuwa na mradi wa kuzalisha umeme wa kuanzia megawatt 2,000. Kwa hiyo, ndiyo maana tumeingia katika miradi mikubwa 70 duniani, nasi ni wa 60 duniani. Kwa hiyo, napenda tuwapigie makofi Watanzania wote walioshiriki katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi, hata Kiafrika tulikuwa hatusomeki kwenye miradi mikubwa ya kuzalisha umeme. Leo tunaongelea Stiegler’s yenye uwezo wa kuzalisha Megawatt 2,115, ni mradi wa nne Afrika kwa ukubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri sana Wakandarasi ambao wanatekeleza mradi huu ambao ni Arab Contractor kutoka Egypt pamoja na El Sewedy wanatoka katika nchi ambazo zipo katika nchi tano za kuzalisha umeme mkubwa duniani. Walioshiriki sana kwenye kuzalisha umeme wa Aswan Dam wa Megawatt 2,100 kule Egypt. Kwa hiyo, hatuna mashaka na Wakandarasi na hatuna mashaka na maamuzi ya Kiserikali yaliyofanyika. Ni matumaini yetu mradi utatekelezeka vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuwaambia Watanzania kwamba utekelezaji wa mradi huu ndiyo unaanza. Tumesaini mikataba mwezi uliopita, kwa hiyo, hatutarajii Mkandarasi kuwa amelipwa hela nyingi kwa sasa kwa sababu ndiyo kazi zinaanza. Kwa hiyo, ni matumaini yetu tunakokwenda tutamlipa Mkandarasi kulingana na kazi zinavyofanyika. Ndiyo maana kwenye taarifa umeona shilingi bilioni 26 tu kati ya shilingi bilioni 700 za utekelezaji wa kazi hii. Kwa hiyo, ni matumaini yetu, wala hatuna mashaka na wenzetu wa Hazina wataendelea kulipa vizuri kadri utekelezaji wa mradi utakavyoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kutaja umuhimu wa mradi huu. Pamoja na kutekeleza miradi mchanganyiko ya kuzalisha umeme, kama ambavyo tunaendelea kuzalisha umeme wa megawatt 300 ambao tumeanza kuutekeleza sasa kule Mtwara kupitia JICA, wenye uwekezaji wa takribani Dola za Marekani milioni 395 ambao ni megawatt 300, mradi huu tunaanza kuutekeleza kuanzia Julai mwaka huu na utakamilika Juni, 2022 ambao utatuzalishia megawatt 300 za gesi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo kweli kwamba tumeacha miradi mingine ya kuzalisha umeme. Umeme huo tutausafirisha kwenye gridi ya Taifa kutoka Mtwara, umbali wa kilometa 512 kwa kuingizwa kwenye rridi yetu ya Taifa. Bado tunatekeleza Mradi wa Kinyerezi na mingine. Hii inaonesha kwamba Watanzania tunaamua kwenda na umeme mchanganyiko. Kwa hiyo, kutekeleza Mradi wa Stiegler’s hakuna maana kwamba tunaondoa utekelezaji wa miradi mingine ya kuzalisha umeme. Naomba Watanzania tuendelee kuunga mkono, tushirikiane mradi utekelezeke ili tuondokane na changamoto ya umeme hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, ni kweli kabisa leo tunapoongea hapa, tuna umeme wa ziada megawatt 278, matumizi yetu ya leo ni megawatt 979, lakini haina maana kwamba hatuhitaji kuendelea kuzalisha umeme. Unatutosha leo, lakini kwa kesho haututoshi. Kwa hiyo, hatuna budi kuzalisha umeme mkubwa ili kujihakikishia ujenzi wa uchumi wa viwanda hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu miradi ya REA, kwanza kabisa, napenda naomba niwapongeze Waheshimiwa Wabunge, mnatuunga mkono sana kwenye miradi hii. Tunapokwenda kwenye miradi yenu, huko kwenye Majimbo yenu mnatupa ushirikiano mkubwa. Nitoe rai tu kwa Wakandarasi kwa sababu limesemwa hapa, kwamba utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini ni mradi shirikishi. Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuagiza Wakandarasi kwamba popote walipo wasiingie kwenye maeneo ya Wabunge bila kuwashirikisha Wabunge au uongozi ulioko kule ili utekelezaji uwe na tija zaidi. (Makofi)

Leo tunapoongea, tunapeleka umeme vijiji takribani 6,212. Mwaka 2015 tulipeleka umeme vijiji 1,927 tu, kwa hiyo, ni zaidi ya asilimia 300 kwa miaka hii mitatu tumetekeleza mradi huu wa kupeleka umeme vijijini. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge, mwendelee kutuunga mkono ili tufanye kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Heche alivyosema; juzi tu alituomba tumpelekee umeme Susuni, tukapeleka; tumepeleka Kerenge, tumepeleka Nyamwaga, Nyanungu na Nyurito. Ndugu yangu Mheshimiwa Heche anataka nini? (Makofi)

MHE. JOHN W. HECHE: Taarifa.

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza miradi kwa ufanisi sana.

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpe taarifa Mheshimiwa Heche na Wabunge wengine, mradi huu ni wa miaka minne iliyobaki, mwaka…

MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.


NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, muda wetu umekwenda sana, kwa hiyo, sitaruhusu taarifa kwa sasa. Mheshimiwa Dkt. Kalemani endelea.

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Niwape tu taarifa Waheshimiwa Wabunge, tunachukua michango ambayo wamesema kuhusiana na utekelezaji wa miradi hii, lakini tumejipanga vizuri kwa upande wa vifaa, sasa hivi Wakandarasi wameshaanza kupeleka vifaa site. Ni matumaini yetu kuanzia mwezi ujao speed itaongezeka zaidi ili kufikisha umeme kwenye vijiji ambavyo tumepanga kuvitekeleza kwenye mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la mikataba ya Songas; kwanza nikupongeze kupitia Kiti chako kwamba mwaka 2018 kupitia kwa Mheshimiwa Spika wakati ule, Waheshimiwa Wabunge waliunda Kamati Maalum ya kupitia mikataba hii ya kuzalisha gesi, mafuta pamoja na biashara. Kwenye mapendekezo ya Kamati, ilipendekezwa mikataba yote ipitiwe upya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni sikivu sana, imeanza kupitia upya mikataba yote ukiwemo Mkataba wa Songas. Kwa hiyo, suala la kwamba mkataba ufutwe, urekebishwe ufanyiwe maboresho, itatokana na mapendekezo ya Kamati ambayo sasa marekebisho na mapitio ya mikataba hiyo yanafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yetu matokeo ya kupitia mikataba yatakuja na mapendekezo ya kuboresha ambayo nia ya Watanzania ni kuhakikisha kwamba stahili ya Watanzania kwenye mikataba hii inapatikana. Kwa hiyo, niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba kwa vile mikataba inapitiwa kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ni matumaini yetu mapitio hayo yataboresha zaidi, siyo kwa upande wa mkataba wa Songas tu, lakini mikataba yote ya kuzalisha gesi pamoja na utafiti wa gesi na mafuta hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kusema kuhusiana na Mradi wa Kinyerezi. Tunayo miradi mingi sana. Mradi wa Kinyerezi wa megawatt 185 hivi karibuni utakamilika. Bomba la gesi ambalo Waheshimiwa Wabunge wanataja, ni kweli kabisa huwezi kuona mahitaji makubwa ya gesi kwa sasa kwa sababu viwanda vingi vya gesi vitaendelea kujengwa. Tutakuwa na mradi wa Kinyerezi Na. 1 unaoendelea extension, tutakuwa na Kinyerezi No. 3 wa megawatt 600 pamoja na Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mahitaji na matumizi ya gesi yataongezeka zaidi. Kwa hiyo, uamuzi wa Serikali walivyofanya kujenga bomba kubwa ambalo leo tunaona matumizi yake ni madogo, siyo vibaya kwa sababu tuna miaka mingi, zaidi ya 100, kuendelea kutumia bomba hili. Kwa hiyo, kutumia asilimia ndogo wala isiwatishe, tutaendelea kutumia kwa sababu miradi mikubwa itaendelea kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa LNG ni kati ya miradi mikubwa sana duniani. Mradi huu mnatambua kwamba uwekezaji wake siyo chini ya Dola za Marekani bilioni 35. Hata hivyo, Serikali imeanza kuutekeleza mradi huu. Tunaposema ujenzi wa uchumi wa viwanda, ndiyo viwanda vya LNG tunavyozungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge na nitoe taarifa; mradi huu haujakwama na hautakwama na tumeanza kuutekeleza. Kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wamesema, tumeanza majadiliano na mmoja mmoja, tumeanza na Equinor, lakini wadau wote ambao wanashiriki kwenye kuzalisha, tunajadiliana nao na sasa tunaongeza kasi ili maeneo ambayo yameshapitiwa, yakamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge wa eneo anakotoka kule Likong’o kwamba tathmini ya fidia ya wananchi imeshafanywa na imeshakamilika. Kinachofanyika sasa hivi ni kufanya uhakiki. Taratibu za uhakiki zikikamilika, wananchi watalipwa fidia na mradi utaendelea kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana kusema mengi katika miradi hii, lakini jambo la msingi pia ni umeme wa gridi Kigoma pamoja na Katavi. Katika mradi huu tunatekeleza miradi mikubwa miwili; wa kwanza, ni mradi wa kutoka Iringa, Sumbawanga, Mpanda, Kigoma hadi Nyakanazi ambao umeanza kutekelezwa kwa portion ya kuanzia Iringa mpaka Sumbawanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hatua za haraka ili tuwapelekee umeme wa gridi wananchi wa Kigoma pamoja na Katavi, Serikali kuanzia Desemba mwaka 2018 tumeanza kutekeleza mradi wa kusafirisha umeme wa kilovoti 132, umbali wa kilometa 391 kutoka Tabora, Urambo mpaka Kidahwe, Kigoma. Mradi huu tumeshatenga fedha, Dola za Marekani bilioni 81. Mradi utatekelezwa kama tulivyosema na utakamilika Februari, 2020. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, Katavi…

NAIBU SPIKA: Muda umekwisha Mheshimiwa Dkt. Kalemani. Ahsante sana.

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)