Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nichangie kwenye hoja iliyo mbele yetu kwa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Naipongeza Kamati, nawashukuru sana kwa ushirikiano wanaotupa mimi pamoja na watendaji wa Wizara yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye maoni na mapendekezo ya Kamati juu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Kulikuwa kuna hoja ya kukosekana kwa Sera ya Ulinzi wa Taifa nchini ambayo inaathiri ufanisi katika uratibu wa ulinzi wa Taifa, napenda niliarifu Bunge lako kwamba tatizo hili sasa limekwisha. Kwa muda mrefu tulikuwa hatuna hii sera kwa sababu hakukuwa na maoni ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Napenda niliarifu Bunge lako kwamba maoni hayo sasa yamepatikana, mchakato unaendelea ndani ya Wizara ili kuikamilisha sera hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kukosekana kwa alama za mipaka ya nchi (beacons) kunachangia uvamizi wa raia wa kigeni katika baadhi ya maeneo ya mipaka, jambo ambalo linaweza kuathiri ulinzi na usalama wa nchi. Nataka niwaeleze Waheshimiwa Wabunge kwamba na eneo hili nalo limeanza kufanyiwa kazi kwa nguvu kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mipaka yetu upande wa Kenya na upande wa Uganda tayari beacons zimeanza kurudishiwa, upande wa Kenya tayari tuna kilometa zipatazo 172 kati ya 760 ambazo tayari wameshaudishia beacons kuanzia kwenye Ukanda wa Ziwa Victoria kuelekeza Ziwa Natron. Kwa hiyo zoezi hili linaendelea na tumeanza upande wa Kenya na Uganda, tutaendelea katika maeneo mengine, lakini nia na madhumuni ni kurudisha beacons hizo ili kuwepo na uhakika wa kwamba mipaka kati yetu na nchi jirani inajulikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, madeni kwa mashirika yaliyo chini ya SUMA JKT yanaathiri shughuli za uzalishaji mali wa shirika; tunakubali kwamba Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) lina madeni mengi hususan ule mrdai wao wa matrekta. Nataka nitoe taarifa hapa kwamba toka Mheshimiwa Rais ametoa agizo la wale wote wanaodaiwa waweze kurudisha fedha zile, shirika limeweza kukusanya Sh. 2,900,000,000 na tunaendelea na mchakato huo na baada ya hapo kuna Kampuni maalum ya SUMA JKT ya auction ambayo itachukua hatua za kisheria dhidi ya wale wote ambao watakuwa wameshindwa kulipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kukosekana kwa uzio katika baadhi ya Kambi za Jeshi kunasababisha migogoro ya ardhi kutokana na wananchi kuvamia maeneo hayo; ni kweli kwamba maeneo mengi ya Jeshi hayana uzio na hayawezi kuwa na uzio kwa sababu ni maeneo makubwa
sana. Tunachokifanya sasa hivi ni kwamba kuna maagizo kwa kila Mkuu wa Kikosi kuhakikisha kwamba wanaweka alama katika borders zao na hususan yale maeneo makubwa sana, wapande miti na waweke mabango yanayoonesha kwamba haya ni maeneo ya Jeshi, nia na madhumuni ni kuhakikisha kwamba wananchi wanaelewa mipaka ilipo na hawaingiliwi katika maeneo hayo. Baadhi ya maeneo hayo ni ya mazoezi, kwa hiyo wananchi wakiingia huko wanaweza kupata athari kubwa kutokana na dhana zinazotumika katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja nyingine kwamba wananchi kutolipwa fidia katika maeneo yaliyotwaliwa kwa ajili ya matumizi ya Jeshi kumeendelea kusababisha migogoro ya ardhi kati ya wananchi na vikosi vya Jeshi. Hapa ni kama nilivyosema, migogoro ya ardhi kati ya wananchi na Jeshi ipo ya aina kadhaa; moja ni pale wananchi wanapovamia maeneo ambayo tuna uhakika ni ya Jeshi kwa sababu ya ufinyu wa ardhi ya kulima na kufuga, hao hakuna hoja, ni kuwaondoa tu kwa sababu lazima Jeshi libaki na maeneo yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini yapo maeneo yaliyotwaliwa kweli na wananchi hawa wanastahili fidia, tumeweka katika bajeti ya mwaka huu shilingi bilioni 20 na mpaka sasa hivi tumeshapokea karibu shilingi bilioni 3 ambazo tumeanza na kulipa eneo la Kilwa ambapo tunaweka base ya Navy. Kwa maana hiyo, kila fedha hizi zitakapoendelea kutolewa wananchi hawa wenye stahili za kulipwa fedha kwa sababu walihamishwa katika maeneo yao wataendelea kulipwa ili migogoro hiyo iishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa ni uchakavu wa majengo ya Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Monduli kunashusha hadhi ya chuo hicho kinachotoa mafunzo ya kimataifa. Tumekuwa na jitihada mbalimbali za kukiendeleza na kukiboresha chuo kwani ni cha muda mrefu na baadhi ya majengo yake yamechakaa. Nataka nieleze kwa mfano makazi, katika ule mradi wetu wa nyumba 6,064 pale Monduli wamepata nyumba hizo kwa ajili ya Askari na kuna baadhi ya majengo mapya yamejengwa mfano mzuri ni maktaba, kuna maktaba mpya pale lakini tunaendelea kukarabati Ofisi na maeneo mengine kwa awamu kadri bajeti inavyoruhusu. Tunaelewa kwamba chuo hiki sasa ni cha kimataifa kinachukua wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali ya SADC na East African Community kwa maana hiyo kuna kila sababu ya kukiboresha ili kiwe na hadhi inayostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo la kutotolewa kwa fedha za maendeleo kwa Shirika la Nyumbu na Mzinga kumeendelea kuathiri shughuli za kitafiti na ubunifu wa shirika hilo. Ni sahihi kwamba kwa kipindi kirefu Mashirika haya ya Nyumbu na Mzinga yamekuwa hayapati bajeti inayostahili na kwa maana hiyo kazi zao zimeendelea kupungua. Nataka nilieleze Bunge lako Tukufu kwamba tayari kuna mpango mkakati maalum kwa mashirika yote mawili haya ambayo yana bajeti na mpango huo tunaupeleka Serikalini ili kuhakikisha kwamba fedha hizo zikipatikana basi mashirika haya yanaweza kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja nyingine iliyotolewa ya ubovu wa barabara za mipakani. Hapa nataka nilieleze suala hili kwamba mpaka sasa hivi sera iliyopo haiweki barabara hizi chini ya Wizara ya Ulinzi au Jeshi la Wananchi, barabara hizi bado ziko kwenye mamlaka ya Halmashauri za Wilaya. Ndiyo maana tunapata tatizo kwa sababu zinakuwa siyo za kipaumbele chini yao matokeo yake ni kwamba barabara nyingi hazina hadhi inayotakiwa. Tunaweza kushauri hapo baadaye tutakapokutana kati yetu sisi, TAMISEMI na wenzetu wa Ujenzi kuona kwamba ni muhimu tukatafuta mpango maalumu kwa ajili ya barabara hizi. Hizi ni barabara za kiulinzi zinatakiwa zipitike muda wote kwa sababu huwezi kujua tatizo litatokea lini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, tunapokea ushauri wa Kamati, tutakaa na wadau wote ili tuone njia nzuri zaidi. Tukiwezeshwa kibajeti hata Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania wanaweza wakazitengeneza barabara hizi ili ziweze kupita wakati wote pale zitakapohitajika ziweze kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge mmoja alielezea suala la Jeshi kugeuka kuwa la kiuchumi. Nataka nieleze tu kwamba Jeshi lina matawi ya kiuchumi. Suma JKT, Nyumbu na Mzinga ni sehemu za Jeshi na mashirika yote haya yanafanya biashara. Kwa maana hiyo, siyo kwamba wakati huu wa amani Jeshi limekaa tu kuna biashara kubwa zinazofanyika mfano mzuri ni Suma JKT. Suma JKT wana viwanda vingi tu ikiwemo kiwanda cha maji, kiwanda cha ushonaji, kiwanda cha kutengeneza viatu, wako kwenye kilimo na ufugaji na wana miradi mingi mbalimbali. Nia na madhumuni ni wapate fedha ili kutatua matatizo ya Jeshi ambayo yako nje ya bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba na mimi nichukue fursa hii niwataarifu wenzetu wa Kamati kwamba mapendekezo yao tumeyapokea, tutayafanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)