Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makambako
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nami niungane na wenzangu kukushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu.
Mheshimiwa Spika, nianze na jambo ambalo limezungumzwa sana jana leo na tangu huko nyuma kuhusu udhaifu wa sisi Wabunge.
Mheshimiwa Spika, hawa wenzetu upande wa pili, katika bajeti ambazo tumekuwa tukipitisha hapa hawajawahi kusema ‘ndiyo’ hata mara moja. Kwa maana hiyo, wanataka kutuchelewesha kwa kazi nzuri zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. Kazi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na Waziri Mkuu na Mawaziri pamoja na wewe mwenyewe Spika ambaye unatusimamia kuisimamia Serikali, ni kazi nzuri sana. Kwa hiyo, tunaipongeza sana Serikali kwa namna ambavyo Waziri Mkuu amewakilisha hoja iliyoko mbele yetu.
Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo, nianze kwa kuishukuru Serikali kwa namna ambavyo kwenye Jimbo langu la Makambaku, kwa namna ambavyo wananchi wangu wamekuwa wakilia juu ya kulipwa fidia kwa Soko la Kimataifa zaidi ya miaka 18; mwaka 2018 kupitia Ofisi hii inayosimamiwa na Mipango na Waziri, amelipa fidia zaidi ya shilingi bilioni tatu na kitu. Natoa shukrani sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi langu ni kwamba kuna baadhi ya watu kumi na kitu hawakuwepo wakati wa uhakiki, naomba sana watu hawa walipojitokeza watu wa uhakiki walikuwa wameondoka. Kwa hiyo, naomba waweze kuhakikiwa ili nao waingie kwenye kulipwa fidia.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili naiomba Serikali, kuna eneo pale pale Idofyu kuna mpango wa kujenga one stop center, sasa napo tunahitaji wananchi wale kulipwa fidia. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, kwenye mpango huu iweze kuwalipa fidia wananchi wangu wa Makambaku.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, naishukuru Serikali kwa suala la umeme awamu ya tatu. Kwenye Jimbo langu natoa shukrani kubwa sana, najua na Watanzania wenzangu, Waheshimiwa Wabunge wenzangu ni hivyo hivyo. Napongeza sana kwa namna ambavyo wananchi, wameweza kupata umeme katika maeneo yote ya Jimbo langu la Makambaku.
Mheshimiwa Spika, ombi kwa Serikali, kuna kijiji kinaitwa Mtanga ambako umeme umefika kule Kifumbe, pale ni kilometa tano, kimebaki peke yake; naiomba Serikali iwapatie umeme ili nao waweze kufaidi kama ambavyo wenzao wanafaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vile vile niishukuru pia Serikali kwa namna ambavyo imeweza kutupa fedha katika vijiji kadhaa kwa ajili ya suala la maji. Kwa kweli naishukuru sana. Ombi, tunataka kujua, fedha hizi za mkopo nafuu kutoka India ni lini mradi huu utaanza ili wananchi wa Makambaku waweze kufaidika na mradi huu mkubwa ambao utatatua changamoto kubwa kabisa ya maji iliyopo katika mji wetu wa Makambaku na Kijiji cha Ikelu?
Mheshimiwa Spika, mimi nimekuwa Diwani kwa miaka 10. Mpango wa afya kwa namna ambavyo Serikali imetoa fedha nyingi kwenye Vituo vya Afya, nami ni mmojawapo nimepata. Kwa hiyo, naishukuru sana Serikali kwa dhati kabisa. Vile vile tumepata fedha kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Rufaa ya Halmashauri ya Mji wetu wa Makambaku, shilingi 1,500,000,000/= na hivi tunakwenda vizuri, naishukuru sana Serikali kwa kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi, tuna Kituo cha Afya ambacho tulikuwa tunakiita Hospitali ya Mji wa Makambaku, tupate X-Ray kwa ajili ya huduma mbalimbali katika mji wetu wa Makambaku. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, upande wa TARURA tunakwenda vizuri. Tunaiomba Serikali iongezee fedha upande wa TARURA ili barabara zinazounganisha baadhi ya kijiji na kijiji ziweze kupitika vizuri. Naomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana anayehusika; Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Rais mgombea wakati ule 2015 tuliahidiwa kilomita sita za lami katika Mji wa Makambaku. Mpaka sasa zimetengenezwa mita 150. Ombi langu ni kwamba barabara hii ya kilomita sita iweze kutengenezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kilimo. Amezungumza Mheshimiwa Vuai Nahodha hapa; suala la kilimo ni asilimia kubwa sana ya wakulima wetu na mbolea ambazo wanazipata ziko bei juu, haziwiani na mauzo ya mazao yanayozalishwa. Nini kifanyike?
Tunaiomba Serikali ione namna ya kusimamia bei ya pembejeo ili ziweze kupungua ziendane na uzalishaji wa kilimo, lakini vilevile tunaiomba Serikali ilete wawekezaji kwa ajili ya kujenga Kiwanda cha Mbolea ili mbolea hii iweze kuwa bei chini na izalishwe nchini kwetu hapa hapa.
MBUNGE FULANI: Kweli.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, jambo lingine, tuna maboma ya Zahanati kwa nchi nzima. Kwangu peke yake kuna maboma ya zahanati zaidi ya 13 katika vijiji. Tunaiomba Serikali, katika mwaka huu wa fedha wa 2019/ 2020 angalau ione namna ya kutoa fedha nyingi ili maboma haya yaweze kupungua. Kila Jimbo angalau maboma matano au mangapi, tukifika 2020/2021 tunaweka tena bajeti maboma haya tutakuwa tumeyamaliza. Kwa hiyo, ombi langu ni kwamba Serikali iongeze fedha kwenye maboma haya.
Mheshimiwa Spika, nilisema hapa kipindi kilichopita na leo naomba nirudie; mwenzangu amesema kwamba kiongozi wetu, Rais wetu ana maono makubwa sana, wote hapa tunakubaliana. Mipango hii mizuri iliyowekwa, nilisema hapa kwamba huyu anatakiwa aombewe awe Rais wa kudumu kutokana na mipango aliyoifanya. Sasa kama siyo hivyo, basi ili mipango hii iweze kukamilika vizuri, tuombe angalau aongezewe kipindi kimoja mpaka 2030 ili mipango yake aliyoipanga iweze kukamilika vizuri. Kama ni hivyo, mimi na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, 2021 tutatembea nchi nzima, mimi nitakuwa wa kwanza kuwaambia Watanzania tumwombee aongezewe kipindi kingine ili akamilishe mipango na ndoto zake nzuri za maendeleo kwa Watanzania.
Mheshimiwa Spika, wewe mwenyewe ni shahidi, hata kwenye Jimbo lako unaona namna ambavyo shughuli mbalimbali zinavyofanyika ikiwepo barabara, Vituo vya Afya, na kadhalika. Kwa hiyo, tunaiomba sana Serikali na hasa Waheshimiwa Wabunge, tutakapofika 2021 tuanze kutembea kuwaambia Watanzania, kwamba tumwongezee kipindi kingine ili ndoto zake ziweze kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wenzetu hawa ambao sasa wametoka humu ndani, watakuja tena hapa, watapinga hii bajeti ambayo tunaijadili hapa, lakini kwenye Majimbo yao wanahitaji huduma mbalimbali. Kwa sababu Rais wetu alisema maendeleo hayana chama, basi wananchi wapelekewe maendeleo, lakini isingekuwa hivyo, hawa walitakiwa walambwe na viboko kabisa. Kwa sababu wamekuja hapa kuwakilisha kwenye Majimbo yao… (Kicheko)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Sanga.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ahsante sana. (Makofi)