Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika,
nakushukuru kunipatia nafasi kufafanua baadhi ya mambo ambayo yamechangiwa na Waheshimiwa Wabunge katika masuala yanayohusiana na Wizara yangu.

Mheshimiwa Spika, pili, nichukue nafasi hii kushukuru sana kwa uongozi madhubuti ambao Wizara yangu inapata kutoka katika Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa ambayo ndiyo Kamati inayohusika na Wizara yangu. Wanafanya kazi nzuri, Mheshimiwa Rweikiza, Makamu wake Mheshimiwa Mwanne Mchemba, pamoja na Wajumbe wote wa Kamati ile tunakwenda vizuri sana na mafanikio tunayoyapata katika Wizara yetu ni mafanikio pia yaliyochangiwa na Kamati hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikianza na suala la uhaba wa watumishi, nadhani juzi nililifafanua na leo nitalisema kwa kifupi sana. Tunakubadili kwamba mwaka jana walimu wengi wamestaafu na wengine wameaga dunia, nikasema tayari tuliomba tupate takwimu hizo kutoka Wizara ya Elimu wamekwishatuletea tunangoja za TAMISEMI nao watuletee. Tunataka kwanza kujaza mapengo hayo, tukijaza mapengo hayo maana yake ni kwamba hakuna gharama ya mishahara mipya, tena kwa uhakika ni kwamba hata mishahara tutakayolipa ni pungufu kwa sababu hawa watakaowaajiri ni wapya, wale waliostaafu walikuwa na mishahara mikubwa kuliko tunaotaka kuwaajiri. Kwa hiyo, haitupi mashaka na hatupati shida kutamka kwamba tutajaza mapengo kwanza baada ya hapo tutaangalia hali ya uchumi wetu tutakuwa na ajira mpya. Kwa hiyo, nilitaka niseme hivyo kwa upande wa watumishi hasa upande wa elimu na afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini juzi pia nilipochangia nilisema kwa wimbi hili la kwamba tunajenga zahanati, vituo vya afya na hospitali kila mahali, msingoje mmalize kabisa, wale ambao wanajua kwamba zahanati au kituo chetu cha afya tutafungua tarehe fulani, tuleteeni maombi hayo ili jengo likikamilika, vifaatiba vikipatikana kazi ya tiba ianze mara moja. Naomba wote mfanye hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine amezungumza ndugu yangu, Mheshimiwa Selasini kuhusu masuala ya utawala bora. Kauliza swali, je, hao tunaowateua tunawapekua? Kwa uhakika nataka nithibitishe tunaowateua kabla hatujakuteua tunajiridhisha, je, wewe raia, mwenendo wako, akili yako iko timamu, unaishi vizuri na watu, upekuzi tunafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ambalo amelizungumza ambalo namuunga mkono na nataka niseme hii ni practice ya dunia nzima, utawala wa Rais mpya akiingia anafanya mabadiliko kwa jinsi anavyoona yeye inafaa. Nilitoa mfano siku moja mule ndani, ukienda Marekani kule mpaka wapika chai wale wote State House mfagizi, dereva, wote wanaondoka kupisha timu mpya. Sasa hili lililofanyika ni kwamba uteuzi umefanyika lakini namuunga mkono mdogo wangu Mheshimiwa Selasini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la mafunzo kwa wale wanaoteuliwa, jambo hili nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tumelifanya. Tumefanya mafunzo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala na sasa tumeshaandaa tayari mafunzo kwa Makatibu Tawala wa Wilaya, yatafanyika muda wowote kuanzia leo. Kila kitu wameshapelekewa, nauli na jinsi watakavyofika, wanangoja tu tuwaambie lini na wapi, watapata mafunzo kwa sababu ni muhimu sana hawa Maafisa Tawala wa Wilaya wakapata mafunzo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo amelizungumzia ni Regional Administration Act ya mwaka 1997, nataka nirudie tena kufafanua, ambayo inampa Mkuu wa Wilaya madaraka ya kumweka mtu ndani muda wa saa 24. Nataka nirudie, muda wa saa 24, lugha iliyozungumzwa pale ni kwa usalama wake. Kwa usalama wake maana yake, ameua mtu, jamaa zake wamekasirika wanataka kumpiga yule aliyeua, unamweka ndani kwa usalama wake. Sheria inasema akishamaliza saa zile 24 asubuhi lazima umpeleke Mahakamani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mahali popote, nilisikia siku moja, Mkuu wa Wilaya kumweka mtu ndani muda wa saa 48 ni makosa kwa sababu sheria inampa yeye saa 24, Mkuu wa Mkoa amepewa saa 48. Nataka niwahakikishie Watanzania kupitia Bunge hili, mimi ni Waziri wa Utawala Bora, kazi zangu sifanyi kwenye mkutano wa hadhara na kusema leo tumefanya haya na haya, watumishi wote wa umma wanahusika na utawala bora. Kwa hiyo, inapokuja kwenye suala la utawala bora mimi ni Waziri wa Wizara zote, tunafuatilia tunachukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkuu wa Mkoa saa zake ni 48, anaweza akamweka saa 24 akipenda. Nachotaka kusema siyo lazima wewe umuweke mtu ndani kama ni criminal offence OCD yupo, kama ni suala la Uhamiaji, Afisa Uhamiaji yupo, kama amekwepwa kodi mtu wa TRA yupo, siyo lazima haya mambo utamke wewe!

WABUNGE FULANI: Sawa kabisa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Tuache. Yupo mzee wangu mmoja anasema kujimwambafai yaani uonekane wewe ni mwamba. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, nawaomba huko mlipo msiniharibie kazi yangu, mimi ndiye mwenye title ya utawala bora. Mimi ndio Waziri mwenye nafasi ya utawala bora, ukiendesha mambo kinyume na utawala bora unaniharibia kazi na sitaki Mheshimiwa Dkt. Magufuli anibadili. Mimi nataka Mheshimiwa Dkt. Magufuli aseme mzee endelea hapohapo ulipo. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, hili jambo humu ndani tumelizungumza na kwenye mafunzo tumelielekeza. Sasa nina hakika na upande mwingine pia mngepongeza maana ile vurumai siyo imepungua kidogo, imepungua sana, maji yametulia kwenye mtungi. Yametulia kwenye mtungi kwa sababu tumewapa elimu na wameelewa. Kwa hiyo, naunga mkono alichosema ndugu yangu Mheshimiwa Selasini kwamba tuwape elimu na tumewapa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niwaambie, mkitaka kujua kwamba masuala ya utawala bora nchi hii tunakwenda vizuri, mtupongeze tu. Jana, siyo juzi, Taasisi ya Transparency International inaonyesha kwamba mwaka 2017 duniani Tanzania tulikuwa wa 102 lakini jana tumekuwa wa 99. Kwa nchi zote duniani unazozijua wewe katika suala la utawala bora Tanzania ya 99. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nachosikitika tu ni kwamba bado hatujamshinda Rwanda katika Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, yeye anaongoza sisi tunashika nafasi ya pili. Nasema kwa mwenendo huu tulipoacha kutianatiana ndani hovyo, nina uhakika tutakuwa wa kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo limegusiwa na wachangiaji ni Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) kutokufika baadhi ya maeneo. Nataka niwahakikishie TASAF tumefikia walengwa asilimia 70 nchi nzima, bado asilimia
30. Serikali imefanya maandalizi katikati ya mwaka huu malengo ni kufikia asilimia 30 iliyobaki. Kwa hiyo, wale ambao hamjafikiwa msiwe na wasiwasi, Serikali inafanya maandalizi ili tuweze kufikia maeneo yote.

Mheshimiwa Spika, lakini katika hili la TASAF nataka kutoa onyo moja, mnisikilize ili huko mliko msije mkaniletea matatizo katika Wizara yangu. Baadhi ya viongozi wa Wilaya wanawalazimisha walengwa wa TASAF kutoa michango bila kuwashirikisha na hasa ile ya bima ya afya. Tunasema zungumzeni nao wajiunge bima ya afya lakini wilaya moja tumeshamfukuza yule wa TASAF na mkubwa wake pengine anasubiri ngazi za juu huko. Michango ya maendeleo vijijini, sijui wanajenga shule, zahanati, watu wakiwa wagumu kuchanga wanakwenda kukata hela za TASAF, hilo ni marufuku. Nasema wilaya moja imeshatokea, taarifa zimefika kwangu, yule wa TASAF tumemfukuza, wale wengine wanasubiri wakubwa waliowaweka wawachukulie hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani mtu anapata Sh.20,000 kwa mwezi baada ya miezi miwili halafu wewe unamkata Sh.15,000 unasema mchango wa kujenga shule lakini wale ambao wana uwezo hawakuchanga, unakwenda kumchangisha maskini. Nasema ikitokea namna hiyo hatutavumilia. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, ilibaki pointi moja, walikuwa wanaomba wenzangu na mimi naomba hapohapo na kwa sababu unatupenda wote sawa utaniruhusu tu. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ndugu zangu, humu ndani nilitoa ufafanuzi nini maana ya barua kusema UFS, Kiswahili ni Kupitia Kwa, nikasema mtumishi yeyote wa Serikali ana haki ya kuwasiliana na mwajiri wake. Nikasema pia mtu akiandika barua ya kuomba uhamisho wewe Mkurugenzi, Mkuu wa Shirika, Katibu Mkuu anaandika barua inakwenda kwa mwajiri wake, anaomba barua ile ipite, wewe unachukua barua unaweka katika droo unasema mimi sipitishi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilisema siku ile tukimpata kiongozi wa namna ile tutamuwajibisha. Anapopitisha barua kwako amekuheshimu, maana yake barua iende lakini with comments, anakupa fursa wewe kutoa maoni. Unaandika pale nakubali ahamishwe ili mradi nipate mbadala.

MBUNGE FULANI: Ndiyo.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Amekuja juzi hajamaliza miaka mitatu sipendekezi uhamisho huu. Barua lazima iende wenye kuamua kule kwamba uhamisho umekubaliwa au haukukubaliwa ni yule aliyemuandikia siyo wewe UFS. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini na watumishi nao nataka niwape darasa, barua yako ikishapitishwa haina maana kwamba uhamisho wako tayari umeshakubaliwa, ni kwamba pale imepitia inasubiri uamuzi kule juu. Niliomba siku ile msitufanyie kazi ya kuamua sisi tulioandikiwa barua, tuachieni sisi wenyewe tuamue. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono taarifa za Kamati hizi, nakushukuru. (Makofi)