Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
Ex-Officio
Constituent
None
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa hii kwa mara nyingine niweze kuchangia hoja hii muhimu sana ya Waziri wa Katiba na Sheria. Nikushukuru wewe Mheshimiwa Naibu Spika kwa kunipa fursa hii na nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri na niseme moja kwa moja kwamba naiunga mkono hoja hii.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema haya, naomba sasa nijielekeze kutoa ufafanuzi na ushauri kwenye hoja mbalimbali ambazo zimeelezwa na Waheshimiwa Wabunge ndani ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nianze na yale ambayo nimeyasikia kutoka kwa Wabunge hapa. Waheshimiwa Wabunge wameleta mapendekezo, kwa mfano Mheshimiwa Kakunda na Mheshimiwa Maige wameleta mapendekezo ya kufanya mabadiliko kwenye Sheria hii ya Manunuzi ya mwaka 2011.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba katika Mkutano huu wa Bunge Serikali italeta Muswada wa Marekebisho ya Sheria hii ya Manunuzi. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge mjiandae wakati utakapofika mchangie kukosoa ubovu wa ile sheria iliyopo sasa hivi ili tuwe na sheria nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nichukue fursa hii kujibu hoja ambayo imezungumzwa na Mheshimiwa Makamba ambapo alikuwa anasisitiza juu ya umuhimu wa wanafunzi wanaosoma Shule ya Sheria kwa Vitendo ya Tanzania kupata mikopo. Niwafahamishe Waheshimiwa Wabunge kwamba katika Bunge hili mlishapitisha sheria, katika Bunge la mwezi wa kumi mpaka wa kumi na moja mwaka 2014 ambayo inawapa haki sasa wanafunzi wanaosoma Shule hii ya Sheria ya Tanzania kupata mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Mheshimiwa Mtolea amezungumza akishauri kwamba pengine ingekuwa vizuri kwamba wakati wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria basi Kamati ya Sheria Ndogo nayo ingekuwa inatoa taarifa. Naomba kushauri tu kwamba ile Kamati haiwezi kutoa taarifa kwa sababu sio Kamati ya Kisekta. Kwa hiyo, hii Kamati ina muda wake huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ambalo ningependa kulitolea ufafanuzi katika hoja ambazo nimesikia kwa Waheshimiwa hapa ni kuhusu mapendekezo ambayo yameletwa na Mheshimiwa Holle kuhusu umuhimu wa kufanya mabadiliko kwenye Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kuchukua fursa hii kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba katika Mkutano huu wa Bunge hili pia Serikali italeta Muswada kwa ajili ya marekebisho ya sheria mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nichukue fursa hii kuzungumza mambo ya msingi sana ambayo yamejitokeza ndani ya Bunge hili Tukufu.
Kwanza nianze kwa kuwatahadharisha na kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge kwamba Ibara ya 12 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hasa ile Ibara ndogo ya (2) inasema; ―Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.‖
Mheshimiwa Naibu Spika, huu ndiyo msingi ambao pia umewekwa kwenye Kanuni ya 64 ya Kanuni za Kudumu za Bunge. Kanuni ya 64(1)(f) na (g) zinasema, Mbunge; ―(f) hatamsema vibaya au kutoa lugha ya matusi kwa Mbunge au mtu mwingine yeyote na (g) hatatumia lugha ya kuudhi au inayodhalilisha watu wengine.‖
Mheshimiwa Naibu Spika, huu ndiyo msingi ambao unapaswa utawale. Kwa sababu hizi Kanuni ambazo zina msingi wake kwenye Katiba, Ibara ya 12, zikitawala Bunge litaendeshwa kwa amani na Waheshimiwa Wabunge mtajikita tu kwenye hoja, mtawasaidia wananachi wenu ambao wanawasikiliza na ambao wamewatuma ili mje muwatete.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba hizi nimeona mambo haya ya kudhalilishana yakijitokeza na mambo yameanzia kwenye hotuba rasmi ya Kambi ya Upinzani. Naomba kushauri kwamba hatupaswi kufikia hatua hiyo. Nianze na hili la kuwaita Majaji kama majipu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, Katiba hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 30(2)(d) inalinda hadhi na uhuru wa mahakama na heshima yao. Ibara hii inasema hivi, naomba kunukuu yaani; ―ni wajibu wa kila mtu na kila raia kulinda sifa, haki na uhuru wa watu wengine au maisha binafsi ya watu wanaohusika katika mashauru mahakamani; kuzuia kutoa habari za siri; kutunza heshima, mamlaka na uhuru wa mahakama.‖
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona imezungumzwa vibaya hapa, Waheshimiwa Majaji wakiitwa majipu, hiyo ni kuwavunjia heshima yao. Pia ni kuudhalilisha mhimili wa Mahakama ambao tunapaswa tulinde heshima yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu fulani kwenye hotuba hii imezungumzwa kwamba sasa hivi Majaji hawa siyo watakatifu na kweli hakuna mtu ambaye ni mtakatifu lakini wanaishi kwa kuzingatia Katiba na sheria. Wao katika Ibara ya 107 Katiba inasema watakuwa huru wanapotekeleza majukumu yao isipokuwa tu watapaswa kuzingatia masharti ya Katiba hii na sheria za nchi. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kushauri kwamba tunapokuwa tunazungumzia ama mtu au mihimili tutumie lugha fasaha ili kulinda hadhi na sifa za mihimili mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna hii haikuwa sahihi pia kumzungumzia Mheshimiwa Jaji Mkuu kwa namna ambayo imezungumzwa, ni kinyume cha Ibara ya 12 ya Katiba na Kanuni kwa sababu Kanuni yenyewe ya 64(1)(c) inakataza hata unapojadili kutolitumia vibaya jina la Jaji, Rais na kumuongelea mtu ambaye hayupo.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Kwa hiyo, mimi nilikuwa nashauri kwamba mambo haya tuyazingatie sana tunapotekeleza majukumu yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa sababu ya kulinda hadhi na thamani ya utu ambao umewekwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania sharti tuheshimu mamlaka ya viongozi wa Serikali walioko.
Sehemu fulani katika hotuba hii imezungumzwa kwamba Rais Shein ni kibaraka. Rais Shein kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar huyu ni Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, utamwitaje Rais wa nchi kwamba ni kibaraka. (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Huku ni kumdhalilisha kitu ambacho kimekatazwa na Kanuni zetu za Bunge, ni kumvunjia hadhi, ni kuidharau mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hili halipaswi kusemwa na Wazanzibari wako hapa halafu wanashangilia that is too much odd to me. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwakumbushe tu kwamba sisi Wabunge tunapokuja hapa tunakula kiapo. Kwa mujibu wa Ibara 68 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatupasa tule Kiapo cha Uaminifu. Kanuni ya 24 ya Kanuni za Kudumu pale kuna kiapo cha utii na ambacho kinasisitiza kulinda na kuhifadhi Katiba, wote tumeapa hapa. Muungano huu upo kwenye Katiba na ni kwa sababu ya Muungano huu ndiyo maana leo tuko hapa na ndiyo maana tunapata fursa ya kuzungumzia wananchi wetu na kutoa hoja mbalimbali za kuisaidia Serikali. Kwa hiyo, mimi naomba tuheshimu viapo vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Zanzibar haiwezi kuwa koloni. Ukisoma Ibara ya 1 ya Katiba ya Zanzibar inasema hiyo ni nchi ambayo kabla ya Muungano ilikuwa ikiitwa Jamhuri ya watu wa Zanzibar. Ibara ya 2 inasema, Zanzibar ni mojawapo ya nchi mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano Tanzania. Sasa leo Zanzibar itakuwaje tena koloni? Lazima muelewe haya mambo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, si kweli kwamba Zanzibar imekuwa koloni la Tanzania, Zanzibar ni mamlaka halali. Ibara hii ya 1 na ya 2, ukiacha tu makubaliano ya 1964 (Articles of Union) zimepitishwa baada ya kupigiwa kura ya maoni na Wazanzibari wote wakakubali ule Muungano. Kwa hiyo, si vizuri kutumia fursa hii kuwavuruga wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Ibara ya 28(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inataka kila raia pamoja na mambo mengine alinde, adumishe na kuhifadhi umoja wa Taifa letu. Ibara ya 23(4) ya Katiba ya Zanzibar nayo inawataka Wazanzibar kudumisha umoja wa Wazanzibar. Mimi naona kama tunakuwa salama sana tunapokuwa tunadumisha umoja kuliko kuja kutofautiana hapa kwa sababu ambazo wala hazina sababu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba Ibara ya 20(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inakataza vyama vya siasa kupigania kuvunjwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huwezi kuwa umekula kiapo cha kuitii Katiba ambayo ina masharti ya kutokusajili vyama vinavyopigania kuvunjwa kwa Muungano wa Tanzania halafu ukabaki Bungeni. Mimi nafikiri umefika wakati sasa mamlaka zinazohusika zichukue hatua. (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nizungumzie hili la hati ya mgawanyo wa madaraka ya Rais. Nimesema sana hapa na naomba nirudie tena kwa sababu ni kazi yangu. Baadhi ya Waheshimiwa Wabunge hawakuwepo na nalazimika kuirudia hii ili niweke record sawa.
Moja, Mawaziri hawa wanateuliwa na Rais kwa mujibu wa Ibara ya 55 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wanakabidhiwa majukumu yao chini ya Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Mawaziri, Sura ya 299 halafu kuna hiyo hati inaweza ikatolewa na Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mchengerwa amelifafanua vizuri hili, nilimuona Mheshimiwa Tundu akimpigia makofi na mimi nimeshalisema siku nyingi sana yaani hata kulisema naona kama nachoka. Kwa sababu neno linalozungumzwa pale katika ile kifungu cha 5 linasema, the president „may‟ from time to time na matumizi ya neno ‗may‟ limetafsiriwa vizuri kabisa katika Sheria ya Tasfiri ya Sheria, kifungu cha 53 kinaeleza nini maana ya maneno ‗may‟ na ‗shall‟ yanapotumika katika sheria. Neno ‗may‟ linaashiria hiari na ‗shall‟ inaashiria lazima, kwa hiyo, hili lisingekuwa ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika hali ya kawaida hata Waheshimiwa wasomi wanafahamu kwamba sheria ndogo (subsidiary legislation) haiwezi ika-supersede sheria kuu, ile sheria yenyewe ya Utekelezaji wa Majukumu au Katiba. Rais alipokuwa anatangaza zile Wizara alisema kabisa, kwa mfano Wizara inaitwa Wizara ya Maliasili na Utalii…
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Kwa hiyo, unajua kwamba haya ni majukumu yao. Kwa hiyo, kutoitoa ile hati hakuwa amevunja Katiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nieleze pia kwamba Sheria hii ya Utekelezaji wa Majukumu ya Mawaziri inasema ikiwa kuna jambo lolote labda linachunguzwa Mahakamani au is likely to be inquired in the court, basi hawa watu wataenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwanasheria Mkuu wa Serikali atakachosema ni kwamba suala hili linaangukia dhamana ya mtu fulani au Wizara fulani ndiyo mwisho wa hilo suala, kwa hiyo, sheria yenyewe haimlazimishi Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niwaambieni Kanuni zinatukataza kusema uongo. Jana niliwaambia na wiki iliyopita nilisema mpaka nikawapa waandishi habari, gazeti la Sauti ya Watu Daima liliandika kwamba Rais alishatoa hiyo hati tangu tarehe 22/04/2016…
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Kupitia government notice ambayo ni public notice.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili halipaswi kutusumbua sana. Ni suala ambalo linaletwa labda kwa namna ya kupotosha tu. Haiwezekani kwamba subsidiary legislation ika supersede sheria kuu na hata Katiba yenyewe.
MBUNGE FULANI: GN namba ngapi?
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Ni GN namba 144…
MBUNGE FULANI: Iko wapi?
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Ya tarehe 22 Aprili, 2016.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa AG naomba uongee na Kiti.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kutakuwepo kwa hiyo, haisaidii kwa sababu Mawaziri na Serikali yote inafanya kazi kwa mujibu wa Katiba, sheria, sera na Ilani ya Uchaguzi ya chama kinachotawala. Mpaka sasa hivi hakuna mtu yeyote aliyekwenda mahakamani au aliyekuja kuniuliza mimi kwamba hivi suala hili linaangukia kwenye dhamana ya nani? Rais hakupewa muda kwamba ndani ya muda fulani awe ametekeleza suala hili. Kwa hiyo, mimi naomba kushauri hili suala labda sasa kama Kiti chako kinaweza kuamua kiamue kwa sababu tumelisemea mno halina tija kwa Watanzania. (Makofi)
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Mheshimiwa Rais huyu ambaye amezungumzwa hapa kwamba anatawala kiimla Rais huyu hatawali kiimla. Ibara ya 33 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema Rais ni Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu. Kama kiongozi wa Serikali katika mgawanyo wa madaraka, Serikali ina mamlaka ya kusimamia utekelezaji wa sheria, anachokifanya sasa Rais ni kutukumbusha turejee kutekeleza sheria kwa ufanisi. Hata haya mambo yanayofanyika ya uwajibishaji ni katika kuturejesha katika uzingatiaji wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais mwenyewe ana mamlaka chini ya Ibara ya 36 ya Katiba kuwawajibisha hata wale ambao hakuwateua, lakini pia Mawaziri wana mamlaka ya kuwawajibisha wale ambao wanawateua, Makatibu Wakuu na Bodi zina mamlaka ya kuwawajibisha wale ambao wanawateua. Mtu ambaye anadhani ameonewa Mahakama iko pale aende akatafute haki yake. Watanzania wengi sana ambao walidai wameonewa wameenda mahakamani wamepata haki zao. Kinachofanyika hawafukuzwi, wanachoambiwa ni kwamba wanawekwa pembeni ili wakachunguzwe na wakati wa kuchunguzwa wanapewa fursa ya kujitetea.
MBUNGE FULANI: Naam!
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Kama wana hatia basi wanawajibishwa, kama wengine wana makosa ya jinai wanashtakiwa. Kwa hiyo, hili sasa halipaswi kurudiwarudiwa hapa kila siku kana kwamba ni jambo la msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo naomba kulizungumzia ni suala la kudai kwamba Bunge linaongozwa na Ikulu hii si kweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma Ibara ya 62 ya Katiba inamtaja Rais kuwa sehemu ya Bunge hili na Ibara ya 63 ndiyo inasema Bunge ndicho chombo kwa niaba ya wananchi kina jukumu la kuisimamia na kuishauri Serikali. Rais huyu huyu ambaye ni sehemu ya Bunge hili ndiye anayelipa hata hizo posho kwa masharti yenu yale. Masharti ya posho zile mpaka ziidhinishwe na Rais.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, haya mambo ya matangazo ni mambo ambayo iliamuliwa na ikapitishwa humu kwamba matangazo sasa yafanywe na studio ya Bunge na Bunge likapitisha hapa Sheria ya Matumizi ya Fedha. Kwa hiyo, siyo sahihi kudai madai hayo. Halafu mnawachonganisha viongozi wa Bunge, Bunge ni mhimili ambao hauwezi kuingiliwa tu na Serikali itauingiliaje?
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala hili mimi nashauri Kiti chako kilichukulie hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.