Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

Hon. Rwegasira Mukasa Oscar

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018

MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na kwa namna ya pekee namshukuru Mungu kwa nafasi hii na nawapongeza Wenyeviti wote wawili wa Kamati hizi kwa kazi nzuri kabisa. Kimsingi kwa kiwango kikubwa sana binafsi nakubaliana na mapendekezo yao lakini nina mambo machache ya kuchangia. Miongoni mwa mambo ambayo kwa upande wangu, naona ni mafanikio ya juu kabisa ya Serikali ya Awamu ya Tano ikiongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli toka imeanza, ni lile jambo la uchumi jumuishi. World Economic Forum ilitangaza Tanzania kwamba ndio nchi inayoongoza kwa kuwa na uchumi jumuishi kwa mwaka 2018. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni jambo kubwa kwamba ni uchumi ambao mbali ya kujali saizi yake au unafanyaje kazi, kwa uzuri kiasi gani, unajumuisha watu wengi wa makundi yote kwenye nchi husika, hili ni jambo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kulileta kwenye muktadha wa leo, juzi tarehe sita nilimsikia Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli akisihi mahakama zetu mhimili wa mahakama, kwamba sasa wakati umefika wa kuanza kuhakikisha kwamba sheria zetu sasa zinaandikwa na kufanyiwa kazi kwenye mahakama kwa lugha ya Kiswahili. Kwa nini naona hilo ni jambo zuri, mtafiti mmoja amefanya utafiti mwaka 2014 hapa Tanzania anasema miongoni mwa Watanzania milioni 54, asilimia 90 wanaongea Kiswahili na asilimia nne wanaongea Kiingereza nne tu na waliosalia ndio wanaongea zile lugha za kienyeji kabisa.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria yetu ya Tafsiri za Sheria kifungu cha 84 kina vifungu vitatu, cha kwanza kinasema the language of the laws of Tanzania shall be written in English or Swahili, kwamba itakuwa kwa Kiingereza ama Kiswahili na pale ambapo hizo version mbili zinagongana, ile version ambayo ndio original sheria ilitengenezwa kabla ya kutafsiriwa ndio itatumika, lakini pale ambapo zilitungwa zote kwa pamoja Kiingereza kitapewa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapo swali langu ni kwa nini tunapambana kujiondoa kwenye utegemezi wa mambo ya kiuchumi na mengine lakini hatutaki kuondoka kwenye utegemezi wa mambo ambayo yanatupa nafasi ya wananchi wetu kushiriki vizuri pale wanapotaka haki zao, kushiriki vizuri pale ambapo wanatakiwa kujieleza, kushiriki vizuri pale ambapo hata kama anasimamiwa na Wakili mahakamani, pamoja na kwamba hana uwezo wa kufanya tafsiri ya kisheria, lakini angalau awe na fursa ya kuelewa Wakili wake anasema nini mwenendo wa Wakili wake unakwendaje kwa maana ya hoja. Hiyo inakuwa ni sehemu ya kupata ile haki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ibara ya 71 ya Katiba ni mfano ambapo kifungu kile kinatoa masharti ya ni namna gani mtu atapoteza nafasi ya Ubunge. Kuna tofauti kwenye version ya Katiba ya Kiingereza na ya Kiswahili, ambapo kifungu ambacho kinasema kwamba yoyote ambaye
samahani niangalie kidogo hapa, kifungu (e)Iwapo Mbunge atachaguliwa ama kuteuliwa kuwa Makamu wa Rais ni moja ya masharti ya ibara hiyo kwamba atapoteza Ubunge, lakini version ya Kiingereza ya ibara hiyo inaongea kitu kingine. Kwa hiyo suala hili limeshatokea mahakamani, ukatokea mtafaruku, sio mtafaruku wa maana ya kukosea nini kinasema pale, lakini mtafaruku wa maana kwamba kilichoandikwa upande huu ni tofauti kabisa na kilicho upande huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahakamani wanatoa haki ya Katiba ya Kiswahili kwamba ndio iwe ya kwanza kufanyiwa rejea kabla ya ile ya Kiingereza kwa sababu Katiba yetu ilitungwa kwa Kiingereza kama version ya kwanza kabla ya kutafsiriwa. Ushauri wangu niiombe Serikali hebu tufanye mabadiliko tulete hadhi ya lugha yetu, lakini na fursa ya watu kushiriki kwenye haki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, katika ukurasa wa 41 wa ripoti ya Kamati ya Katiba na Sheria, wanasema moja ya mapendekezo yao ni usimamizi wa utoaji haki nchini kwamba ni jambo la muhimu sana na wameeleza pale. Nimewahi kushuhudia Biharamulo miongoni mwa mahabusu ambao wamewekwa gerezani pale kwa muda mrefu kabisa, nilipata fursa siku moja nikaingia gerezani pale, nikazungumza na baadhi yao kila mmoja akasema jambo lake. Nikagundua kwamba kulikuwa na mambo ambayo mengine hata sikuwahi kudhani kama yako dunia hii, lakini nikachukua fursa nikamwomba Waziri wa Sheria wakati huo Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe alifanya kazi nzuri sana akaja na DPP pale wakasikiliza watu kwa siku moja tu, kuna mahabusu 40 waliondoka mle gerezani kwa sababu ukaaji wao mle ulikuwa kwa kweli huko kinyume cha sharia, wengine hata zile hati za kuwafutia mashtaka zimeshatolewa miezi sita iliyotangulia lakini watu wako mle. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuwe na utaratibu mbali na hii ambayo Mbunge anaweza kumwomba Mheshimiwa Waziri wa Sheria na DPP kwenda, tuweke utaratibu wa kimfumo wa kuhakikisha tunaweza tukafanya checks and balances za mambo kama haya kwa sababu kuna watu wako kule chini hana mahali pa kusemea, anaminywa haki yake, anakaa miaka miwili, mitatu bila sababu ya msingi na ushahidi Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe nilikwenda nae katika Gereza la Biharamulo, waliondoka watu 40 kwa yeye na DPP kukaa na kuwasikiliza watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti ya Kamati ya Sheria Ndogo, katika ukurasa wa sita yapo mambo ambayo wanalalamika, wanasema kumekuwa kuna tatizo la sheria ndogo kwenda kinyume na sheria mama au sheria nyinginezo za nchi, lakini kuna matatizo ya sheria ndogo kuwa na makosa ya uandishi, matatizo ya sheria ndogo kutozingatia misingi ya uandishi, kwa mfano hansard zinaonesha wamewahi kupata report ambayo sheria mama inasema kosa fulani adhabu yake ni shilingi 100,000, sheria ndogo kule imekwenda imefanya kitu kwenye muktadha ule unasema 300,000 kwa sababu ya makosa ya uandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya mambo unaweza kuona ni kosa la uandishi kwenye karatasi, lakini huko kwenye field haya mambo yanaumiza watu. Tunaomba tujue namna gani Wizara inayohusika watachukua hatua kwa sababu kumbukumbu za Bunge zinaonekana kwa Kamati hii haya ni malalamiko ambayo yamekuwa yanajirudia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru na naunga mkono. (Makofi)