Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Peter Ambrose Lijualikali

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi hii. Sikuwa nimepanga kusema haya maneno, lakini nitasema kidogo. Kwa kweli ni jambo ambalo linasikitisha sana kuona katika Bunge letu kuna Wabunge wana mawazo ya kufanya Rais aliyeko madarakani aendeleze kipindi ambacho kipo katika Katiba.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli ni jambo ambalo kama tunaweza kuruhusu Katiba yetu ianze kufanyiwa marekebisho makubwa kama haya na kama haya ndiyo mawazo ambayo tunayo, yaani CCM wote ninyi mlioko humu ndani na nje, yaani hamjaona mtu mwingine Tanzania nzima, kwa kweli ni masikitiko makubwa sana.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Kwa hiyo, kwa kweli ni jambo la fedheha. Mimi binafsi nimesikitika sana.

MBUNGE FULANI: Haukuwa mpango.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Aah, kwa sababu hata huo nao haukuwa mpango na alisikika, kwa hiyo, ni vyema mkanisikiliza tu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati anaongea, alizungumzia maendeleo mengi, mipango ya Serikali ambayo inafanywa na kwenye Sekta ya Barabara ya miundombinu akaizungumzia barabara yangu ya Ifakara Kidatu kwamba inaendelea vizuri na katika moja ya vipaumbele vya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, hii barabara ya Ifakara – Kidatu, jambo la kwanza ni barabara ambayo inafadhiliwa na wafadhili mbalimbali na tayari mikataba yake imeshasainiwa na fedha zipo. Rais mwaka 2018 alikuja kule Ifakara, Kidatu akazindua, akaweka jiwe la msingi, lakini hii barabara ni kama vile haifanyiwi kazi.

Mheshimiwa Spika, site yupo Mkandarasi, ni kweli, lakini huyu Mkandarasi ni kama hafanyi kazi yoyote, amekaa tu, analalamika fedha hapati, mambo hayaendi, mizigo yake na vifaa vyake viko kule Bandarini. Akiomba vitoke anaambiwa alipe kodi.

Mheshimiwa Spika, Bunge la mwezi wa Pili, Bungeni hapa niliuliza swali nikamwomba Mheshimiwa Waziri anayehusika twende Ifakara, Kidatu akaangalie maendeleo ya ile barabara na kwa nia, nami niliona kabisa alikuwa na nia njema akasema tutakwenda mbele ya kiti chako, wananchi wakasikia, Taifa likasikia, lakini ukimpigia simu hapokei, ukimtumia message hajibu. Sasa hii maana yake ni nini?

Mheshimiwa Spika, ukimwangalia Rais Dkt. Magufuli, ukiwa makini ukamsikiliza vizuri, analalamika sana. Huyu Rais wetu amekuwa Rais wa kulalamika. Tena imefikia hatua analalamikia mpaka Mawaziri. Juzi hapa alisema Mawaziri ham-communicate. Sasa hii maana yake nini?

Mheshimiwa Spika, sasa mimi nafikiri labda sijui kuna kitu Mheshimiwa Rais watu wanamtegea hawamuungi mkono, kwa sababu kama tuna Mheshimiwa Waziri anakubali atakwenda Jimboni kwenda kutekeleza kitu ambacho Rais wake alikwenda tena nchi nzima ikawa live kwenye TV, watu wote wanaona kabisa, Mheshimiwa Rais anasema kabisa, “natoa miaka mitatu barabara hii iwe imeisha” na akasema fedha zipo.

Mheshimiwa Spika, mimi nasema kule kazi haziendi, Mheshimiwa Waziri anakiri kwamba twende tukaone. Mheshimiwa Waziri hapokei simu, hajibu message, anaingia mitini. Maana yake nini? Sasa sijui ni kumgomea Mheshimiwa Rais, sijui ni maneno ya kampeni tu, sijui maana yake nini?

Mheshimiwa Spika, kama tunataka kweli kukomboa Taifa letu, kuna vijitabia kama hivi lazima tuviache. Sisi ni viongozi humu ndani, tabia hizi nami niseme kabisa kutoka moyoni, mimi Rais Dkt. Magufuli namwonea huruma sana. Mheshimiwa Spika ni shahidi, Rais Magufuli kila anaposimama ni kulalamika, anasema Wizara hii, Wizara hii, jambo hili, jambo hili, hili niliagiza, hili nilisema, hili nilisema, watu wote hawa hivi Rais wenu hamumpendi, mbona analalamika sana, ninyi manafanya kazi gani, mbona hamsaidii? Kila siku ni kulalamika tu yaani vitu ambavyo anatakiwa alalamike Mbunge, analamika Rais, mpo Mawaziri, kuna Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya wote mpo. Nyie Magufuli hamumpendi ila tu hamsemi ukweli, kama mnapenda kwa nini hamumsaidii?

Mheshimiwa Spika, niombe, kama fedha za barabara hii hakuna mseme, hizi fedha hakuna, kama fedha zimeenda kwenye Stiegler’s Gorge mseme, zimekwenda Stiegler’s Gorge, kama zinafanya kazi mseme, watu wa Ifakara, watu wa Kilombero, watu wa Kidatu, watu wa Mkula, watu wa Sanje tumechoka. Tunahitaji barabara hii ijengwe, kama fedha hakuna mseme, sisi tumechoka jamani, mbona nyie mna raha, mnakaa kwenye lami sisi tumewakosea nini? Kwa upande huu nilikuwa na hili.

Mheshimiwa Spika, ukija kuangalia kwenye Wizara ya Kilimo, nimeangalia randama ya kilimo, lakini fedha ya pembejeo, hakuna. Rais Dkt. Kikwete ameondoka madarakani kwenye bajeti ya 2015/2016 aliweka bilioni 78, bajeti hii kwenye randama ya Wizara ruzuku ya pembejeo nil, hata mia hakuna, yaani wanataka kuwaambia Watanzania kile ambacho Rais Kikwete alikifanya wao kwa miaka miwili wameshindwa tayari, yaani wameshashindwa. Mwaka 2016/2017 asilimia 89 ya bajeti ya Kilimo haikutoka, wamepeleka only 11, halafu sasa wanahuburi nchi inakwenda mbele, nchi inasonga, pembejeo tu zimewashinda, wataweza kweli.

Mheshimiwa Spika, kama Rais wetu hawamsaidii kumwambia ukweli kwenye haya mambo, hii nchi ilipofikia inategemea with due respect tunaongea hapa unasikia sauti za kunikejeli, is not fair, sisi tukifanya vitu kama hivi kidogo tu kama hivi toka nje, ondoka, lakini Msukuma na mwenzake wanaongea kejeli kabisa, as if mimi hapa naongea ujinga, lakini kwa sababu mnasema nchi ni ya kwenu, lakini nataka niwambie jambo moja CCM, hamtakaa hapa milele, hamtakaa milele, mtatoka na tutawatoa…

SPIKA: Mheshimiwa Lijualikali kidogo tu, utaratibu wa humu ndani unaongea na mimi, wewe hao usiwasikilize, wewe niambe mimi tu, utajikuta hugombani nao, endelea kuchangia ili dakika zako zisipokee.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, naongea na wewe na hata sisi wakati tunaongea na wewe, watu wanapofanya mambo kama haya, wewe unatakiwa unilinde, ni haki yangu kuwaambia wanyamaze niseme, lakini wewe kuwaachia is not fair.

SPIKA: Sasa nimekupa nafasi ya kusema na unapaswa kusema na mimi, badala lake unanifokea, unanifundisha si ndio hapo tunapokosana na ninyi ndugu zangu. Wewe umepewa nafasi changia hiyo bajeti, ongea na mimi usisikilize watu wangine, wewe ongea na mimi.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika ninachosema ni kwamba kama unahisi, kama unafikiri…

SPIKA: Hivi ngoja nikwambie, unajua kwenye Bunge hubishani na Spika mnafahamu, ndio haya yanafanyika, kujua kwingi ndio tatizo, yeyote anayesimama hapa anaongea na Spika. Ongea na Spika kama una cha kuongea, kama huna cha kuongea, pumzika.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika naomba unisamehe kama ambacho nimekiongea, unadhani kwamba nimekufokea au nimekusema, sio lengo langu wala sio kusudi langu. Naomba unisamehe kwa hilo, lakini ambacho mimi namaanisha, naomba kwamba mtu anapoongea watu wote tuheshimiane. Hilo ndio ombi langu, naomba hili litusaidie ili twende vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilikuwa nasema, ruzuku ya pembejeo 2000 kwenye randama ya bajeti ya Wizara ya Kilimo, inaonekana ni nil, haipo. Mheshimiwa Rais Dkt. Kikwete aliondoka akacha bilioni 78, sisi miaka miwili tu ya Rais Magufuli akiwa madarakani, miaka miwili tu, wameshindwa kutenga bajeti ya pembejeo, maana yake wanawaambia wakulima kule mtaani, wapambane wenyewe. Sasa huko mtaani ajira hakuna, vijana hawajaajiriwa kwa 98%, kitu pekee labda ambacho kingeweza kuwasaidia kilikuwa ni kilimo na utaratibu wa nchi ulitenga ruzuku, wao wametoa, hawa watu wanafanya kazi gani?

Mheshimiwa Spika, wanasema wanakwenda katika nchi ya viwanda, sijui nchi ya nini, mimi nimeangalia style nyingi, wakati wenzetu wanafanya revolution za uchumi, walianza na agriculture revolution, walianza kupata kwanza mazao, kilimo kikaimarishwa ndio viwanda vikaja, sasa kilimo kinakufa, wategemee kutakuwa na viwanda, vitatoka wapi? Hivyo viwanda vita-feed kitu gani? Yaani unakuwa na kiwanda cha nini kama hakuna raw materials na lazima kuwa na mkakati wa nchi. Kuna siku nilisema hapa development lazima kwanza ingalie watu na 89% au 80% ya Watanzania wapo kwenye kilimo.

Mheshimiwa Spika, katika jambo ambalo naamini lilikuwa zuri ambalo pengine lilifanyika, ile sheria ambao tuliipitisha hapa ya tani moja kwa mkulima apite bila ushuru, wale wakulima wadogo kabisa, nilijua kwamba itakomboa na sincerely kabisa naamini hivyo, lakini ukienda field wakulima hawa wanafanya nini? Wanafanyiwa nini, ni kweli kwamba ile tani moja wakipita hawatozwi ushuru? Ni kweli unakuta wakulima wanatozwa ushuru, vibibi, vimama, ambavyo wanalima heka moja, heka mbili kupata substance, tumetunga sheria hapa Bunge ya kazi gani? Rais Mheshimiwa Dkt. Magufuli alikuja Ifakara, nilimwambia kwamba Rais ile sharia, ile amri yako hapa haitekelezeki, akasema marufuku nchi nzima, nini kinafanyika? Wakuu wa Mikoa wapo, Mawaziri wapo, Wakuu wa Wilaya wapo, Serikali ipo, as if hamna mtu anayeona, yaani hatuumii.

Mheshimiwa Spika, jana ulisema hapa Lema alipata mkopo milioni mia sita na ngapi, ni kweli kapata kwa sababu hiyo ni haki yake, hawa wakulima wa nchi hii wanapata nini? Mbona hatuwapendi?

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya nashukuru na Mungu akubariki, uendelee vizuri, ufanye kazi zako vizuri, ingawa Mwenyekiti wangu wa chama leo hakufanya kazi yake hapo ya kuwasilisha bajeti yetu ya Kambi, lakini kwa sababu alitoka Bungeni na wewe ukatoa ile amri yako, lakini anasikitika sana. Nashukuru. (makofi)