Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Nitachangia katika taarifa ya Kamati ya Katiba na Sheria katika maeneo machache, lakini la kwanza nitaanza ni katika suala la kuwajengea uwezo kiuchumi vijana ambalo linafanyika kwa kutumia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Naomba nitumie fursa hii kuipongeza sana Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa jitihada ambazo zinafanyika katika kuwawezesha hawa vijana ambao ndiyo inapunguza kasi ya changamoto ya ajira katika nchi yetu. Hilo ni moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maelezo ya kwamba sehemu hii mwaka 2015/2016 zimetolewa bilioni moja; 2017/2018 zimetolewa bilioni 2.7; na naamini baadae wataendelea kutoa zaidi na zaidi, hii ni nia njema. Tatizo ndiyo hilo changamoto imeonekana, naomba niiseme ili iweze kufanyiwa kazi na Serikali, ni usimamizi wa hivi vikundi vya vijana ambao wanapewa hizo fedha, yaani hizi SACCOS. Kwa kweli imeonekana kwamba hizi fedha zimetolewa kwa lengo jema, lakini vikundi ambavyo vinapewa vinaonekana kwamba vinatumia hizo fedha kinyume cha malengo waliyojiwekea, hiyo ni changamoto. Pia inaonekana kwamba hizo fedha pia zinatolewa bila kuelewa kama hicho kikundi kweli kipo ama hakipo. Kwa hiyo wito wangu ni kwamba Serikali iweze kuzisimamia au kuzishinikiza halmashauri zetu ziweze kusimamia hivi vikundi vya vijana ili lengo jema kabisa la Serikali ambalo limekusudiwa liweze kufanikiwa. Hiyo ni sehemu moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ni suala la ufinyu wa ukomo wa bajeti kwa baadhi ya taasisi zinazosimamiwa na Kamati ya Katiba na Sheria ambayo ni miradi iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika sehemu ya Bunge, Kazi, Vijana na Ajira na Wenye ulemavu. Hii imeonekana kwamba miradi mingi inategemea fedha za nje, hii ni changamoto. Kutegemea fedha za nje ni changamoto na kwa nini nasema hivyo? Nasema kwa sababu Mheshimiwa Rais ameshaligundua hilo kama ninavyoliona mimi na Watanzania wengi naomba waelewe hivyo. Fedha za ndani ni muhimu, kwa hiyo ili tuweze kupata fedha za ndani lazima wananchi tuhimizwe kukusanya kodi kwa wakati, tulipie, tuwe watiifu, tutengeneze miradi mingine kupitia Serikali yetu ili tuongeze vyanzo vya mapato ya ndani ya nchi yetu na hili jambo linafanywa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tuongeze jitahada ya kuunga mkono Serikali kuongeza mapato ya ndani ya nchi. Misaada ina madhara, Waheshimiwa pamoja na Watanzania naomba tuelewe hivyo, ukiona unasaidiwa, basi kuna lengo fulani linatakiwa huko. Kwa hiyo sasa hii tuikwepe kwa njia yoyote na napongeza sana kwa kweli jitihada za Mheshimiwa Rais ameliona hilo na ameligungua na ndio maana anakwepa hii misaada ya nje kwa gharama yoyote. Kwa hiyo na sisi tumuunge mkono tuendelee kupigania fedha zetu za ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo kubwa ambalo nimeona pia ni upande wa magereza, naomba nizungumzie kwa upana wake. Lengo la kuweka magereza ni kuwapa mafunzo wale wanaofanya makosa ya aina mbalimbali ili wakitoka nje uraiani waachane na hayo, wafanye mambo mema ili wawe kama raia wa kawaida waweze kujenga Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ambayo naomba niielezee hapa kwa undani, ni jinsi ambavyo magereza yetu pamoja na mahabusu zinavyokusanya wafungwa wa aina tofauti; mwizi wa kuku, mbakaji, muuaji, jambazi sugu, wote wako pamoja wanafungwa pamoja. Si hivyo tu, mwenye miaka 18 ambaye anajulikana huyu sasa ni mtu mzima na kuendelea hadi kufika 30 humo humo ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachokusudia hapa ni hivi, tunawaweka kule ili wapate mafunzo, wakija uraiani wawe watu wema, badala yake mule ndani watoto wetu ambao ni vijana kuanzia miaka 18 ni kijana tunavyosema kwa mujibu wa sharia, wanatoka mule ndani wamebakwa, wamelawitiwa, wanarudi uraiani wameisha hawana nguvu kazi ya vijana, kwa hiyo hilo nalo tuliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tufanye mpango maalum wa magereza yetu kupitia Serikali ili tuone utaratibu maalum hawa wabakaji sugu wawekwe tofauti na watu wengine, wananitia uchungu mimi wanawaharibu watoto wetu vijana. Pia hawa wauaji, majambazi sugu nao wanafundishana vitendo viovu, wanaweza wakawafundisha vijana wetu mambo ambayo yatawajengea uwezo, wakitoka huku nje badala ya kuwa mwizi wa kuku anakua muuaji, kwa hilo jamani naomba sana Serikali itafakari kwa kina kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina pingamizi na hukumu zinazotolewa mahakamani, hata ukija kwenye hiyo money laundering yaani utakatishaji wa fedha, inawezekana yule mtu ambaye amefungwa kwa kutakatisha hizo 300,000, hizo 300,000 zimepatikana labda pengine kwa mafunzo ya ugaidi, kwa mafunzo ya uuaji, kwa hiyo anaweza akafungwa hata miaka sita, hata miaka 10 hata zaidi there is no ploblem. Kwa hiyo hiyo mimi sina pingamizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba upande mwingine nimalizie kwenye challenge ambayo tunayo kwenye mazingira wezeshi ambayo wenzangu wamezungumza na mimi nitumie fursa hii kupongeza uongozi mzima wa Bunge naona jengo letu linakarabatiwa kwa hiyo kutakuwa na lift karibuni na itakuwa ni mazingira wezeshi kabisa kwa wenzetu wenye ulamavu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kwamba sasa Serikali iweze kuona mpango mzuri wa kutekeleza sheria ya mwaka 2010 ili Baraza hili sasa la Watu Wenye Ulemavu liweze kuanzishwa lakini pia na Mfuko wa Maendeleo ambao umekusudiwa kwenye sheria hii uweze kuanzishwa na kuweza kuwasaidia kwa umakini hao wenzetu wenye ulemavu. Suala la mwisho katika upande wa watu wenye ulemavu ni kwamba, halmashauri zetu ziweze kushughulikiwa kwa ukamilifu kuona kwamba ile asilimia mbili inawafikia walengwa kwa wakati mahususi kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hayo natumia fursa hii kukubali hoja hii ya Kamati ya Katiba na Sheria kwa maana ya taarifa nzima kwa upande wa Ofisi ya Makamu wa Rais, sina pingamizi, mambo yanakwenda vizuri, changamoto ndogo ndogo naamini zitafanyiwa kazi, lakini
kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu nao pia nitumie fursa hii kuwapongeza kwa kazi kubwa wanayoifanya kwenye Mifuko ya WCF, OSHA na Taasisi zote zinafanya kazi kuwawezesha wafanyakazi wetu katika hali nzuri kufanya kazi, pia malipo ya fidia nayo yanafanya kazi kwa uzuri, kwa hiyo nitumie fursa hiyo, kama kuna changamoto ndogo ndogo tuzirekebishe. Kwa ujumla wake natumia fursa hii kukubali hoja zote za Kamati kama zilivyo, lakini na kuipongeza Serikali kwa kadri ambavyo wanajitahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)