Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwimba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MANSOOR S. HIRAN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru umenipa nafasi na mimi nisimame leo Bungeni hapa nizungumze. Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa afya niweze kusimama kwenye Bunge hili Tukufu kuzungumza kuhusu hoja ambayo iko mbele yetu.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri ya bajeti aliyowasilisha leo asubuhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kutoa mchango wangu, naomba nipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri sana ambayo inaifanya. Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imesema mambo mengi sana, naomba nipongeze mambo machache. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, naomba nipongeze Serikali kwa maamuzi ya kujenga reli ya kisasa ambayo ni ya historia, kwa Afrika nzima itakuwa ni reli ya kwanza ambayo inatumia umeme. Pili, ni Surrender Bridge ambalo ni kero kubwa kwa wananchi kwa sababu ya msongamano wa magari. Kwa kweli hilo daraja pia litapunguza msongamano wa magari. Mambo mengi sana yamefanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, tuna mradi wa Stigler’s Gorge na sera ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala ambalo nitalichangia hapa ni ajira. Nchi yetu tuna changamoto kubwa sana ya ajira. Jimboni kwangu hata nchi nzima tuna changamoto ya ajira ni za aina mbili. Jimboni kwangu Wilaya ya Kwimba changamoto ya ajira ni kwanza ya wale vijana wanaomaliza form four ambao wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu hakufaulu kwenye mtihani wake au hana uwezo wa kuendelea na masomo. Changamoto nyingine ni wale ambao wamepata digrii, wamesoma mpaka chuo lakini hawana ajira. Kwa hiyo, kuna aina mbili ya vijana ambao hawana ajira.
Mheshimiwa Spika, changamoto ya ajira ni kubwa sana, natambua Serikali ina mipango mingi kupunguza kero ya ajira lakini kero ya ajira Jimbo la Kwimba ni kubwa sana. Mara nyingi utaona ajira zinatangazwa kwenye Mikoa na Miji mikubwa, vijana wa Jimbo la Kwimba hawana uwezo wa kufuta ajira hizo kwenye Miji mikubwa wanabaki pale pale, wanadumaa hawana pa kwenda.
Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali ingefanya utaratibu wa kuwa na mpango mkakati wa kusaidia vijana vijijini ambao hawana uwezo wa kwenda mijini kutafuta ajira. Tuwe na mpango mkakati ambapo kuna mambo mawili, nashauri Serikali itusaidie Jimbo la Kwimba. La kwanza, tuna maombi ya miaka mingi sana tujengewe Chuo cha VETA. Vijana wengi ambao wanafeli masomo na kurudi nyumbani hawana pa kwenda kusoma wangeenda kwenye Chuo cha VETA, wangepata ufundi na wangejiongezea ujuzi wakajiajiri wenyewe wakasaidia familia zao. Hiyo ni kero kwa wananchi wa Jimbo la Kwimba ya miaka mingi sana. Eneo lipo, tunaomba Serikali itufikirie itujengee VETA itapunguza kero ya ajira kwenye Wilaya ya Kwimba.
Mheshimiwa Spika, pili, tuna utaratibu wa kutoa asilimia 10 kutoka Halmashauri kwa ajili ya vijana, akina mama na walemavu hizo fedha hazitoshi hasa kwa sisi Wilaya Kwimba kwa sababu mapato ya Halmashauri yetu si kubwa sana. Ukiangalia Mkoa wa Dar es Salaam wana mapato ya shilingi bilioni ya 12 kwa vikundi vya akina mama, vijana na walemavu, sisi Wilaya ya Kwimba hatufiki hata shilingi milioni
300. Ukiangalia ukubwa wa Wilaya ya Kwimba ambayo ina majimbo mawili vijana ni wengi sana wanatafuta mitaji lakini mitaji ambayo inatoka Halmashauri haitoshi.
Mheshimiwa Spika, naomba Serikali itafute mikakati mingine ya kutafuta mitaji ya kusaidia vijana ambao wako vijijini kupata mikopo ili waweze kufanya biashara. Kusubiri fedha za Halmashauri ni ndogo sana, hazitoshelezi mahitaji ya wananchi au vijana wa Jimbo la Kwimba.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni changamoto ya maji. Jimbo la Kwimba tuna matatizo mengi sana ya maji. Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka jana alifanya ziara kwenye Jimbo la Kwimba, aliagiza Serikali ya Wilaya na Mkoa kwamba kuna Mradi wa Maji wa Kijiji cha Shilima ambao unategemea kupeleka maji kwenye vijiji takribani 14, kata takribani tatu kwamba ukamilike ndani ya miezi mitatu lakini mpaka sasa maagizo ya Mheshimiwa Waziri bado hayajatekelezwa. Kwa unyenyekevu mkubwa Watendaji wananisikia, maagizo ya Waziri Mkuu hayajatekelezwa, naomba angalau wafuatilie ili yatekelezwe.
Mheshimiwa Spika, kwenye masuala ya afya, nashukuru Serikali kwenye Kituo chetu cha Afya cha Mwambashimba tumeletewa shilingi milioni 400, tumeongeza majengo matano, sasa hivi tutakuwa na Ultrasound na majengo ya mama na watoto. Naomba nichukue nafasi kuishukuru sana Serikali kwa mradi huu wa kuboresha kituo cha afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho naomba Serikali kwenye Wilaya ya Kwimba, Makao Makuu yetu ambayo ni Ngudu tuna Hospitali yetu ya Wilaya ambayo ilianzishwa kama Kituo cha Afya lakini tunakitumia kama Hospitali ya Wilaya tuna changamoto ya X-ray. Tuna X-ray ambayo ni ya zamani sana ambayo inatumia gharama kubwa sana na kila mara inaharibika na ni analog, tunaomba tupate X-ray ya kisasa ili tuweze kutoa huduma nzuri kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika, pia Hospitali yetu hiyo ya Wilaya hata mashine ya kufua nguo haina, tuna watumishi wanafua mashuka kwa kutumia mikono. Sasa kwenye Hospitali ya Wilaya mnaosha shuka kwa kutumia mikono kwa kweli sidhani kama inaweza kuwa ni salama.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia na naunga mkono hoja. (Makofi)