Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia taarifa za Kamati hizi tatu na nianze kwa kuwapongeza Wajumbe wa Kamati zote tatu na Wenyeviti wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kuanza na suala la UKIMWI. Suala hili siyo siri. UKIMWI ulipoingia nchini kwetu miaka ya 80 ungeweza kumgundua mgonjwa wa UKIMWI kwa kumuangalia kwenye macho hivi kwamba huyu tayari, walikuwa wanasema kupandisha kenchi, unamwona mtu mabega yamepanda juu lakini kutokana na kuwepo kwa dawa za kufubaza leo ni vigumu kuweza kumgundua mgonjwa kwa macho. Mtu unamuona anakwenda anadunda kawaida amejaza vizuri lakini kumbe anaumwa, ni kwa sababu ya vile vidonge anavyokula. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, linalonituma kuzungumza suala hili ni utaratibu wa Taifa letu kutegemea wahisani katika kusaidia wagonjwa kwa asilimia 95. Hoja yangu hapa ni kwamba sasa inabidi tujiangalie. Mwenyekiti na Wajumbe wa Kamati, idadi ya watu hawa ni wengi na hawakutaka wenyewe, inabidi Taifa tujifikirie tutafute vyanzo. Wakati mwenzako anapokubeba Waswahili wanasema muangalie kisogo au ujikaze mwenyewe. Kuna hatari hawa watu wakaja kutukwamisha kwa kutukamatia kwenye ugonjwa huu. Napendekeza na Wabunge iwapendeze tuanze ku- allocate pesa nyingi zaidi kwenye tatizo hili ambalo tunalo. Ninalo hilo dogo, imebidi nilichangie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitachangia kidogo kwenye michezo. Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii ambaye amemaliza kuchangia, Mheshimiwa Nkamia, alikuwa anataka kujifanya eti ni wakala ananitafutia mimi timu za kwenda kukimbia, hapana. Hizi mbio za juzi nilikuwa na-test mitambo, mimi siyo mwanariadha. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo ambalo nataka kuungana naye ni kwenye dhana ya utawala bora, naazima msemo wa Rais wa Uganda, Mheshimiwa Kaguta Museveni, walipomuliza kwa nini Museveni uko madarakani, akasema ni vitu viwili; prosperity na security. Kwa hiyo, kwa nini mtu anaweza akawa anatamani kukaa miaka saba, labda anataka kujenga shule kila kijiji. Ikikupendeza mkwe wangu, Mheshimiwa Nkamia, kama una malengo mahsusi kama huyu Rais wa Uganda ambaye anatafuta prosperity na security kwenye nchi yake, basi na iwe hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianzime maneno ya Mheshimiwa Serukamba, juzi Mheshimiwa Museveni alikuwa anapokea kiwanda kinachozalisha lita 100,000 za maziwa akawa anamkabidhi mkwewe, akasema mimi tangia mwaka 1966 nachukia umaskini akawa anaonesha hiyo. Kwa taarifa Uganda inachakata maziwa lita milioni mbili kwa siku wakati sisi tunachakata lita 150,000 lakini nilipokuwa kule waliniambia tuna fursa ya kuchakata lita milioni 4. Nimeshazungumza na Waziri anayehusika na sisi tunakwenda huko, msiwe na wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumze suala la elimu. Tumefungua neema ya elimu ambayo imekuja na changamoto. Mimi kwetu huko kwa kipindi cha miaka mitatu nimeanzisha shule mpya za msingi tano, nimshukuru Waziri wa Elimu alinisaidia kuzi-fast track na kusajiliwa. Changamoto niliyoiona, jengo la vyumba vinne walijitokeza watoto 300 kuanza shule.

Mheshimiwa Spika, nachotaka kuliambia Bunge na Serikali ni kwamba tunapaswa tujiandae, Mwenyezi Mungu ametujalia kupata uzao sasa hao watoto wetu wasiwe bora wingi wa watu ila watu walioandaliwa vizuri. Zitafutwe rasilimali, watafutwe walimu ili waende kufundisha huko. Mimi nakwenda zaidi kwamba ikishindikana kuwaweka kwenye majengo bora hata tutengeneze maturubali ili mradi tuwe na walimu wawafundishe wale watoto kwa sababu mtoto aliyefika umri wa kwenda shule hawezi kusubiri.

Mheshimiwa Spika, Muadhama Cardinal Laurean Rugambwa alikoanzia darasa la kwanza kule kwetu Busita alikuwa kwenye nyumba ya nyasi, it was a shelter ya nyasi, lakini akasoma kwenye jengo lile na akaishia kuwa Kadinali wa kwanza Muafrika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Elimu wale Wadhibiti Ubora wadhibiti lakini wakikuta watoto wanasoma chini ya miti waruhusu wasome hata kwenye nyumba ya nyasi mpaka siku hiyo tutakapoweza kuwapatia jengo wanalohitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine kwenye elimu, naomba Waheshimiwa Wabunge wenzangu tukubaliane, mtoto ni wa kila mtu, kama ambavyo Mama Kikwete huwa anasema kwamba mtoto wa mwenzio ni mwanao. Sasa huyu mzee aliyekuja na elimu bure tusichukue watoto wetu tukamuachia, yeye alikuja na dhana nzuri kwamba elimu bure sasa tusimrushie mzigo, jukumu liwe la kwetu sisi.

Mheshimiwa Spika, unakwenda kwenye maeneo mengine watu wanajenga shule, unakuta mzazi ambaye mwanaye amekosa chumba cha darasa, hakuna mbao anataka kukuuzia mbao. Sasa sisi Wabunge tuisaidie Serikali, tupige propaganda, tuwahimize mtu awe tayari kutoa, aone kutoa mawe ni fahari, kushirikia kujenga ni fahari kwa sababu Mwenyezi Mungu ametusaidia ametupatia huu uzao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichangie kidogo suala la afya. Nimesikia Mheshimiwa Kapteni Mkuchika juu ya wataalam, nazijua taarifa nzuri za TAMISEMI wanapojenga majengo. Tunapofanya rationing ya majengo tuangalie ni wapi tunasubiria kupeleka wataalam na wapi tunasubiria kupeleka kituo kipya.

Mheshimiwa Spika, nikukaribishe siku moja uende kwetu Goziba, mimi nikiwa nchi kavu kwetu kwenda Ziwani Goziba nakwenda saa nane, sasa mtu anapokuwa Dodoma anafanya uamuzi wa wapi apelike wataalam, kituo changu ambacho drifting kwenye maji ni saa nane unasema tunasubiri, unakuwa hufikirii kwa kuwaangalia wale wenye tatizo. Ninayo zahanati kwetu Rutoro, ni kilometa 70 kutoka kwetu nilipozaliwa, wale watu wanakwenda kilometa 72 kwenda kwenye Jimbo la Mheshimiwa Rweikiza, unapokaa Dodoma, TAMISEMI, Utumishi wa Umma unasubiri kuja ku-allocate ina maana tunakuwa hatuangalii uhalisia. (Makofi)

Niombe TAMISEMI, Wizara ya Afya, mnapofikiria mnifikirie mimi, nahitaji wataalam Goziba kwa sababu watu wanakufa maji kila siku kule, hawawezi kupata huduma na kuna baradi kali. Keleba hakuna wataalam, tumeshajenga maboma, kwa miaka mitatu nimemaliza maboma tisa, Serikali na mimi mniunge mkono na wananchi wangu, tuna maboma tisa tayari yanahitaji kumaliziwa na yote yapo kwenye critical points ambazo haziwezi kufikiwa bila kutembea kilometa ndefu. Nilitaka nizungumze hilo la afya.

Mheshimiwa Spika, nizungumze na watu wa Utumishi kwamba kuna jambo unaweza kusubiri. Unaweza kusubiri kwenda shule lakini huwezi kusubiri kwenda kupata tiba. Kama tuna upungufu wa wataalam kwa mujibu takwimu tujinyime tuweze kuwaajiri watu, mgonjwa hawezi kusubiri. Utakaa uwe mjinga usijue kusoma na kuandika, sawa, utasoma ukiwa mtu mzima miaka 20 ndiyo uko darasa la kwanza unasoma ‘a, e, i, o, u’, hata usipojua kusoma basi utaangalia wenzako wanakwenda lakini mtu anayeumwa hawezi kusubiri. Maana yangu ni nini? Naiomba Serikali yangu sikivu mjitahidi tupeleke watu wa afya kwa sababu wagonjwa hawawezi kusubiri lakini watu wenye nguvu ndiyo wanaweza kuchangia uchumi.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, naomba kuunga mkono hoja zote. (Makofi)