Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

Hon. Raphael Michael Japhary

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji

MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kushukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia. Pia niipongeze sana hotuba ya msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa namna ambavyo ipo katika mtazamo wa kuisaidia Serikali kuboresha mpango wake wa kuifanya Tanzania ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maeneo machache ya kutoa mchango wangu. Mpango wa kuifanya Tanzania kuwa ya viwanda ni mwema na maombi yetu sote tufikie hapo. Lakini mashaka yangu mimi ni sababu zilizotusababisha tukashindwa kufikia hapo siku za nyuma. Kwa sababu miaka ya 80 tulikuwa tunaenda vizuri, ni kizungumkuti gani kilituingia mpaka tukaamua kuruhusu mipango isiyo mizuri ambayo imelifikisha Taifa hapa mpaka leo ndiyo tunaanza kutafakari namna ya kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Hofu yangu ni kwamba inawezekana mpango huu wa Serikali ukawa ni mpango unaosikika vizuri masikioni lakini bado ukawa na shida katika utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni nini ambavyo tunavikosa katika Taifa hili? Ukiangalia Serikali ya Awamu ya Tano inafanya kazi kama vile Serikali imeanguka leo, haikuwepo tangu huko nyuma, kama vile ni chama kipya kimeanza kutawala Taifa hili wala sio Chama cha Mapinduzi kilichokuwa kinatawala. Kwa hiyo, hakuna muunganiko kati ya mfumo wa Serikali iliyopita na mfumo wa Serikali inayofuata sasa ambao ungesaidia kujua ni mabaya yapi mnayaacha, ni mazuri yapi mnayapokea. Matokeo yake kila mtu anakuja na mtazamo kama vile anataka kuizaa Tanzania leo wakati Tanzania ina miaka 50 tangu imeitwa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hofu yangu kubwa ni consistency ya government. Hiyo ndiyo inanipa mashaka kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kutofikia hii mipango yote ambayo tumeipanga. Mimi ukiniuliza leo ningekuambia kilichokosekana katika Serikali zilizopita, ya Awamu ya Tatu na ya Nne ni dhamira na uzalendo kwa viongozi waliopewa dhamana, ndicho ambacho ningekujibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa msingi huo kama Rais wetu kweli ana dhamira na kama Waziri wa Viwanda leo alivyotoa hotuba yake kweli ndiyo dhamira yake hivyo ana wajibu wa kuhakikisha kwamba anaambukiza hiyo dhamira kwa watu wote wanaomzunguka ili Tanzania ifike hapo inapotaka kufika kuwa Tanzania ya viwanda. Kama hatutaweza kuibadilisha culture ya rushwa, ubadhirifu na ufisadi zilizopo katika Taifa hili hizi zitakuwa ni nyimbo na ngojera ambazo zitaimbwa kila mwaka na hatufiki popote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nachoshauri ni kwamba Serikali ijiandae katika hilo, kwanza kwa kubadilisha utamaduni wa watendaji wetu wa kuliibia na kuliumiza Taifa ili kidogo tunachokipata sasa tukielekeze kwenye maendeleo. Nina hakika tukifanya hivyo tunaweze kufika mahali fulani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utangulizi huo, nataka niongelee suala la wafanyabiashara kama wenzangu waliotangulia walivyosema. Taifa hili bado halijaonyesha kiukweli, kama maneno nitakayotumia siyo mazuri sana lakini nadhani hivyo kwamba Taifa hili bado halijaonyesha kiukweli kwamba lina haja ya kuwasaidia wafanyabiashara wake wa ndani, bado halijaonyesha kwa dhati. Ndiyo haya unasikia mambo ya kodi watu wanapoingiza mali lakini hata wafanyabiashara wa ndani mazingira yao waliowekewa vikwazo vyao vimekuwa ni vingi sana kiasi kwamba uwezo wa wafanyabiashara hawa kufanya kazi yao vizuri wakawa ni sehemu ya wawekezaji muhimu katika Taifa hili umekuwa ni mdogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wakati tumejikuta tunathamini wawekezaji wa nje kuliko wa ndani, siyo jambo baya lakini siyo vizuri kushindwa kuwatengenezea fursa na mipango mizuri wafanyabishara wa ndani ili waweze kuwa wawekezaji ambao wana uhakika kuliko wawekezaji wa nje na watakaohakikishia Taifa hili kubaki na pato lake la ndani na uchumi wake kukua kwa haraka sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu kwa Serikali ni vizuri tuhakikishe tunaondoa vikwazo kwa wafanyabiashara wetu wa ndani, tozo zimekuwa nyingi mno. Leo ukiuliza hivi ni kwa nini bado corporate tax ni kubwa kwa wafanyabiashara hakuna majibu ambayo ni ya msingi sana. Ukiuliza kwa nini VAT bado ni kubwa kwa wafanyabiashara hakuna jibu ambalo ni la msingi sana. Kanuni mojawapo ya kodi ni kuwa na compliance ili mfanyabiashara aweze kulipa kodi hiyo. Sasa leo kodi inatumika kumfilisi mfanyabiashara, anaingia kwenye uchumi kesho, kesho kutwa anafilisiwa na kodi na anafilisiwa na Watanzania wenzake halafu mnakwenda kufikiri kuwaneemesha watu wa nje waje kuwekeza wakati mnashindwa kuwawezesha wafanyabiashara wa ndani wakafanya vizuri maana yake ni kwamba hamsaidii wafanyabiashara wenu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo pamoja na jitihada ya kuvutia wawekezaji wa nje ni vizuri tusaidie wafanyabiashara wetu wa ndani ili wafanye biashara zao vizuri. Hebu tuangalieni tax regime yetu kama ipo sawa sawa na inawasaidia wafanyabiashara wa ndani? Kodi ya Taifa hili imekuwa ni kikwazo kikubwa kwa wafanyabiashara. Leo katika nchi hii mfanyabiashara akimuona mtu wa TRA ni afadhali amuone simba kwa jinsi ambavyo muda wote anafikiri kufilisiwa. Bahati mbaya Serikali inajenga taswira hasi kwa wafanyabiashara kwamba wote ni wizi, ndiyo inavyoonekana hivyo, hakuna wakati maafisa wa TRA wamekuwa tayari kuamini taarifa halisi za wafanyabiashara na ndiyo maana leo unasikia gari inanunuliwa nje shilingi dola 500 inakuja kuchajiwa kodi ya dola 2,000 kwa sababu ya kutoamini wafanyabiashara. Nadhani ni muhimu sana kuangalia eneo hili kama tuna dhamira ya kuwafanya wafanyabiashara hao wawekeze katika sekta ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niongelee suala la sekta isiyo rasmi. Kama Mheshimiwa Waziri alivyoonyesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha anasaidia viwanda vidogo, vidogo sana na vya kati na wafanyabiashara wadogo sana na wa kati, ni lazima sekta hii ipewe kipaumbele. Kipaumbele nachozungumzia siyo kwa maneno ya kisiasa, siyo kwa kuzungumzia habari ya asilimia tano ya Halmashauri kwa akina mama ambayo haipatikani, ni lazima tujenge mkakati rasmi wa kuhakikisha kwamba tunatengeneza mazingira ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo katika Taifa hili Mheshimiwa Rais anasema wafanyabiashara wadogo wasibugudhiwe, wasisumbuliwe katika Halmashauri zao lakini huko chini Wakurugenzi wanasumbua wafanyabiashara hao. Ni lini wafanyabiashara hawa wataweza kwenda mbele? Rais anatoa maagizo, huko chini maagizo ni mengine. Rais anaagiza kwamba watu watengewe maeneo ya kufanyia biashara, hakuna maeneo ya kufanyia biashara kila siku watu hawa wanaishi kama swala anayemuogopa simba katika Taifa hili. Hatuwezi kupeleka Taifa hili mbele, ile sekta ni muhimu sana na ina uwezo ikitumika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimekuwa Meya katika Halmashauri yangu najua ikitumika vizuri ina uwezo wa kulitoa Taifa hili hapa kulipeleka mahali pengine na wana uwezo hao kuwekeza vizuri katika eneo la viwanda. Kwa hiyo, ni vizuri mtengeneze mkakati thabiti wa kuwasaidia hawa watu kule chini. Toeni maelekezo kwa Wakurugenzi wawe creative, wabuni namna gani wawasaidie wale wafanyabiashara rather than kuwapiga na kuwasumbua katika maeneo yao wanayofanyia biashara ili nao waishi kama Watanzania wengine na wapate faida ya matunda haya tunayotaka kuyafikia ya lengo la kuwa na Tanzania mpya ya viwanda. Nilidhani hiyo sekta ni muhimu sana na muione kama engine muhimu sana inayoweza kutusaidia kufika tunapotaka kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nizungumzie kidogo kwenye suala la forward and backward linkage ya sekta zetu. Bado tuna tatizo kama wengi walivyosema la kilimo, ni vizuri tuone sasa kwamba kama tunataka kweli kufika kwenye viwanda pamoja na matatizo hayo huko nyuma ambayo tunaweza tukayarekebisha, lakini ki ukweli ni lazima tukiinue kilimo chetu kiwe ni kilimo chenye sura ya viwanda. Kama hatutafanikiwa hili bado tutaimba tu viwanda na hatutafikia lengo. Bila kumung‟unya maneno…
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha hoja yangu, ahsante sana.