Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mungu kwa nafasi hii na nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa imani aliyonipatia na kuniteua kuwa Waziri wa Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile namshukuru sana mtangulizi wangu, Mheshimiwa Angellah Kairuki ambaye amekuwa Mwalimu wangu mzuri sana kwenye nafasi hii. Wakati nikihudumu kama Naibu Waziri wa Madini, amekuwa Mwalimu mwema, aliyenifundisha, aliyeni-expose kwa kweli kwa kila namna ya kujifunza namna ya kusimamia Sekta ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru vile vile Mheshimiwa Nyongo ambaye pia ni Naibu Waziri kwa ushirikiano mkubwa ambao walinipatia wakati nikiwa Naibu Waziri mwenzake na hata sasa ambapo tunaendelea kushirikiana pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo ya utangulizi, kama walivyoanza wengine, nami naomba nimpongeze sana Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Nishati na Madini, Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula na Makamu wake, Mheshimiwa Mariam Ditopile pamoja na Wajumbe wote wa Kamati kwa kazi kubwa wanayoifanya na kwa maelekezo ambayo kwa kweli wanatupa kila wakati tunapokutana nao kwenye vikao vya Kamati na kwenye mashauriano mbalimbali wanapoona kuna mambo yanayohitaji kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba, binafsi naona fahari kubwa kufanya kazi pamoja na Kamati hii kwa sababu ya umakini wao na ubunifu wao, lakini vilevile kujali kwao na kufuatilia mambo mbalimbali ambayo yako kwenye Sekta ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijasahau nami niseme naunga mkono hoja iliyoletwa hapa na Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini. Nami nitoe mchango mdogo tu kwenye mambo mbalimbali ambayo yamezungumzwa kwenye taarifa lakini vilevile na Waheshimiwa Wabunge mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, itashangaza sana kama nitasema hakuna changamoto kwenye Sekta ya Madini. Changamoto zipo na hazikuwepo leo, zimekuwepo kwa muda mrefu. Ninyi mnafahamu kwamba hapa Afrika Sekta ya Uvunaji wa Madini sisi tumeanza miaka ya 1990 kwa kuleta mitaji mikubwa kutoka nje. Huko nyuma waliokuwa wanachimba madini walikuwa wachimbaji wadogo. Ukianza mwaka 1987 mpaka mwaka 1997, miaka kumi ile wachimbaji wadogo peke yao ndio walikuwa wanachimba kwa asilimia 94, hapakuwa na mtaji wa mgeni hata mmoja, tulikuwa sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, walikuja wenye mitaji miaka hiyo ya 1990 na hapo sasa Sekta ya Madini ikawa ndilo jambo linalojadiliwa. Bunge hili linafahamu, kama kuna sekta ambayo imeundiwa Kamati nyingi mno ni Sekta ya Madini. Kamati za Ushauri za Bunge ziliundwa kwenye Sekta ya Madini, Kamati za uchunguzi ziliundwa kwenye Sekta ya Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, toka mwaka 2002 iliundwa Kamati ya Kipokola, mwaka 2004 ikaundwa Kamati ya Masha; mwaka 2006 ikaundwa; zimeundwa Kamati nyingi na hata Bunge hili na lenyewe limeunda Kamati mbalimbali. Nia ilikuwa moja tu, kuondoa changamoto zilizomo kwenye Sekta ya Madini; na Serikali imekuwa ikifanya hivyo hatua kwa hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunavyoendelea kufanya kazi ya kusimamia Sekta ya Madini, tunagundua changamoto zilizomo, tunatafuta mbinu za kuziondoa. Namna mojawapo ya kuondoa changamoto hizo, ipo kwenye sheria. Ndiyo maana mnaona Sheria ya Madini imekuwa ikibadilika miaka hadi miaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1998 ilibadilika, mwaka 2010 ilibadilika na baadaye 2017 tukafanya marekebisho makubwa sana ya mwelekeo wa Sheria yetu ya Madini. Nia ni kuleta tija kwa nchi kwenye Sekta hii ya Madini. Bado tunaendelea kukabiliana na hizo changamoto pamoja na kwamba tumeshapiga hatua kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikiliza michango ya Waheshimiwa Wabunge hapa na nianze kueleza mchango mdogo tu ambao umeelezwa na ndugu yangu, Mheshimiwa Frank Mwakajoka, sijui ni kwa nia njema au ni kwa sababu ya kunogesha, anasema Sekta ya Madini mchango wake umeshuka. Naomba niweke taarifa sahihi kwenye Bunge hili; mchango wa Sekta ya Madini kwenye nchi ya Tanzania toka tumeanza kuchimba haujawahi kushuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitampa rekodi kidogo hapa; mwaka 2013, Sekta ya Madini ilikuwa inachangia asilimia 3.3; mwaka 2014, Sekta ya Madini ilikuwa inachangia asilimia 3.7; mwaka 2015, ilichangia kwa asilimia 4.0; mwaka 2016, imechangia constantly na mwaka uliofuata 2017, kwa asilimia 4.8. Haijawahi kuchangia kwa asilimia tano na ikashuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukuaji wa Sekta yenyewe ya Madini ni ule ambao ni very promising. Mwaka 2013, ukuaji wa Sekta ya Madini ulikuwa asilimia 6.9; mwaka 2014, ukuaji wake ulikuwa asilimia 9.4; mwaka 2015, ulikuwa asilimia 9.1. Mwaka juzi, mwaka 2017, sekta iliyoongoza kwa ukuaji katika sekta zote sio mchango wa sekta, ni Sekta ya Madini, ilichangia kwa asilimia 17.5. Nadhani tusivunjane moyo, tutiane moyo, tuna safari kubwa ya kufanya. Kazi ya kudhibiti madini kutoroshwa sio kazi ya mtu mmoja, Wizara ya Madini, ni kazi ya Watanzania wote. Leo nataka niwaambie tunapokamata wanaotorosha madini hatukuti wageni peke yao, tunawakuta na Watanzania wenzetu wamo wakisaidia utoroshaji wa madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani Serikali iwe yenyewe peke yake bila Watanzania wenyewe kutengeneza mindset ya kuwa na wivu na rasilimali zao. Naomba nipaze sauti kwenye Bunge hili kuwaomba Watanzania; madini tuliyonayo kuna siku yataisha, lazima tuone wivu, tuyalinde kwa nguvu zote. Wanaokamatwa wote wawe wenyeji, wawe wageni, ukienda utakuta aliyetengeneza huo mchongo ni Mtanzania mwenzetu aliyekuwa anachimba nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda naomba nieleze vilevile, wameeleza hapa Waheshimiwa Wabunge kwamba sasa wachimbaji wadogo waanze kurasimishwa na wameeleza maoni waliyoyatoa kwenye mkutano tulioufanya, tukamwalika Mheshimiwa Rais, kwamba tuyasikilize. Naomba niwaondoe wasiwasi; mapendekezo yao yote yako 22, yote tunayafanyia kazi kama Serikali, yote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo waliyoyatoa yanayohusiana na sharia, Serikali inayafanyia kazi lakini yapo mengine ya kiutendaji kwa mfano kuwapatia maeneo ya kuchimba; baada ya wiki inayokuja nitatoa taarifa ya leseni ngapi tunazifuta kwa sababu tunazo leseni nyingi kwa kweli, zaidi ya 2,038, zimeshikiliwa na watu ambao hata humu nchini hawamo. Zinadaiwa fedha zaidi ya dola milioni 42, zimekalia maeneo wachimbaji wadogo wakienda kule wanafukuzwa, tunakwenda kuzifuta zote hizo tuwapatie wachimbaji wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo limeelezwa hapa juu ya TEITI, kwamba TEITI haijafanya kazi yake; naomba niweke rekodi sawasawa, ni kweli kwamba TEITI kazi inayofanya ni reconciliation kati ya kile kilichotolewa kwenye mgodi na kile kilichoingia Serikalini, hakuna fedha yoyote


iliyopotea. Kinachofanyika makampuni yanayoshughulika na Sekta ya Madini na Gesi, mafuta, ni makampuni 2,087. Wao wakatengeneza utaratibu wa kuyachambua baadhi kama sampuli, wakachukua yale yenye threshold ya mtaji wa milioni 300 ndiyo yakafika hayo 50. Sio kweli kwamba tulipaswa kukagua 2,000 sasa tumekomea 50, hapana, ni wale MCG waliamua wenyewe kuchambua kwamba tukague wale ambao wana mtaji mkubwa kuanzia dola milioni 300, ndiyo tukapata kiasi hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo fedha anayozungumza imepotea sio fedha iliyopotea, ni reconciliation, kwamba ukienda kwenye mgodi unakuta anakwambia nimelipa shilingi 10, ukija huku Serikalini unakuta pengine hiyo hela haijawa recorded au unakuja huku Serikali unakuta kuna fedha fulani haijawa recorded, ukienda kwenye mgodi unakuta hiyo fedha. Kwa hiyo, hiyo kazi unachukua hizo anomalies zote, unampelekea CAG ili aweze kuhakiki kujua kama kweli kuna fedha zimepotea, kwa hiyo hakuna pesa iliyoibiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati njema Mheshimiwa Mwakajoka ni Mjumbe kwenye Kamati, majibu haya tulimpatia kwenye Kamati, lakini kwa sababu ni lazima tunogeshe, ruhusa tunaendelea, lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mwakajoka; hakuna mtu ataiba fedha kwenye Sekta ya Madini akabaki salama, hakuna mtu atatorosha madini kwenye Sekta ya Madini atabaki salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, wachimbaji wamelalamikia kodi, wamelalamikia masoko. Nilikuwa na mkutano hapa juzi wa Wakuu wa Mikoa yote Tanzania, tumeshaanzisha maeneo na kuyatenga kwa ajili ya masoko ya madini. Hata ule utaratibu wa kusema mtu anayetaka kuleta madini hapa nje awe na mlolongo mrefu, mlolongo huo tumeuondoa, sasa watu wanaotoka Congo, Msumbiji, wale wanaotaka ku-trade madini yao ndani ya nchi, ruhusa, ilimradi waseme kwamba tunataka kuja kufanya biashara. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Doto Biteko, muda wako umekwisha.

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)