Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa mwanzo katika hotuba hii Bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na kuweza kusimama hapa. Napenda ni-declare interest mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naanza kwa masikitiko, hotuba ya Mheshimiwa Waziri ambayo naamini maneno yale mengi kama yatatekelezwa ni mwendelezo mzuri na ningependa na ningetamani sana Watanzania waisikie na pia wasikie maoni ya Kambi ya Upinzani ili kuonesha mwelekeo sahihi wa ile kauli ya Rais ya Tanzania ya Viwanda, nilitamani sana. Kwa bahati mbaya sana Bunge hili bado tumeendelea kukaa gizani, tutaambiana sisi kwa sisi, tunaendelea kuambiana haya tuliyoambiana kwenye Kamati, mengi tunayajua.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nifarijike jana tu kwa Wabunge wawili wa CCM, niwapongeze sana kwa kitendo chao kizuri sana walichoionesha jamii ya Watanzania kwamba sisi siyo wapinzani tu tunaopenda haya tunayoyasema hapa kwamba Bunge hili lionekane live. Wao walitumia jitihada ya kupigana picha za video, Mheshimiwa Abuu na Mheshimiwa Aeshi na gazeti la Nipashe likaonesha Watanzania kumbe letu ni moja, lakini tunatofautiana tu kimtazamo.
Mwimbaji mmoja kule Zanzibar aliimba nyimbo akasema kisebusebu na kiroho kiko papo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, haya tuendelee kuambiana katika njia za upole nadhani tutaelewana tu, hakuna haja, muone tu umuhimu wa haya mambo. Mheshimiwa Mwijage leo katika majibu yako ya maswali hapa, kuna raia wangu alinipigia akasema nilitamani nimwone Mwijage kila muda lakini wapi umeyatupa ndugu yangu hulitetei hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba Msemaji wa Kamati, Makamu Mwenyekiti alizungumzia jambo moja zuri. Alizungumzia umuhimu wa biashara na namna Serikali inavyowa-treat watu wanaoingiza bidhaa kutoka nje kutokana na ukadiriaji wa kodi ambazo wakati mwingine tunasema hazina mashiko. Kwa mfano, hivi sasa Watanzania wengi wanafilisiwa magari yao katika Bandari ya Dar es Salaam kwa tatizo moja tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe hukuwepo Bunge la Kumi, nilisimama hapa wakati Waziri wa Fedha akiwa Mheshimiwa Saada Mkuya nikasema ikiwa Serikali mmeweza kuweka Maafisa wa TBS katika nchi tunazochukua bidhaa kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa ubora wa bidhaa, ni kipi kinachowashinda katika suala hili la bei? Kwa sababu nchi ambazo Watanzania tunachukua magari kubwa ni tatu tu hapa duniani, ni Uingereza, Japan na Dubai, wakaweka usahihi wa ile bei ya gari Mtanzania analonunua ili akifika hapa atozwe kodi kulingana na thamani halisi ya gari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa sababu kauli ile ilitoka left hand ikaonekana haifai. Leo Wabunge wenyewe wameonja bakora hii, wameagiza magari, thamani ya gari anavyolinunua akija hapa TRA tayari wameweka bei yao ambayo hiyo ni bei astaghfirullah wameifanya kama bei ya Msahafu maana Msahafu na Bibilia ndiyo ambayo haipingiki. Hii inapelekea watu kuona ugumu kiasi fulani wa kufanya biashara na watu wengi kufilisiwa gari zao zinapofika pale bandarini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naweka msisitizo wa hili, gari aina ya Suzuki Carry inauzwa si zaidi ya dola 500 Japan na ukiingia kwenye mitandao utaziona hizo bei, leo inachukuliwa hata carry ni gari ya anasa? Tungeondoa kutumia wanyama huko vijijini, mkulima mdogo mdogo analima mazao yake badala ya kutumia wanyama na kuokoa muda na kufikisha bidhaa zake katika soko angeweza kununua carry kwa dola 500 akija hapa akalipishwa kwa thamani ya ununuzi na usafirishaji ambayo haizidi dola 800, dola 1500 ikapigwa thamani lakini ukifikisha hicho kigari TRA wanakuambia thamani yake ni dola 2,500. Hii si haki, ni dhuluma na ni aibu sana kwa Serikali kuwadhulumu raia wake, tuliangalieni hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kumekuwa na wigo na maneno mengi juu ya biashara ya magendo baina ya Tanzania Bara na Zanzibar. Yamekuwa yakisemwa njia za panya zimekithiri katika ukanda wa bahari, lakini sababu ni moja. Sababu inayochangia hili ni vikwazo vya wafanyabiashara wa Zanzibar wanapoingiza bidhaa katika soko la Tanzania Bara. Kumekuwa na vikwazo na ugumu mkubwa sana ambao unasababishwa na Mamlaka ya Bandari na TRA Dar es Salaam kuwafanya wafanyabiashara wa Zanzibar watafute njia mbadala.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata katika hali ya kawaida ukimziba mdomo lazima atatoa pumzi kwenye pua. Wafanyabiashara wale wa Zanzibar cha kushangaza TRA ni moja, maafisa wa TRA wanateuliwa na Kamishna Mkuu wanafanya kazi kule Zanzibar, hakuna TRA mbili. Leo hii bidhaa kutoka Zanzibar zinapofika Dar es Salaam zinatazamwa kwa mtazamo hasi na kuonekana ni bidhaa ambazo hazifai kuingia ndani ya nchi yaani zinaangaliwa kwa ukakasi mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na Tume za Pamoja toka miaka ishirini ya Bunge hili kujadili kuondoa vikwazo vya wafanyabiashara wa Tanzania Bara na Zanzibar lakini hili nalo linaonekana ni jipu. Ninukuu usemi wa Mheshimiwa Nahodha, Waziri Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar namheshimu sana kwamba ni jukumu la uchumi mkubwa kusaidia uchumi mdogo. Kwa hiyo, badala ya kuitazama Zanzibar kwa jicho hasi na wafanyabiashara wake lazima sasa muwatazame kwa mtazamo wa huruma na kuwaongoza katika njia stahiki ili biashara ifanyike pasipo na vikwazo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo, nilisema na ninarudia raia wa nchi yoyote jirani ana haki ya kutoka na gari lake akaingia Tanzania, akitumia ruhusa ya kibali maalum kwa kukaa ndani ya nchi karibu miezi mitatu. Hilo kwa Zanzibar limeondoka na halipo, hawezi Mzanzibar kutamani kwenda Mikumi na gari yake na watoto wake ku-enjoy akaingiza gari lile na akapewa permit ya kwamba utakaa miezi mitatu gari kwa sababu labda kodi ya Zanzibar na hapa ina tofauti ukimaliza miezi mitatu urudi Zanzibar, hilo halipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii raia wa Burundi ambaye hayupo kwenye Muungano ataingia na gari lake na ata-enjoy kukaa nchi hii anavyotaka Wakongo halikadhalika. Kwa hiyo, hili nalo ni jambo linalotakiwa liwekewe utaratibu. Wapo wanaoleta magari yao kwa biashara wapitie ule utaratibu wote wa kiforodha na kama kuna makusanyo ya kodi ni sawa lakini anayekusudia kuja kukaa na gari lake katika kipindi kifupi kuna tatizo gani kupewa temporary document ya kukaa hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mbona mkitoka na gari zenu hapa mkiingia kule hakuna kikwazo hiki, kwa nini? Leo hii ukitoka na gari lako Tanzania Bara ukiingia nalo Zanzibar njoo Konde uta-enjoy utaenda kulala under water room kule Jimboni kwangu hakuna tatizo lakini hapa kwa nini? Tatizo ni kwamba …
MHE. KHATIB SAID HAJI: Hatujipambi wakati wa kuolewa twajipamba wakati wa kuachwa.