Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Dr. Susan Alphonce Kolimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. DKT. SUSAN A. KOLIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana nami kupewa nafasi ya kuchangia hoja hii iliyoko mbele yetu. Moja kwa moja kama wenzagu waliotangulia, naomba niunge mkono taarifa zote mbili zilizotolewa mbele yetu na maoni na maazimio ya Kamati hizo zote mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyoongea Mheshimiwa Timotheo, Mbunge, jirani yangu, narudi pale pale kwenye suala la uhuru. Tunapozungumzia suala la haki ya uhuru kwa raia yeyote wa Tanzania, tunazungumzia suala ambalo liko ndani ya Katiba yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Timotheo alipozungumzia kuhusu suala la haki na uhuru, pia alitukumbusha kwamba tunapodai uhuru lazima pia tujue kwamba tunatakiwa kuwa na wajibu. Ukimsikiliza mzungumzaji, Mheshimiwa Mbunge Lema, alipokuwa anazungumza alitukumbusha sisi wote kama Wabunge wa Upinzani na wa Chama Tawala kwamba tunapozungumza kwamba watu wengine wako Magerezani, maana yake ni kwamba tukumbuke kwamba nasi pia tutakwenda Magarezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hoja yake na dhana yake naitafsiri kwamba Mheshimiwa Lema anakubali kabisa utendaji wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu inasimama kwenye haki na wajibu. Pale ambapo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaposimamia suala la uhuru, haki na wajibu, maana yake ni kwamba pale inapoona mwananchi au raia yeyote wa Tanzania anavunja sheria, ni lazima hatua za kisheria zichukuliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kwamba nakubaliana na Mheshimiwa Lema anaposisitiza kwamba sisi wote tuwajibike, tusimamie sheria, tuzifuate na tuzitekeleze. Sheria hizi ni msumeno, inaweza ikakata upande wowote na hatuwezi kusema kwamba pale wanapowekwa Magerezani labda wanachama wanaotokana na Chama cha Mapinduzi maana yake ni sahihi; lakini wanapoguswa wanachama wanaotokana na vyama vingine maana yake sheria inavunjwa au Katiba inavunjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naomba nizungumzie kuhusu utendaji wa Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zake. Tumeona katika Kamati, Wizara hii imejipanga vizuri na hasa kwa kuanzisha vile vyombo vipya ambavyo vimewekewa utaratibu. Kitu ambacho nimekipenda zaidi ni pale ambapo Taasisi mpya ambazo zimeanzishwa ndani ya Wizara hii ya Katiba na Sheria zinapoweka utaratibu wa mpango kazi wa utekelezaji wa majukumu yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kitendo cha Wizara ya Katiba na Sheria cha kuanzisha zile Mahakama za kielektroniki, nafikiri ni wazo zuri kwa sababu litakuwa linasaidia kupunguza msongamano wa uendeshaji wa mashtaka madogo madogo yaliyopo ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ndani ya Kamati, tumepata taarifa ya jinsi Wizara ya Katiba na Sheria ilivyojipanga vizuri katika kujenga capacity ya watumishi watakaojiriwa katika Taasisi hizi mpya na kule katika Wizara zao. Ninachoshauri, Wizara iweze kutumia nafasi waliyonayo ya kuhakikisha kwamba katika kila mwaka waweke mpangokazi wa kuhakikisha kwamba wanajenga uzoefu na ujuzi kwa wafanyakazi na watumishi watakaoajiriwa na wale ambao wanafanya kazi katika Ofisi husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba Wizara pia iweze kutumia vizuri zile scholarships ambazo zinatolewa na Mataifa mbalimbali rafiki ili kuwajengea uwezo na hasa practice katika Taasisi hizi mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naunga mkono ushauri uliotolewa pia na Kamati Ndogo ya Sheria Ndogo ya Bunge ambayo pia imejaribu kuangalia upungufu unatotokana na sheria ndogo ndogo zinazotungwa katika Taasisi, kwenye Wilaya au Ofisi za Kiserikali. Katika upungufu huo, tunaungana nao kwamba utaratibu uwekwe vizuri, pale ambapo Taasisi au Ofisi zinapotunga hizi Kanuni, zihakikishe kwamba zinatengeneza mpangokazi wa kuhakikisha kwamba kabla hazijatolewa kwa matumizi, zinapitiwa vizuri na kuhakikisha kwamba hazikiuki masharti yaliyowekwa kwenye sheria na Katiba ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na-declare interest kwamba mimi ni Mjumbe kutoka kwenye Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge, nitaendelea kuishauri Serikali na kuhakikisha kwamba wanatekeleza majukumu yao bila kuvunja sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka pia kutoa mawazo kwamba pale ambapo sheria au sheria ndogo zinapotungwa, waweze kuwajulisha watumiaji, wadau wanaotumia hizo sheria ndogo ili waweze kuzitumia sheria hizi bila kuzivunja na kupata mataizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja kwa taarifa hizi zote mbili. Ahsante sana. (Makofi)