Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Labda kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujaalia afya njema na kuweza kukutana kuzungumza mambo mbalimbali ya nchi yetu. Pili niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Tanga Mjini ambao wameniwezesha nirudie mara kwa mara kuwa Mbunge wa kwanza wa Upinzani kufika katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, vilevile pia niwashukuru wazazi wangu kwa namna walivyonilea mpaka nikakubalika.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, hebu ili taarifa zetu zikae vizuri, wewe ni Mbunge wa kwanza wa Upinzani, au Mbunge wa kwanza wa Upinzani kutokea Tanga? Ili taarifa zikae vizuri kwenye Taarifa zetu Rasmi za Bunge.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mbunge wa kwanza wa Upinzani katika Jiji la Tanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nianze kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nachangia katika bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nianze kwanza na suala la vijana. Vijana kuna usemi unaosema kwamba ni Taifa la kesho, lakini mimi niseme vijana ni Taifa la leo. Kwa nini nasema hivyo? Nina mifano ya kutoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi nyingi duniani katika masuala ya maendeleo, katika masuala labda ya michezo, katika masuala ya uzalishaji mali kwa mfano ajira viwandani, wanaoajiriwa kwanza ni vijana. Hata hapa tulipofikia leo sisi Tanzania, vijana ndio wanaokuwa ni nguvukazi, wana nguvu ya kufanya mambo ambayo yanaweza kuipeleka nchi mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, muda siyo mrefu tulizungumzia masuala ya vilabu vyetu, ukitazama kwa mfano Klabu ya Simba, vijana wale wa kikosi kipana cha Simba, ndio waliowezesha kuifanya Simba ifanye vizuri kuweza kuipiga JS Saoura, kuifuga AS Vita kuzifunga Al-Ahaly kwa sababu ni vijana wana nguvu. Pia kwa Taifa Star. Taifa Star wamefanya vizuri kuipiga Uganda bao tatu bila kwa sababu ni vijana wenye nguvu ambao wameandaliwa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nami naishauri Serikali yetu vijana tuwaandae vizuri ili tuweze kuwatumia katika nguvu kazi ya Taifa letu. Kwa mfano, leo Tanzania tuna maeneo mengi sana ya mapori ambayo hayajatumika, ajira zimekuwa zikikosekana. Kama Serikali itaweka mipango mizuri ya kuweza kuwatumia vijana, tukaweza kuwawezesha kwa vifaa, mitambo na mashine mbalimbali pamoja na mitambo hii ya irrigation, tunaweza kabisa kujizalishia chakula ambacho kitaweza kututosheleza nchi yetu na nchi jirani tutaweza kuwauzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa imekuwa kuna tatizo kidogo ambalo mimi naliona. Kwa mfano, kwenye masuala ya Kambi za JKT vijana zamani walikuwa wakimaliza Darasa la Saba asilimia kubwa wanapelekwa kwenye Kambi za JKT. Sasa hivi kuipata nafasi ya kuingia JKT imekuwa ni shughuli. Lazima pawe na mipango ya chini kwa chini, pawe na undugunaizesheni, pawe na ujamaa ndiyo mtu ataweza kuingia katika Kambi za JKT.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hili siyo sawa hata kidogo. Wale wengi ambao wanashindwa kufaulu mtihani wa Darasa la Saba, kwenda Form One, wale ambao wanashindwa kufaulu mtihani wa Form Four kwenda Form Five, Form Six, naamini kama tungewawekea mazingira mazuri, tukawapeleka katika Kambi zetu za JKT wakajifunza huko uashi, ufundi umeme, kilimo cha kisasa, mechanics na aina mbalimbali ya ufundi hata kuchomelea (welding) na mambo mengine, tungekuwa na jeshi kubwa la vijana ambalo lingeweza kuwa la uzalishaji mali. Sasa hivi imekuwa ni kinyume. Kwa hiyo, naishauri Serikali kwamba tuiangalie upya taratibu za kujiunga na JKT.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi, kwenye Sekta ya Walemavu; Tanzania tunao walemavu. Naishukuru Serikali kwamba angalau tunajitahidi sasa katika makusanyo ya kila Halmashauri, 2% ya kati ya zile 10% inakwenda kwa walemavu; 4% kwa akina mama, 4% kwa vijana. Hivi tukiulizana hapa Waheshimiwa Wabunge, ni kweli hizi fedha zinapelekwa huko kwa walemavu hizo 2%? Ni kweli zinapelekwa kwa vijana hiyo 4%? Kidogo angalau kwa akina mama, lakini kwa vijana bado. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba hizi asilimia za mapato, lazima Halmashauri tuzisimamie vizuri tuhakikishe kwamba hizi fedha zinakwenda; vijana na akina mama na walemavu wapatiwe hizi fedha. Kwa sababu kama watapatiwa hizi fedha, Watanzania wana upeo wa kuelewa mambo haraka. Kama watawezeshwa, wataweza kuzitumia vizuri, zitaweza kuwasaidia katika maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo walemavu wengine ambao ni mafundi viatu, wengine ni mafundi vyerahani tena wanawaajiri na wenzao, lakini mitaji wanakuwa hawana. Sasa niseme tu kwamba tuwawezeshe...

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mussa Mbarouk, kuna taarifa.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Ahsante.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge wa Tanga kwamba Bunge lililopita ziligawiwa hapa Kamusi za Kiswahili na lugha sahihi ya kutumia hapa ni kwamba ni watu wenye ulemavu, sio watu lemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Ahsante. Naibu Waziri

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbarouk, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeipokea. Watu wenye ulemavu, sio walemavu, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami niombe tuwasaidie hawa wenzetu kwa sababu, sisi tuliokuwa wazima hatukuwa na mipango na Mwenyezi Mungu kwamba tuwe wazima na wale wenzetu waliokuwa wenye ulemavu sio kwamba kuna kitu wamekosea. Kwa hiyo, tuwaangalie kwa jicho la huruma na tuwasaidie pale inapobidi kihalisia, siyo iwe kimaneno maneno tu, kwamba tukija humu tunaambiana maneno, lakini ukirudi huko unamkuta mlemavu anakwambia Mheshimiwa Mbunge kama ungenipatia mashine ya cherehani, ungenipatia na ngozi na uzi ningewaajiri vijana wenzangu hapa wenye ulemavu wanne, watano. Sasa tuwasaidie kama inavyotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye suala la wazee. Sote sisi hapa ni wazee watarajiwa lakini cha kushangaza, ukienda kwa wazee unaambiwa watatibiwa bure. Wameandaliwa vitambulisho, wamelipa shilingi elfu elfu lakini ama akienda hospitalini au kwenye Kituo cha Afya, ataishia kuandikiwa tu dawa aambiwe hizi kanunue. Mzee huyu kipato chake kimeshakuwa kidogo kwa sababu hizo pensheni zenyewe pia wanazopewa hapewi moja kwa moja hiyo shilingi 66,000/= analimbikiziwa baada ya miezi mitatu ndiyo apewe. Kwa hiyo, hana uwezo hata wa kununua ile dawa anayoandikiwa. Niseme, hawa wazee kama tumeamua watibiwe bure, akina mama wajawazito na watoto basi iwe wakienda wanapata dawa zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC tumekwenda kutembelea bohari la madawa MSD Dar es Salaam, tumekuta kuna madawa mengi mpaka yanafikia ku-expire kwa sababu hayafikishwi kule kunakohitajika. Tulipowahoji wataalam wetu, wanasema Madaktari wa Wilaya, na wa mikoa dawa nyingine hawaziombi. Kwa mfano, dawa za nyoka, dawa za mambo mengine, sukari na nini haziombwi, kwa hiyo, zinakaa mpaka zina- expire. Tungezipeleka kule ili hawa wazee na akina mama na watoto wanaotakiwa kutibiwa bure, zi-expire huko huko kwenye Vituo vya Afya sio zi expire pale MSD. Kwa hiyo, nasema wazee wetu watibiwe bure.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta amekwenda labda mzee, mwanamke ana cheni ya dhahabu. Daktari anamwambia ah, wewe unataka kutibiwa bure, mbona una cheni ya dhahabu? Sasa kwani cheni ya dhahabu ni dhambi? Si Sera ya Taifa kwamba wazee watibiwe bure? Ama amekwenda na gari, au amekwenda na taxi, sera inasema atibiwe bure.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Taarifa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, lingine niende kwenye hali ya kiuchumi. Kwenye kitabu cha Waziri Mkuu ukurasa wa 11.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mussa Mbarouk, kuna taarifa. Sasa kengele ya pili imeshagonga. Nitakuongezea dakika moja ili umalizie.

Mheshimiwa Ummy, Taarifa.

T A A R I F A

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa taarifa Mheshimiwa Mussa Mbarouk kwamba, sera kuhusu matibabu bure kwa wazee ni kwa wazee wasio nauwezo na sio kila mzee anatakiwa kupata matibabu bure, ni mzee asiye na uwezo. Niliona nitoe taarifa hiyo.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mussa Mbarouk unaipokea taarifa hiyo?

MHE. MUSSA MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenda suala la kiuchumi, pato la Taifa limekuwa kwa 6.7% mwaka 2018 na 6.2% kwa mwaka 2017, lakini niseme linakuwa katika makaratasi lakini kihalisia ukiwatazama watanzania huko nje wako hoi bin taabani…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)