Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI MHE. GODBLESS JONATHAN LEMA (MB)

Hon. John John Mnyika

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

TAARIFA YA KAMATI YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE KUHUSU SHAURI LA KUDHARAU NA KUDHALILISHA BUNGE LINALOMKABILI MHE. GODBLESS JONATHAN LEMA (MB)

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Wakati Mwenyekiti wa Kamati anawasilisha taarifa na mapendekezo kwa Bunge pamoja na mambo mengine amesema uamuzi huu unalenga kulinda heshima ya Bunge dhidi ya kudhalilishwa, kuzarauliwa na mambo kama hayo.

Mheshimiwa Spika, heshima ya Bunge lolote haiwezi kulindwa kwa kuwafukuza, kuwaadhibu, kuwadhalilisha na kuwahukumu Wabunge wake. Heshima ya Bunge lolote inalindwa kwa Bunge kutumia vizuri madaraka yake na kwetu yamewekwa kwenye Katiba, Ibara ya 63(2) mamlaka ya kuishauri na kuisimamia Serikali, kuwawakilisha na kuwatumikia wananchi, Bunge linalofanya kazi hiyo vizuri ndiyo Bunge lenye heshima kwa wananchi na siyo Bunge la adhabu, siyo Bunge la kudhalilisha. (Makofi)

SPIKA: Nadhani nilisahau kusema muda, kwa kawaida huwa tunatumia dakika tano, tano lakini kwa hili nitawapeni dakika kumi, kumi.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Katika mazingira kama hayo, mapendekezo ya adhabu zilizotolewa na taarifa yote ya Kamati yasikubaliwe na Bunge hili tukufu ili Bunge liachane na haya ambayo kimsingi badala ya kulinda heshima ya Bunge yanazidi kuendelea kudhalilisha heshima ya Bunge, Bunge lijielekeze kwenye kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuko kwenye Bunge la bajeti hakuna….

SPIKA: Unajua unaongea na mimi, sasa ukipandisha sana unakuwa unanifokea, ongea taratibu.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, naongea taratibu na kukuomba kwamba Kanuni 5 ambayo umeapa kuilinda ya Kanuni za Bunge inakutaka wewe Mheshimiwa Spika unapoliongoza Bunge uhakikishe Bunge linazingatia Katiba, Sheria na Kanuni. Kanuni ya 5(3) inakutaka wewe Mheshimiwa Spika pale ambapo ukiona Mbunge amekiuka utaratibu umtake huyo Mbunge anayekiuka utaratibu ajirekebishe. Vilevile Kanuni ya 8(a) inakutaka uendeshe Bunge hili bila chuki wala upendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nini kilitokea? Ndiyo maana nasema, mapendekezo yote ya Kamati yanapaswa kutupiliwa mbali na Bunge.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kumbukumbu za Bunge (Hansard) kwa sababu ya muda sitarejea pale ambapo Mheshimiwa Lema alinukuu taarifa ya Kamati juu ya maneno ambayo Mheshimiwa Mdee aliyasema kuunga mkono kauli ya CAG. Ila nitanukuu kauli aliyosema Mheshimiwa Lema.

Mheshimiwa Spika, baada ya kunukuu maelezo yote hayo, Mheshimiwa Lema akasema, mimi ni Mbunge wa Vipindi viwili, nathibitisha Bunge hili ni dhaifu. Mara baada ya Mheshimiwa Lema kunukuu maneno hayo, Mheshimiwa Naibu Spika, kinyume na kanuni ya 5 (1) ya Bunge, kinyume na kanuni ya 5 (2) ya Bunge, kinyume na kanuni ya 8 (a) ya Bunge akasimama akasema, Mheshimiwa Lema kwa maneno hayo uliyoyasema, nawe unapelekwa kwenye Kamati ya Maadili na ukae na hakuna mchango kwa sababu tunajadili adhabu kuhusu maneno hayo hayo na wewe unasema unayathibitisha. Haya maneno muhimu sana “unayathibitisha.” Nawe utaelekea kwenye Kamati ili ukathibitishe. Nasisitiza “ukathibitishe” vizuri kule.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu Mheshimiwa Naibu Spika alisema ukathibitishe kule; kwa kanuni zetu za Bunge, Mheshimiwa Naibu Spika alipokuwa hapa mezani alipaswa kuongozwa na kanuni ya 63 ya Kanuni za Bunge. Kanuni ya 63 ya Kanuni za Bunge inasema; maana yake hili jambo mlitofautishe kati ya kauli inayotolewa nje ya Bunge na kauli inayotolewa ndani ya Bunge. Kauli zinazotolewa ndani ya Bunge zina kinga ya Kibunge ya Ibara ya 100 ya Katiba, zina kinga ya Kibunge ya Kanuni za Bunge, zina kinga ya Kibunge ya Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukikubali leo Bunge likapitisha azimio la kumwadhibu Mbunge kwa kauli aliyosema Bungeni kwa kumpeleka Kamati ya Maadili bila utaratibu wa kikanuni, mkipitisha utaratibu huu maana yake mmetengeneza mazingira ya Bunge hili la Bajeti linaloanza leo kwa Hotuba ya Waziri Mkuu Wabunge kuminywa mamlaka na haki yao ya kikatiba ya kuishauri na kuisimamia Serikali, ambalo ndiyo lingelinda heshima ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, sasa utaratibu ambao ulipaswa kufuatwa ni upi? Ibara ya 61, 63 (1)(a) inaweka makatazo kwa Mbunge, baada ya hapo, inaeleza nini ambacho Mbunge mwingine angefanya. Siyo Mbunge mwingine angefanya, ndiyo kusema kwamba hicho ulichosema siyo sahihi au ni uongo. Ibara ya 63 (5) inasema: “bila kuathiri masharti ya fasiri zilizotangulia za kanuni hii, Spika au Mbunge mwingine yeyote, baada ya kutoa maelezo mafupi ya ushahidi unaotilia mashaka ya dhahiri kuhusu ukweli wa kauli au usemi au maelezo juu ya jambo au suala ambalo Mbunge amelisema Bungeni, anaweza kumdai Mbunge huyo atoe uthibitisho wa ukweli au kauli au usemi au maelezo yake na kama atashindwa kufanya hivyo, afute kauli au usemi wake.

MBUNGE FULANI: Taarifa Mheshimiwa Spika.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Naibu Spika hakufanya hayo, badala yake…

MBUNGE FULANI: Taarifa.

SPIKA: Nawaombeni leo wala kusiwe na taarifa. Tuwaache waseme, watumie dakika zao 10, na wengine nao watasema, watatumia dakika zao 10. Leo sitaki fujo, anayeleta fujo leo, hamna cha taarifa wala nini. Endelea bwana, dakika zako 10.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kama utaratibu huo ungefuatwa, maana yake ama Mheshimiwa Lema angetakiwa afute kauli, au angetakiwa athibitishe hapa Bungeni. Kama angeshindwa kuthibitisha, utaratibu wa adhabu ambao ungefuatwa uko kwenye kanuni ya 63 (9) ambapo adhabu pekee zilizotajwa kama ni kosa la kwanza, vikao visivyozidi 10 kama ni kosa la pili, vikao visivyozidi 25 na kadhalika. Adhabu zimetajwa hapa.

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa adhabu ungekuwa tofauti na ilivyopendekezwa na Kamati, asingesimamishwa mikutano mitatu kwa mapendekezo mnayotoa ambayo ni kinyume kabisa na utaratibu, isingekuwa namna hii na utaratibu usingekuwa hivi.

Mheshimiwa Spika, sasa nasimama kusisitiza hili na nayasema haya na naomba taarifa ya Kamati isikubaliwe. Kwa sababu kama taarifa ya Kamati ikikubaliwa; Mheshimiwa Lema alikata rufaa baada ya uamuzi wa Naibu Spika kabla Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge haijakaa. Alitumia haki ya kikanuni, kanuni ya 5 (4) akapeleka taarifa ya rufaa kwa Katibu, kama kanuni inavyosema, akaeleza nimesema hoja moja tu ya kasoro za jambo zima kama nitakuwa na muda nitakwenda kwenye nyingine, alikuwa na hoja tatu; akakata rufaa kabla. Akaenda mbele ya Kamati ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge akaiambia Kamati, nimekata rufaa ipo kwa Katibu, nakala ya rufaa hii hapa. Kamati ikasema hatujapokea rufaa, hatuko tayari kuipokea kutoka kwako, sisi tunaendelea mbele. Kimsingi Kamati ilikuwa imesha-shape uamuzi.

Mheshimiwa Spika, kwa misingi ya haki, kwa kauli zako za jana tayari ulishatoa hukumu kabla ya Kamati kufanya kazi. Huu mchakato mzima ukiendelea, ni mchakato ambao ni batili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama uamuzi ukishafanywa na Bunge, hakuna mahali popote pengine pa kukata rufaa isipokuwa Mahakamani na Mahakama inaminywa kwa Sheria ya Kinga Haki na Bunge kushughulikia mambo ambayo yameamuliwa na Bunge. Sasa kama tukipitisha huu uamuzi leo, maana yake tuna-pre-empty Kamati ya Kanuni. Tuahirishe hii taarifa isijadiliwe kabisa, Kamati ya Kanuni ikakae kwanza kabla ya uamuzi wa Bunge ili taratibu za kikanuni zifuatwe.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, nijielekeze kwenye eneo lingine haraka haraka. Amehukumiwa kwa kosa la kudharau Bunge wakati siyo kosa lake. Kwa kosa hilo, Ibara ya 33 kifungu cha 33 (1) cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kinasema: “Where any member commits any contempt of the Assembly whether specified in section 26 or otherwise, the Assembly may, by resolution, either direct Speaker to reprimand…” ungeweza wewe mwenyewe Spika kuamua kumwonya, kungeweza kuwa na adhabu ya onyo, lakini naendelea mbele. Kwa hiyo, kama Spika ukiamua kuondoa misingi yoyote ya mazingira ya kuonea au nini, unaweza kumpa onyo tu.

Mheshimiwa Spika, sentensi inaendelea, kama ukiamua kutoa suspension: suspend him from service of the Assembly for such period as it may determine. Sheria inaendea mbele inasema, sikilizeni: “provided that, such period shall not extend beyond the last day of the session next following that which the resolution was passed or of the session in which the resolution is passed as the Assembly may so detrmine.”

Mheshimiwa Spika, sheria imeweka ukomo wa kiwango cha adhabu kinachoweza kutolewa. Ninyi taarifa yenu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika ninyi taarifa yenu ya Kamati imekiuka sheria, imekiuka Katiba, imekiuka mambo yote ya msingi isikubalike.

SPIKA: Mheshimiwa Mnyika ahsante sana.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Kwa sababu mko wengi na mmeshaamua, kama mnataka kuamua, ninyi muamue kwenye Mahakama ambayo ninyi wenyewe ndio walalamikaji, ninyi wenyewe ndio watoa hukumu na kila kitu Mheshimiwa Spika na hatimaye mtaendelea kulidhalilisha Bunge kwa haya mnayoyafanya.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kama muda wangu umeisha. Kama bado, niendelee.